Vita Imesababisha Maafa Makubwa Kwa Watoto Sehemu Mbalimbali za Dunia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia, “L’Azione Cattolica Italiana, ACR”, Ijumaa tarehe 15 Desemba 2023 kimekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana heri, baraka na matashi mema katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2023. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru na kuwapongeza walimu na walezi wa vijana; amewakumbusha kwamba, kuna watoto elfu tatu wameuwawa katika vita Ukanda wa Gaza na kwamba, wanahimizwa kumpenda Mungu, Jirani pamoja na Kazi ya Uumbaji, kwani katika Sherehe ya Noeli, Mwenyezi Mungu anawaonesha upendo na kutoa mwaliko wa kumpenda Yeye, Jirani na Kazi ya Uumbaji, sanjari na kuendeleza mafungamano, urafiki na upendo ili kuweza kuukumbatia ulimwengu wote!
Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waalimu na walezi wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia kwa kufuatilia kwa makini malezi na makuzi ya vijana hawa katika safari yao ya imani. Sherehe ya Noeli ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda sana waja wake na anataka kukaa pamoja nao! Hiki ndicho kiini cha Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu akafanyika mwili na kukaa kati yao watu wake katika Familia Takatifu ya Nazareti, hii ni zawadi kubwa sana na ya kushangaza, changamoto na mwaliko ni wanadamu kupendana na kuheshimiana, lakini leo hii kuna watu wengi wanaoteseka kutokana na vita!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, vita Ukanda wa Gaza imepelekea watoto elfu tatu kupoteza maisha yao. Nchini Ukraine kuna watoto zaidi ya mia tano na huko nchini Yemen, kuna maelfu ya watoto waliouwawa kutokana na vita. Huu ni mwaliko kwa watoto kuwa ni mwanga wa Mataifa, ili uweze kuwaangaza na hatimaye, kugusa akili na nyoyo za wadau wakuu wanaoweza kusitisha vita sehemu mbalimbali za dunia. Haki na amani vinaweza kutawala ulimwenguni ikiwa kama binadamu watapendana na kuheshimiana kama ndugu wamoja na kwa njia hii walimwengu wataweza kuona mwanga na hatimaye kujipatia amani ya kweli kama walivyokuwa wanaimba Malaika “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Lk 2:14.
Kumpenda Mungu na jirani ni chachu ya kubadili mwelekeo kwa kuchagua Injili ya uhai na hivyo kurejea tena katika matumaini. Baba Mtakatifu amewataka Vijana Wakatoliki nchini Italia kujikita katika upendo kwa Mungu, upendo kwa jirani na kwa kazi ya uumbaji. Kaulimbiu ya malezi na majiundo yao kwa Mwaka 2023 imekuwa “Hii ni nyumba yako.” Hapa Mwenyezi Mungu anawaita watoto wake kutambua na hatimaye, kuheshimu uzuri wa kazi ya uumbaji inayowazunguka; kazi inayoonekana katika watu na mazingira yao ili kuweza kukomaa katika kushirikishana amana na utajiri wa ulimwengu huu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana hawa kuhakikisha kwamba, wanaumwilisha ujumbe huu, kama chemchemi ya matumaini katika maisha. Sherehe ya Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupendana wao kwa wao pamoja na kupenda na kuheshimu kazi ya uumbaji, kwa kujibu wito wake wa upendo unaounganishwa na urafiki na upendo, waweze kuikumbatia dunia kwa pamoja. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za kitume.