Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa salam na matashi mema kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, CBCK., kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia. Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa salam na matashi mema kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, CBCK., kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia. 

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidipomasia Kati ya Vatican na korea ya Kusini

Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Korea ya Kusini na Vatican zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa salam na matashi mema kwa Askofu Matthias Lee Yong-hoon Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, CBCK, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Korea ya Kusini na Vatican: Haki, Amani na Maridhiano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia inafuata kwa makini sana sheria, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78. Amani ya kweli inakolezwa katika urafiki wa kidugu. Upatanisho ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya mbeleni na unafumbatwa katika toba, msamaha na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, chemchemi ya haki na amani ya kudumu.

Ibada ya Misa Takatifu Kumbukizi ya Miaka 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia
Ibada ya Misa Takatifu Kumbukizi ya Miaka 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko, kinzani na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani!

Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Korea ya Kusini na Vatican zilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia kunako tarehe 11 Desemba 1963. Tangu wakati huo uhusiano huu umedumishwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kufanya hija za kitume nchini humo kunako mwaka 1984 na Mwaka 1989; Na Baba Mtakatifu Francisko kutembea Korea ya Kusini mwaka 2014 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia. Na itakumbukwa kwamba, Vatican ilichangia sana kwenye Umoja wa Mataifa mwaka 1948 ili Korea ya Kusini iweze kutambulika kuwa ni Taifa huru. Ni katika muktadha wa Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Korea ya Kusini na Vatican zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa salam na matashi mema kwa Askofu Matthias Lee Yong-hoon Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, CBCK, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Korea ya Kusini na Vatican. Ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa neema na baraka ambazo watu wa Mungu Korea ya Kusini wamezipata katika kipindi cha miaka 60. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa kuenea kwa Injili; kukua na kukomaa kwa Kanisa nchini Korea ya Kusini sanjari na mchango wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Korea ya Kusini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba mahusiano haya yataendelea kuzaa matunda ya kitamaduni na kiroho hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu anakumbuka kwa moyo wa shukrani hija yake ya kitume aliyoifanya nchini Korea ya Kusini kunako mwaka 2014 ili kuwatangaza watakatifu Mashuhuda wa Imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake na leo hii Kanisa linaendelea kukua na kupanuka.

Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kato ya Vatican na Korea ya Kusini
Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kato ya Vatican na Korea ya Kusini

Vijana wa kizazi kipya ni warithi wa mashuhuda wa imani na kwamba, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana hawa watakuwa ni mashuhuda wa kutukuka wa Kristo Yesu wakati huu, wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 yatakayo adhimishwa Jimbo kuu la Seoul nchini Korea Kusini, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa na ndoto ya umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, ndoto ambayo vijana wa kizazi kipya ni mashuhuda wake. Ni matumaini makubwa ya Baba Mtakatifu kwamba, uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili utaendea kuchanua kwa kufanya kazi kwa pamoja katika mustakabali wa haki, amani na maridhiano kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Korea ya Kusini. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu amewaweka watu wa Mungu nchini Korea ya Kusini chini ya ulinzi na tunza ya Mashahidi wa imani kutoka Korea ya Kusini pamoja na Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa na mwisho amewapatia baraka zake za kitume. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Monsinyo Fernando Duarte Barros Reis, Afisa mwandamizi kutoka Ubalozi wa Vatican nchini Korea ya Kusini. Kwa upande wake, Askofu Matthias Lee Yong-hoon Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini, CBCK, amegusia mchango wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948 na kwamba, nchi hizi mbili zitaendelea kushirikiana na kushikamana ili kudumisha uhusiano huu mwema, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu.

Diplomasia ya Vatican inalenga kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano
Diplomasia ya Vatican inalenga kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Kumbukizi ya miaka 60 tangu Korea ya Kusini na Vatican walipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Amekazia umuhimu wa kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Korea ya Kusini na Kaskazini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Naye Yu In-chon, Waziri wa Utamaduni kutoka Korea ya Kusini amesema, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Korea ya Kusini na Vatican umepata mafanikio makubwa kwa sababu unasimikwa katika hali ya kuaminiana na urafiki wa kijamii, kwa ajili ya kuganga na hatimaye, kuponya madonda ya utengano.

Korea 60 Yrs

 

12 December 2023, 14:49