Mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko Mkesha wa Noeli, 2023: Upendo wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kanisa Katoliki kuhusu Fumbo la Umwilisho linasadiki na kufundisha kwamba: “Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.” Kristo Yesu alizaliwa katika utawala wa Kaisari Augusto aliyetaka iandikwe orodha ya majina ya watu wote ulimwenguni. Kwa maneno mengine, hii ilikuwa ni sensa ya idadi ya watu kama Mwinjili Luka anavyobainisha Lk. 2:1. Wakati Kaisari akifanya hesabu ya idadi ya watu ulimwenguni, Mwenyezi Mungu anaamua kuingia ulimwenguni katika hali ya kificho, wakati Mfalme alitaka kujimwambafai ili aonekane kuwa ni kati ya watu maarufu katika historia, Kristo Yesu Mfalme wa historia anaamua kujinyenyekesha na kuzaliwa kama Mtoto. Hakuna kati ya wakuu wa dunia waliotambua kuzaliwa kwake, lakini Habari Njema wanapewa kwanza wachungaji kondeni, watu waliokuwa wametelekezwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkesha wa Sherehe za Noeli kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2023. Baba Mtakatifu amekazia kuhusu hesabu ya idadi ya watu ulimwenguni, Fumbo la Umwilisho; Mungu kweli na Aliye hai, Ndiye aliyefanyika mwili na Kumwabudu Kristo Yesu ni kielelezo cha kumpokea.
Baba Mtakatifu Francisko anasema “dhana ya Sensa ya watu” inaacha ukakasi katika Maandiko Matakatifu. Mfalme Daudi alidhani kuwa na Idadi kubwa ingeonesha ufahari na ushujaa wake dhidi ya adui zake, lakini baada ya hesabu moyo wa Daudi ulihuzunika sana kwa sababu alimkosea Mwenyezi Mungu na adhabu yake ni kushambuliwa na ugonjwa wa tauni. Rej. 2Sam 24:1-9. Katika mkesha wa Noeli, Kristo Yesu, “Mwana wa Daudi” baada ya kukaa tumboni mwa Bikira Maria kwa muda wa miezi tisa, anazaliwa mjini Bethlehemu, mji wa Daudi, wala hakuna adhabu inayotolewa na Mungu. Huu ni ufunuo wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayefanyika mwili na hivyo kuingia katika udhaifu wa ulimwengu kwa kutangaza “Amani kwa watu aliowaridhia.” Lk 2: 14. Nyoyo za waamini katika mkesha wa Noeli zinaelekezwa mjini Bethlehemu ambako hadi leo hii, Mfalme wa amani bado anakataliwa kutokana na mantiki ya vita, mashambulizi ya silaha yanayomzuia hata leo hii, Kristo Yesu “kupata nafasi” ulimwenguni. Rej. Lk 2:7. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sensa ya watu ni ushuhuda wa sehemu ya binadamu katika historia yake anayetafuta madaraka na nguvu, umaarufu na utukufu; anayetafuta mafanikio ya chapuchapu na matokeo ya papo kwa hapo, kwa kuwa na takwimu pamoja na hesabu, kielelezo cha utendaji wake. Lakini katika sensa ya watu, Kristo anakuja ulimwenguni kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ili kuwatafuta waja wake, utendaji wa Mungu katika Fumbo la Umwilisho, anayetaka kutoa suluhu ya matatizo na changamoto za ulimwengu kwa njia ya upendo, kwa kufuata mipaka ya binadamu na kwa kutwaa hali na udhaifu wa binadamu.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na uelewa sahihi wa Mungu na kwamba, huyu si Mungu mwenye nguvu anayekaa mbinguni, anayekumbatia madaraka, mafanikio ya kidunia pamoja na ulaji wa kupindukia; Mungu anayejitambulisha na watu wabaya, Mungu aliyeumbwa kwa mfano wa binadamu, Mungu anayefaa pale tu anapotatua shida, magumu na changamoto za maisha ya binadamu. Lakini Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho amekuwa jirani sana na binadamu na hivyo kuweza kubadili ukweli kutokana katika undani wa maisha na kwamba, Mwenyezi Mungu amezaliwa kwa