Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme. Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni 26 Novemba 2023

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini yanayopata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka! Mashuhuda wa Matumaini na umuhimu wa kuyakoleza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo wa II, Muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Huu ni utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Majadiliano kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na vijana wa kizazi kipya, waliompenda upeo, ni ushuhuda unaojionesha hadi wakati huu kutokana na maadhimisho ya Siku za vijana kitaifa na kimataifa. Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mwanga wa upendo wa Mungu wenye huruma, alipata mang’amuzi ya pekee kuhusu uzuri na utakatifu wa wito wa watu wa Mungu; akatambua umuhimu wa watoto katika jamii, vijana sanjari na watu wazima. Aliangalia muktadha wa hali za kitamaduni na kijamii. Haya ni mambo ambayo kila mtu aliweza kuyafanyia majaribio na hata vijana wa kizazi kipya wanaweza kuyafanyia mang’amuzi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa sasa vijana wengi wanafahamu historia ya maisha sanjari na mafundisho yake msingi ambayo yanaweza kupatikana kwa njia ya mitandao ya kijamii. Kila kijana anachukua ndani mwake chapa ya tunu msingi za familia yake, hii ndiyo tabia ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Mafundisho yake ni msingi thabiti na rejea yenye uhakika inayoweza kumsaidia kijana kupata suluhu halisi ya matatizo na changamoto mbalimbali za maisha ambayo familia mbalimbali zinakumbana nayo katika ulimwengu mamboleo. Ujana ni wakati uliosheheni matumaini na ndoto, unaochochewa na mambo mengi mazuri yanayoboresha maisha ya binadamu: Fahari ya kazi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, ni wakati wa kukuza mahusiano na marafiki na wapendwa; kwa kujaliwa kukutana: na sanaa na tamaduni, sayansi na teknolojia, pamoja na kukoleza jitihada za binadamu za kufanya kazi kwa amani, haki ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni Ngazi ya Kijimbo
Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni Ngazi ya Kijimbo

Maadhimisho ya Siku ya 38 ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12 na siku hii inaadhimishwa tarehe 26 Novemba 2023 sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Ufalme wa haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema. Huu ni mwaliko kwa vijana kushirikishana matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu anasema chimbuko la matumaini ya Kikristo linabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; Mashuhuda wa matumaini; Matumaini yanayong’ara katikati ya usiku wa giza; Umuhimu wa kukoleza matumaini kwa kuwasha mwenge wa matumaini. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakumbuka Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Haya ni maadhimisho yaliyogubishwa na hofu, mashaka na wasi wasi mkubwa kutokana na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, lakini Mama Kanisa akasimika matumaini yake kwa Kristo Yes una hivyo kufanikiwa kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia Jimbo kuu la Lisbon nchini Ureno, na hapo kukalipuka mwanga na furaha. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 itaadhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake.

Maadhimisho ya Siku ya 37 Jimbo kuu la Lisbon, Ureno
Maadhimisho ya Siku ya 37 Jimbo kuu la Lisbon, Ureno

Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Siku ya 41 ya Vijana Ulimwenguni itaadhimishwa Jimbo kuu la Roma kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho haya. Anasema, Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema vijana ni chemchemi ya furaha na matumaini ya Kanisa na ulimwengu unaosafiri. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “furaha na matumaini (Gaudium et spes), uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao.” Gaudium et spes, 1. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kwanza kutafakari: “Kwa tumaini, mkifurahi” Rum 12:12, baadaye watazama zaidi katika maneno ya Nabii Isaya anayesema, wale wamtumainio Bwana watapiga mbio, wala hawatachoka. Rej. Is 40:31. Kimsingi anasema Mtakatifu Paulo, furaha na matumaini yanabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka; kwa mwamini kukutana na Kristo Yesu na kwamba, furaha na matumaini haya yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waamini kutambua kwamba, wanapendwa na Mungu na kwamba matumaini ni matunda ya imani kwa kutambua kwamba, kama mwamini anakubalika na kupendwa licha ya mazingira magumu na tete yanayomzunguka mwamini. Imani inamwezesha mwamini kuwa na furaha ya ndani anasema Baba Mtakatifu Benedikto XVI.

