Utume na Maisha ya Kipadre: Sala, Neno la Mungu, Ekaristi Na Huduma Kwa Watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Kumbe, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika ngazi mbalimbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, mwaka 2024 litaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa na wasimamizi wa Kongamano hili ni Mwenyeheri Carlo Acutis na Mtakatifu Manuel Gonzales, mashuhuda wa Ibada ya Ekaristi Takatifu, waliofanikiwa kupiga magoti na kumwabudu Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Huu ni mwaliko wa kushikamana na maskini na wale wote wanaoteseka nchini Marekani katika huduma. Huu ni utume unaowataka Mapadre kujikita katika Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Ukarimu wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwafungulia watu malango ya matumaini. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre kutoka Hispania wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Marekani, walipomtembelea mjini Vatican, Alhamisi tarehe 16 Novemba 2023.
Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na sala kama nyenzo msingi za maboresho ya maisha na utume wa Kipadre. Mtakatifu Manuel Gonzales katika maisha na utume wake, alitoa mwaliko kwa waamini wake kusimama kidete kulinda na kudumisha haki jamii kama njia ya kumsindikiza Kristo Yesu katika njia yake ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Hii ni changamoto makini ya kupambana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, mwingiliano wa tamaduni pamoja na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu nchini Marekani, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anaambatana nao hadi utimilifu wa dahali. Mapadre wawe tayari kuwapokea na kuwahudumia watu wa Mungu wanaohitaji huduma ya maisha ya kiroho. Wajitahidi kusimika maisha yao katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu, upendo na ukarimu wa udugu wa kibinadamu pamoja na kujitahidi kuwafungulia watu wa Mungu malango ya maisha yao, wale wote wanaotafuta huduma za kiroho. Mapadre wawe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu wanaowahudumia, wajenge maisha, sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji katika wongofu wa kichungaji unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!