Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maana, Historia na Umuhimu wa Pango la Noeli: Fumbo la Umwilisho

Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu, ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Pango la Noeli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anafafanua kwa kina kuhusu: Pango la Noeli, Asili yake, Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kuhusu Pango kama ishara ya uinjilishaji pamoja na alama za Pango la Noeli. Pango la Noeli ni mchakato unaojikita katika kueneza na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutafakari na kuhisi na kuonja uwepo wa Mungu kwa binadamu; kuhisi na kuonja uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Kwa Waraka huu wa Kitume, uliochapishwa tarehe 1 Desemba 2019, Papa Francisko anapenda kuwahamasisha waamini kuendeleza Mapokeo ya kuandaa Pango la Noeli kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, magerezani na kwenye maeneo ya wazi, kama kielelezo cha ibada katika Fumbo la Umwilisho.

Pango la kwanza lilitengenezwa 29 Novemba 1223
Pango la kwanza lilitengenezwa 29 Novemba 1223

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Bethlehemu pamoja na picha alizowahi kuona kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Alilitengeneza Pango la Noeli, Siku 15 kabla ya Sherehe ya Noeli kama kumbukumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho. Ilikuwa ni tarehe 25 Desemba 1223 watawa Wafranciskani kutoka sehemu mbalimbali za dunia walipofika kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio. Pango likapambwa kwa uwepo wa mahujaji na wanyama mbalimbali na Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa Pangoni humo, ili kuonesha uhusiano wa dhati kati ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Huu ndio ukuu na utakatifu wa Fumbo la Umwilisho, mwaliko kwa waamini kuamsha tena mshangao kwa unyenyekevu wa Mungu aliyefanyika Mtoto!

Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli
Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli

Mara ya kwanza, Pango la Noeli halikuwa na sanamu mbalimbali kama zinavyonekana wakati huu. Pole pole, Pango la Noeli likapambwa kwa Sanamu ya Mtoto Yesu aliyelazwa kwenye hori la kulishia wanyama. Na wote walioshuhudia tukio hili wakarejea makwao wakiwa wamesheheni furaha kubwa nyoyoni mwao. Haya ni matunda ya uinjilishaji uliofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, kiasi kwamba, mafundisho yake, hadi leo hii yanaendelea kugusa sakafu ya maisha ya waamini kwa njia ya imani. Madhabahu ya Greccio yamekuwa ni kimbilio la watu wanaotaka kusali na kutafakari katika hali ya utulivu na kimya kikuu. Pango la Noeli anasema Baba Mtakatifu, ni kielelezo cha upendo wa Mungu; zawadi ya maisha inayokumbatia udugu na urafiki unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye pia ana uwezo wa kuwasamehe watu dhambi zao na kuwaweka huru! Injili na Pango la Noeli ni msaada mkubwa katika kulitafakari Fumbo la Umwilisho, kwa kugusa nyoyo za watu na hivyo kuwazamisha katika historia ya wokovu katika muktadha wa mazingira na tamaduni za watu. Huu ni mwaliko wa “kugusa na kuhisi umaskini wa Mwana wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, ili kuchuchumilia na kuambata njia ya unyenyekevu, ufukara na sadaka ili kufuata ile Njia ya Msalaba kutoka mjini Bethelehemu hadi mlimani Kalvari.

Pango la Noeli lina amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume Kanisa
Pango la Noeli lina amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume Kanisa

Ni katika muktadha wa Pango la Noeli, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wasanii wanaoshiriki katika Pango Hai la Noeli kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, mahali ambapo pamehifadhiwa “Masalia ya Pango Takatifu la Mtoto Yesu” kumbe, kuna uhusiano mkubwa kati ya Kanisa hili na Bethlehemu alikozaliwa Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka watu wa Mungu wanaoishi mjini Bethlehemu na katika Nchi Takatifu, mahali alipozaliwa Mtoto Yesu, akaishi, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Nchi Takatifu kwa sasa inakabiliwa na vita na madhara ya vita yanafahamika, changamoto na mwaliko kwa waamini kuonesha mshikamano wa pekee na watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na vita. Katika maeneo haya Sherehe ya Noeli inagubikwa na majonzi, misiba, bila ya uwepo wa mahujaji wala maadhimisho ya Ibada mbalimbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa liko pamoja na karibu nao kwa njia ya sala na kwamba, kuna machungu makubwa huko Mashariki ya kati na Ulimwengu katika ujumla wake, kutokana na vita. Mwishoni, amewataka wasanii hawa waweze kuiishi siku hii kwa imani, furaha na kwamba, iwe ni ushuhuda wa Injili.

Papa Pango la Noeli
16 December 2023, 15:24