Mtakatifu Stefano Shahidi, Mbegu ya Toba na Wongofu wa Mt. Paulo, Mwalimu na Mtume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Desemba, anaadhimisha Sikukuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shuhuda wa kwanza mbinguni. Hii ni Sikukuu ambayo ina uhusiano wa pekee kabisa na Sherehe ya Noeli kwani Fumbo la Umwilisho linapata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Mtakatifu Stefano Shemasi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza. Huu ni utume ambao aliutekeleza kwa muda mfupi sana, ikilinganishwa na matumaini ya Mitume wa Yesu. Mtakatifu Stefano alikuwa ni mtu mwema, mwenye kujawa na Roho, na hekima. Alitenda maajabu na ishara, kisha akafungwa. Stefano Shemasi, akabahatika kuwa ni shuhuda wa Yesu pamoja na kupewa neema ya kutafakari utukufu wa Kristo Mfufuka, kiasi hata cha kutangaza Umungu wake. Kabla ya kifo chake, akajiaminisha kwa huruma na upendo wa Kristo Yesu. Katika mateso makali akathubutu kuwasamehe watesi wake, mbele ya Kristo Yesu, ili asiwahesabie dhambi hii, akiisha kusema haya akalala usingizi wa amani baada ya kupigwa mawe hadi kufa! Kwa ufupi sana, Mtakatifu Stefano ni mfano bora wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; msamaha, unyenyekevu na utii mfano wa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kwa hakika alikuwa ni shuhuda wa kito cha thamani, yaani imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Yote haya yanafanyika chini ya usimamizi wa kijana mmoja aliyejulikana kama Sauli: Hapa kuna muuaji yaani kijana Sauli na shuhuda wa imani, Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shuhuda.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 26 Desemba 2023, amemwelezea Mtakatifu Stefano kuwa ni shuhuda wa mwanga angavu unaong’aa gizani, kama ilivyo kwa Kristo Yesu: “Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yn. 1:9.5. Mtakatifu Stefano akashutumiwa kwa uwongo, akauwawa kwa kupiga mawe hadi kufa. Lakini katika giza la chuki na ubaya wa moyo, mwanga angavu wa Kristo Yesu, unachomoza gizani: akasali kwa ajili ya watesi wake na kuwasamehe. Akapata nguvu zote hii kutoka katika mwanga wa Kristo Yesu. Ni Shuhuda wa kwanza wa Kristo Yesu na Kanisa lake kati ya umati mkubwa wa waamini wanaoendelea kushuhudia mwanga katika giza la maisha ya mwanadamu hadi katika nyakati hizi. Hawa ni watu wanaojibu ubaya kwa kutenda wema; watu wasiojiruhusu kutumbukia katika vita wala uwongo, lakini wanajitahidi kuvunjilia mbali mnyororo wa chuki na uhasama kwa upole wa upendo. Mashuhuda hawa wanachomoza alfariji ya Mungu katika giza la ulimwengu. Kila Mkristo anahimizwa kuwa ni shuhuda amini wa Kristo Yesu, kwa kumfuasa Kristo kama alivyofanya Mtakatifu Stefano, mfano bora wa kuigwa. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi na kwamba Kristo Yesu anaishi ili kuhudumia kwa kuwa ni Shemasi, yaani msaidizi na mhudumu wa mezani.
Shuhuda ni mtu anayejitahidi kumuiga Kristo Yesu kila siku ya maisha yake, hadi siku ile kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, atakapokamatwa, kuhukumiwa na kufa nje ya mji, Yesu anasali kuwaombea watesi wake na hatimaye, kuwasamehe. Wakati wakimpiga kwa mawe Stefano, naye aliomba akisema: “Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala.” Mdo. 7:60. Baba Mtakatifu anakaza kusema katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya Kanisa kuwa na mashuhuda wanaothubutu kuendelea kusali na kusamahe, kama mfano bora wa kuigwa. Kati ya watu walioombewa na Stefano alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake. Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa; mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Paulo amezaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya huduma, sala, imani na ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anasema “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.” 1Kor 15:9-10.
Huu ni ushuhuda kwamba, matendo ya huruma na mapendo, ni cheche zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu. Haya ni mambo ambayo yamefichika katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu anaongoza historia ya ulimwengu kwa njia ya ujasiri wenye unyenyekevu wa watu wanaosali, wanaopenda na kusamahe. Hawa ndio watakatifu ambao ni majirani wa kila siku, wanaoshuhudia wema na huruma ya Mungu kwa njia ya matendo yao yanayogeuza historia ya ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko anasema hata baada ya kuyoyoma takribani miaka elfu mbili, bado kuna watu wanateseka na hata kuuwawa kutokana na ushuhuda wao kwa Kristo Yesu. Hawa ni watu wanaojitahidi kumwilisha ndani mwao tunu msingi za kiinjili, huku wakiendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wakati walimwengu wakienda kinyume chake. Hata waamini hawa katika ushuhuda wao, wanaweza kuhisi kwamba, pengine wameshindwa katika maisha, lakini ukweli wa mambo si hivyo wanavyofikiri. Kama ilivyokuwa wakati ule, hata leo hii, mbegu ya sala, maisha na ushuhuda wao iliyodhaniwa kwamba, imekufa, bali imeota na kuzaa matunda yanayosaidia watu kutubu na kumwongokea Mungu ambaye anaendelea kutenda kazi ya kuwaongoa na kuwaokoa watu: “Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.” Mdo 18:9-10.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea watu wote wanaodhulumiwa, kunyanyaswa na hata kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Anawataka wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili, huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa kizazi hiki. Ushuhuda wao, umwilishwe katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Wajitahidi kuwa ni mwanga angavu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wawe na ujasiri wa kuwakumbuka na kuwaombea wakosefu na wadhambi; watu “wanao ogelea katika shida na magumu ya maisha.” Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini waendelee kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao, kwa unyenyekevu na imani thabiti. Bikira Maria, Malkia wa mashuhuda wa imani, awasaidie waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake.