Tafuta

Kutokana na Ibada kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko anasema, azikwe kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Kutokana na Ibada kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko anasema, azikwe kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma.  (Vatican Media)

Mahojiano Maalum Kati ya Kituo cha TV Mexico na Papa Francisko: Maziko na Hija 2024

Kutokana na Ibada kwa Bikira Maria, Papa anasema, azikwe kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Baba Mtakatifu kwa mwaka 2024 anatarajia kutembelea Ubelgiji, Argentina na kwenye Visiwa vya Olynesia vilivyoko kwenye Bahari ya Pacific. Ameandaa tayari mwongozo wa Ibada ya Mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Haya ni mambo makuu yaliyozungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahojiano maalum na Kituo cha televisheni cha Mexico, N Plus.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na Ibada kwa Bikira Maria, Baba Mtakatifu Francisko anasema, azikwe kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu kwa mwaka 2024 anatarajia kutembelea Ubelgiji, Argentina na kwenye Visiwa vya Olynesia vilivyoko kwenye Bahari ya Pacific. Ameandaa tayari mwongozo wa Ibada ya Mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanamfahamu fika na wanamchukulia jinsi alivyo na kwamba, afya yake inaendelea kuimarika, lakini bado anawaaomba waamini kumkumbuka na kumwombea ili Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia afya njema na kwamba, ni vyema kupokea zawadi ya maisha ya uzee! Haya ndiyo mawazo makuu ambayo yameelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari Valentina Alazraki kutoka Kituo cha Televisheni cha Mexico, N+ katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, “La Morenita” hapo tarehe 12 Desemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2023 anaadhimisha kumbukizi ya miaka 87 tangu alipozaliwa. Katika mahojiano haya anakiri kwamba anayo Ibada ya pekee sana kwa Bikira Maria na ndiyo maana amechagua kwamba, atakapofariki dunia, azikwe kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma. Hatua hii itakuwa ni mabadiliko makubwa katika historia ya Kanisa, kwani Mababa watakatifu wengi wamezikwa ndani ya Makaburi ya Vatican yaliyoko ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Baba Mtakatifu Benedikto XVI ndiye Papa wa mwisho kuzikwa ndani ya Makaburi ya Vatican. Tangu mwaka 2013, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mara 115 na mara ya mwisho ni tarehe 8 Desemba 2023 alipokwenda kuweka shada la waridi ya dhahabu kwenye Picha ya Bikira Maria, Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” ambayo kadiri ya Mapokeo ya Kanisa picha hii ilichorwa na Mtakatifu Luka. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa miaka mingi amekuza Ibada ya pekee kwa Bikira Maria.

Papa Francisko ana ibada ya pekee kwa Bikira Maria
Papa Francisko ana ibada ya pekee kwa Bikira Maria

Baba Mtakatifu kwa kushirikiana na washereheshaji wa Ibada za Kipapa wameandaa mwongozo wa Ibada ya mazishi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, mwongozo wa zamani mara ya mwisho kutumika ni wakati wa maziko ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 5 Januari 2023, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anakiri kwamba, alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI na mara nyingi alimwendea kuomba ushauri na kumpatia kwa kumwachia uhuru wa kutekeleza ushauri huo. Aliposikia kutoka kwa Muuguzi wake kwamba, hali ya Baba Mtakatifu Benedikto ilikuwa tete, wakati wa Katekesi yake ya mwisho kwa mwaka 2022 alimwombea na kwamba, alipata neema ya kumsindikiza Baba Mtakatifu Benedikto katika hatua yake ya maisha ya hapa duniani na baada ya siku tatu, akafariki dunia. Ni kiongozi aliyeonesha ujasiri baada ya kutambua udhaifu wake wa mwili, akaamua kung’atuka kutoka madarakani. Akaamua kusali kwa ajili ya Kanisa kwa kujichimbia kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” Kwa hakika aliishi katika kimya kikuu na maisha ya kawaida pasi na makuu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anayo desturi ya kwenda kusali kwenye Makaburi ya Mapapa anapita pia kwenye Kaburi la Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliyekuwa mwandani wake wa maisha, lakini kwa sasa amekuwa mbali. Pengine iko siku atafuta nyayo za Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa kung’atuka kutoka madarakani, lakini kwa sasa hana wazo wala mpango huo. Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikwisha kumkabidhi Kardinali Tarcisio Pietro Evasio Bertone, S.D.B., aliyekuwa Camerlengo wa Kanisa Katoliki, ikiwa kama angeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro angeweza kun’atuka kutoka madarakani.

Papa Kwa Mwaka 2024 anatembelea Argentina,  Ubelgiji na Olynesia
Papa Kwa Mwaka 2024 anatembelea Argentina, Ubelgiji na Olynesia

Barua hii itaendelea kuwepo, anatambua ujasiri wa Hayati Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI, lakini kwa sasa hana wazo wala mpango wa kung’atuka madarakani hadi pale Kristo Yesu atakapotaka mwenyewe. Baba Mtakatifu alipoulizwa kuhusu ukali wake mara baada ya kifo cha Benedikto XVI hasa kwa wapinzani na wakosoaji wake anasema, kuna baadhi ya watu anabidi awe mkali kidogo, lakini wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican ni wema na wanamwelewa na kwamba, kadiri mtu anavyozeeka anakuwa ni mpole na mtu mwema zaidi. Baba Mtakatifu ambaye kutokana na changamoto za afya, amewahi kufanyiwa upasuaji mkubwa mara mbili, anasema, kwa sasa afya yake inaendelea kuimarika ingawa anakiri kwamba, kimsingi afya yake ni dhaifu sana ndiyo maana anaendelea kuomba sala kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kwani magonjwa ni sehemu ya uzee. Kumbe, kuna haja ya kupokea zawadi ya uzee ambayo inawawezesha kutenda mengi. Katika maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kufanya mambo mengi, alama kwamba, afya yake inaendelea vizuri. Changamoto ya afya imemfanya Baba Mtakatifu Francisko ashindwe kuhudhuria mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu. Hija za Kitume za Baba Mtakatifu kwa Mwaka 2024 zinaendelea kufanyiwa marekebisho na kwamba, kwa sasa amepanga kutembelea Ubelgiji baada ya kupewa mwaliko na Mfalme Philippe pamoja na Malkia Mathilde, baada ya kukutana na kuzungumza pamoja tarehe 14 Septemba 2023. Nchi nyingine ni Visiwa vya Polynesia vilivyo kwenye Bahari ya Pacific. Rais Javier Milei wa Argentina amemwalika kutembelea Argentina. Mwaliko huu unakuja baada ya Baba Mtakatfu Francisko kuzungumza mubashara kwa njia ya simu na Rais wa Argentina. Wakati wa kampeni wanasiasa wanazungumza mambo mengi, lakini kile wanachofanya baada ya kushinda uchaguzi ni tofauti kabisa.

Papa Mahojiano
14 December 2023, 14:55