Tafuta

Katika kipindi hiki cha kihistoria, Jumuiya ya Kimataifa inaitwa kuwajibika kwa urithi ambao itaacha katika ulimwengu huu. Katika kipindi hiki cha kihistoria, Jumuiya ya Kimataifa inaitwa kuwajibika kwa urithi ambao itaacha katika ulimwengu huu.   (COP28)

Matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mkutano wa COP28

Kardinali Pietro Parolin anaelezea kuhusu matumaini ya Papa katika mkutano wa COP28, Mkataba wa COP21 uliofanyika mjini Paris; Vita kati ya Israeli na Palestina; Urusi na Ukraine na diplomasia ya Vatican na kwamba, licha ya matatizo na changamoto za: vita, maadili na utu wema, athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kisiasa na kiuchumi, bado kuna matumaini makubwa ya kuweza kuboresha ulimwengu huu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi hiki cha kihistoria, Jumuiya ya Kimataifa inaitwa kuwajibika kwa urithi ambao itaacha katika ulimwengu huu. Ikiwa kama haitachukua hatua madhubuti kwa wakati huu, athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kusababisha maafa kwa mamilioni ya watu. #COP28. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28 huko Dubai, kuanzia tarehe 30 hadi tarehe 12 Desemba 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji. Watu wengi wanaathrika sana mintarafu afya ya binadamu, ukosefu wa fursa za kazi, upatikanaji wa rasilimali, makazi pamoja na uhamiaji wa nguvu. Haya ni matatizo ya kijamii yanayogusa na kutikisa utu, heshima, haki msingi na maisha ya binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani zimepelekea ongezeko la kiwango cha joto duniani na matokeo yake ni mvua kubwa zinazoambatana na mafuriko na sehemu nyingine ukame wa kutisha. Ongezeko la kiwango cha joto duniani kunapelekea kuyeyuka kwa barafu na matokeo yake ni ongezeko la kina cha maji baharini. Kumekuwepo na upinzani pamoja na hali ya kuchanganyikiwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari hali ambayo kwa siku za usoni, itawalazimisha watu kuhama kutoka kwenye fukwe za bahari. Taarifa kamili ya matokeo haya zinapaswa kutolewa na kwamba, waathirika wengi zaidi ni maskini, ingawa asilimia 50% ya watu matajiri na nchi tajiri ndio wanaochafua zaidi mazingira nyumba ya wote. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira, changamoto kwa wanasiasa na wafanyabiashara kutenda kwa haraka.

Kardinali Pietro Parolin anaongoza ujumbe wa Vatican COP28
Kardinali Pietro Parolin anaongoza ujumbe wa Vatican COP28

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anaongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu na anashiriki katika sehemu ya kwanza ya mkutano huu. Pamoja naye yupo Kardinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, M.C.C.I, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, anayejikita zaidi katika sehemu ya majadiliano ya kidini na tarehe 3 Desemba 2023 atazindua Banda la Imani kwenye Jiji la Expo, Dubai. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika sana kukosa fursa hii ya kushiriki moja kwa moja kwenye maadhimisho ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28 huko Dubai. Katika mahojiano maalum kati ya Kardinali Pietro Parolin na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anaelezea kuhusu matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano wa COP28, Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015; Vita kati ya Israeli na Palestina; Urusi na Ukraine na diplomasia ya Vatican na kwamba, licha ya matatizo na changamoto za: vita, maadili na utu wema, athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kisiasa na kuchechemea kwa uchumi, bado kuna matumaini makubwa ya kuweza kuboresha ulimwengu huu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anaonesha athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kazi za binadamu, hali ambayo inachangia kuporomoka kwa hali ya maisha ya mwanadamu, hususan maskini na wanyonge. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa kwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28 huko Dubai, 2023. Sera na mikakati ya kiuchumi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia haina budi kusindikizwa na mchakato wa elimu, mtindo bora zaidi wa maisha unaosimikwa katika upunguzaji mkubwa wa ulaji; upyaisho wa maendeleo fungamani ya binadamu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; ujenzi wa udugu wa kibinadamu; ushirikiano na mshikamano; upendo kwa Mungu na jirani walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mkutano wa COP28 Dubai, 2023
Mkutano wa COP28 Dubai, 2023

Tangu mwaka 1990 kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji wa hewa ya ukaa na matokeo yake mwaka hadi mwaka kumekuwepo na majanga makubwa kwa mfano: ni kuibuka kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Vita sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, baada ya Vita Kuu ya Dunia kuna haja ya kujenga na kudumisha: umoja, ushirika, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja. Vita kati ya Israeli na Palestina vilivyo anza kupamba moto tarehe 7 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, vitendo vya kigaidi na watu wenye misimamo mikali ya kiimani na kiitikadi, si suluhu ya changamoto kati ya Israel na Palestina, na matokeo yake ni kuongezeka kwa uhasama, chuki na vita na kwamba, watu wasiokuwa na hatia ndiyo wa kwanza kupoteza maisha. Uhusiano kati ya Palestina na Israeli umekuwa ukisuasua kwa miaka mingi na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi; na kwamba, uundwaji wa Mataifa mawili ndiyo suluhu ya mgogoro kati ya Israeli na Palestina. Majadiliano kati ya Misri, Qatar na Marekani pamoja na utashi wa Serikali ya Israeli kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wote wa vita ni jambo linalopaswa kupongezwa. Vita kati ya Israeli na Palestina huko Ukanda wa Gaza imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, kuna haja ya kuachana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha maisha. Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi sehemu mbalimbali za dunia hali ambayo inakinzana na imani pamoja na uhalisia wa maisha. Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi na kwamba, ziara ya Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia huko Ukraine na Urusi inaendelea kuzaa matunda. Ni matumaini ya Vatican kwamba, majadiliano yatafunguliwa pia katika maeneo mengine. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema kila tatizo linapaswa kuitwa kwa jina lake. Licha ya matatizo na changamoto za: vita, maadili na utu wema, athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kisiasa na kuchechemea kwa uchumi, bado kuna matumaini makubwa ya kuweza kuboresha ulimwengu huu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Matumaini yanahitaji ujasiri wa kuamua na kutenda; uthubutu wa kupiga moyo konde ili kuondokana na maslahi finyu ya kibinafsi au Kitaifa ili kuboresha hali ngumu, tayari kupanda amani kwa uvumilivu na uaminifu.

Parolin COP28
01 December 2023, 15:51