ajili ya watu wakati wa sensa ya idadi ya watu wote ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mungu kweli na aliye hai ameleta mabadiliko makubwa kwa kuishi ndani ya ulimwenguni, ndiye anayeondoa dhambi za ulimwengu kwa kuzibeba ndani mwake, ndiye anayegeuza mateso na mahangaiko ya binadamu sanjari na kutoa matumaini mapya kwa matatizo na changamoto zinazo mwandama mwanadamu, kwa kuwakumbatia wote katika udogo na haki yake, ili aweze kuwa haki kwa watu wa Mataifa. Mshangao wa Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaookoa ulimwengu, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Huu ni mwaliko kwa waamini kuangalia ishara: Mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, pamoja na hori la kulia ng’ombe; ufunuo wa Uso wa Mungu: mwingi wa huruma na mapendo; mwenye nguvu inayomwilishwa katika upendo. Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Rej Yn 1:14. Mwili ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu na Injili inabainisha kwamba, Neno wa Mungu ameingia katika undani wa hali na maisha ya mwanadamu, kwa sababu ya upendo wake mkuu, ambao hauna mipaka. Mwenyezi Mungu aliyeleta mageuzi makubwa katika sensa ya watu, anawadhihirishia waja wake kwamba, wao si namba, bali ni sura na mfano wa Mungu na kwamba, majina yao yameandikwa kwenye Moyo wa Mungu.
Huu ni ulimwengu unaohukumu na kushindwa kusamehe. Lakini, Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele amefanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika huzuni zake na hivyo kuiga mfano wa wachungaji kondeni, waliokwenda kwa haraka ili kukumbatia na kuambata upendo wa Mtoto Yesu, ambaye amekuja kuwaokoa na kwa njia hii, hawa wao watatambua kwamba, kwa hakika ni watoto wapendwa wa Mungu, kwani Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa amekuja kuwaangazia wanadamu katika maisha yao na macho yake yanang’aa upendo. Bethlehemu wakati wa sensa ya watu, ulisheheni watu wengi, lakini Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu, Wachungaji wa kondeni na baadaye Mamajusi kutoka Mashariki, ndio watu pekee katika umati mkubwa wa wale waliokuwa mjini Bethlehemu walioonesha ukaribu kwa Mtoto Yesu, kiasi hata cha kumwabudu. Baba Mtakatifu anasema, Ibada ya Kumwabudu Mtoto Yesu ni njia muafaka ya kulipokea Fumbo la Umwilisho, Neno wa Baba wa milele aliyefanyika mwili. Kuabudu ni kumwezesha Mwenyezi Mungu kuingia na kuishi katika maisha ya waja wake. Bethlehemu yaani “nyumba ya mikate” ni mwaliko kwa waamini kuwa ni “mkate unaomegwa kwa ajili ya upendo kwa wengine.” Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuifanya mbegu ya Fumbo la Umwilisho iweze kustawi ndani mwao, kwa kushirikiana na kazi ya Mwenyezi Mungu ambaye ni chachu inayobadilisha ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kuombea, kutengeneza na hivyo kumruhusu Mungu aweze kuinyoosha historia! Waamini wajenge utamaduni wa kupenda kuabudu Ekaristi Takatifu kwani ndani mwake mwamini anapata haiba, utukufu, heshima, uaminifu na njia ya kweli ya upendo wake wote duniani. Usiku wa kesha la Noeli unaonesha upendo unavyobadilisha historia. Waamini wana amini katika nguvu ya upendo wake tofauti kabisa na nguvu za ulimwengu. Huu ni mwaliko kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu, Wachungaji kondeni pamoja na Mamajusi kutoka Mashariki wakusanyike kumwabudu na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, waamini nao waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri wa Uso wa Mungu ulimwenguni.