Jubilei ya Miaka 800 ya Kanuni ya Mtakatifu Francisko wa Assisi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tarehe 29 Novemba 2023 Familia ya Wafranciskani imesherehekea kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Papa Honorius III alipopitisha Kanuni iliyotungwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Hii ni Kanuni ya utii kwa Injili na Kanisa la Kristo. Kanuni hii ni mwangwi wa hija ya maisha ya kiroho iliyotekelezwa na wafuasi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Kanuni hii ni mwongozo wa maisha na utume wa Wafranciskani unaokita mizizi yake katika Injili, Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Useja na Ufukara chachu ya ujenzi wa maisha ya udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Papa Honorius III alipopitisha Kanuni ya Wafranciskani anasema, Jubilei hii ilete upyaisho wa ndani kwa kujikita katika mchakato wa kimisionari kwani wameitwa na kutumwa ili kwenda kukutana na walimwengu wanaongojea kufarijiwa, kupendwa na kutunzwa. Hii ni changamoto kwa Wafranciskani kujikita katika ufukara, unyenyekevu na katika Injili ya Kristo Yesu. Kanuni hii ni mwaliko kwa Wafranciskani kujitahidi kumwilisha Injili ya Kristo Yesu mintarafu Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Useja na Ufukara, huku Kanisa la Kristo Yesu likipewa kipaumbele cha kwanza ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, ili pamoja na Kristo Yesu daima furaha iweze kuzaliwa upya. Rej. Evangelii gaudium, 1.
Huu ni mwaliko kwa Wafranciskani na watu wenye mapenzi mema kujerejea tena na tena katika dhamana na wajibu wao waliojitwalia wakati walipobatizwa. Kumbe, Kristo Yesu ni kiini pia cha tasaufi ya Kifranciskani, mwaliko wa kuendelea kujifunza Kanuni na Maisha daima wakionesha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake. Mtakatifu Francisko wa Assisi alipenda kuonesha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa mintarafu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anawaalika Wafranciskani kumwilisha Kanuni yao kwa kujikita katika utamaduni wa kusikilizana na majadiliano katika ukweli na uwazi kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Wajitahidi kuboresha maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao hata kama itawagharimu, wakumbuke na kutambua kwamba wanaitwa na kutumwa kwenda Ulimwenguni kutangaza Habari Njema ya Wokovu.
Kanuni ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ilitoa changamoto kwa Wafranciskani kuzunguka Ulimwengu mzima, huku akiwasihi wasigombane, waepukane na mabishano na wala wasiwahukumu wengine. Wajitahidi kuwa wapole, watulivu na wenye kiasi; wanyenyekevu, wakizungumza kwa unyoofu na watu wote. Nyumba yoyote watakayoingia, na waseme kwanza: Amani iwe kwa nyumba hii. Kwenda Ulimwenguni kote ni kutambua wito wa Kifranciskani unaojikita katika mtindo wa udugu wa kibinadamu na maisha ya amani, bila ugomvi au malumbano kati yao; waendelee kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, kwa upole, huku wakitangaza amani ya Bwana, kama sehemu ya mpango wa uinjilishaji unaowezekana kutekelezwa na wote. Mchakato wa uinjilishaji wa Kifranciskani unalenga kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu; na kuendelea kujikita katika ushuhuda wa maisha yanayozungumza; upendo unaotolewa kama zawadi katika huduma kwa wadogo na maskini, ambao katika maisha na utume wao wanapewa kipaumbele cha kwanza na kwamba wanasimama kidete kutangaza na kushuhudia ile furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. “Katika uaminifu kwa mfano wa Kristo Yesu, ni muhimu kabisa kwa Kanisa leo hii kwenda mbele na kuhubiri Injili kwa watu wote; mahali pote, wakati wote, bila wasiwasi, bila kusita au kuogopa. Furaha ya Injili ni kwa ajili ya watu wote: hakuna awezaye kutengwa.” Evangelii gaudium, 23.
Kumbe, hii ni changamoto anasema Baba Mtakatifu Francisko ya kutoka ili kwenda ulimwenguni kutangaza na kushuhudia Injili katika ulimwengu ambamo kuna vita na mipasuko ya kijamii; uchoyo na ubinafsi; unyonyaji na matumizi mabaya ya rasilimali za dunia sanjari na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote pamoja na maskini. Kwa hali na mazingira kama haya Injili ni Habari Njema kwa watu kama hawa, ili waweze kupata ujasiri wa kutembea na kumwendea Kristo Yesu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakabidhi Wafranciskani dhamira ya kutambua njia sahihi za kufuata mintarafu ujasiri na uaminifu wa karama waliyopokea. Amewawekwa Wafranciskani wote chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria na ya watakatifu Francisko wa Assisi na Klara na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!