Ujana ni moto wa kuotea mbali, lakini fainali ni uzeeni
Ujana ni moto wa kuotea mbali, lakini fainali ni uzeeni

Ujana ni moto wa kuotea mbali; ujana ni wakati uliosheheni matumaini na ndoto, unaochochewa na mambo mengi mazuri yanayoboresha maisha ya binadamu: Fahari ya kazi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, ni wakati wa kukuza mahusiano na marafiki na wapendwa; kwa kujaliwa kukutana: na sanaa na tamaduni, sayansi na teknolojia, pamoja na kukoleza jitihada za binadamu za kufanya kazi kwa amani pamoja na haki ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Jamii inaishi katika ulimwengu ambamo matumaini ni haba “kama kiatu cha raba” kutokana na kinzani, migogoro na vita; Uhalifu, unyanyasaji na ukatili wa mitandaoni “cyber bullism” mambo yanayowafunga watu wa Mungu kiasi cha kushindwa kuona mwanga wa matumaini na matokeo ni idadi kubwa ya vijana kujinyonga kwa kukosa matumaini. Lakini binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe, waamini wanaweza kuwa ni kielelezo cha huruma na upendo wake wa daima, kama wanavyoshuhudia mashuhuda wa matumaini hata katikati ya ubaya, wao wakaweza kutangaza na kushuhudia matumaini: Mtakatifu Josephina Bakhita; Wenyeheri Józef, Wiktoria Ulma pamoja na watoto wao saba kutoka Poland. Hawa ni mashuhuda wa matumaini ya Kikristo ambayo ni sehemu ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo. Matumaini ni chumvi ya maisha ya kila siku, ni mwanga unaongaa gizani kama inavyojidhihirisha wakati wa Ijumaa kuu, Jumamosi Kuu pamoja na Dominika ya Pasaka ambayo inageuka kuwa ni Sherehe ya matumaini ya Kristo Kristo Yesu Mshinda, mwaliko kwa waamini kubaki wamejikita katika matumaini, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Matumaini kwani pale Mlimani Kalvari aliamini kwa kutarajia yasioweza kutarajiwa. Rej. Rum 4:18. Mwanga wa matumaini ya ufufuko wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu kamwe haukuzimika, licha ya kimya kikuu Jumamosi kuu, lakini Kristo Yesu, ameshinda dhambi na mauti. Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika imani na mapendo kielelezo makini cha Kristo Mfufuka.

Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa furaha na matumaini
Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa furaha na matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kurutubisha matumaini yao kwa Roho Mtakatifu kwa njia ya sala inayosaidia kukuza matumaini na uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu daima anawasikiliza na kujibu sala za waja wake. “Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ngome yangu, sitatikisika sana.” Zab 62:6. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kushirikishana matumaini na jirani zao na kuendelea kuwasha tochi ya matumaini ambayo ni Kristo Yesu, kwani kwa njia ya Ufufuko wake, maisha ya waamini yanapata mwanga mpya. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kutangaza na kushuhudia furaha na matumaini yanayosimikwa katika imani kila mtu kadiri ya hali na nafasi yake. Waamini wanaweza kuwa wenye furaha kwa kushirikishana na jirani zao neema na baraka kila siku ya maisha yao, kwani matumaini ya Kikristo yanapaswa kuwakumbatia na kuwaambata wote. Huu ni mwaliko wa kuonesha upendo na mshikamano kwa wale wanaoonekana kucheka na kutabasamu kwa nje, lakini kwa ndani wanawaka moto wa chuki na hasira. Vijana kamwe wasiruhusu kumezwa na utandawazi, uchoyo na ubinafsi usiojali wala kuguswa na mahitaji ya jirani, bali wajitahidi kuwa wazi kama mirefeji ya matumaini inayoyotiririkia katika medani mbalimbali za maisha na kwamba, Kristo anaishi na Yeye ndiye tumaini la vijana na uzuri wa ulimwengu huu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana na wale wote wanaojihusisha na utume pamoja na shughuli za kichungaji kwa vijana Wosia wa kitume wa “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ambao umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi!

Ujumbe Siku ya Vijana 2023

 

23 November 2023, 15:40