Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anafanya kumbukizi ya Miaka 54 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969. Baba Mtakatifu Francisko anafanya kumbukizi ya Miaka 54 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969.  (Vatican Media)

Papa Francisko Atimiza Miaka 54 ya Daraja Takatifu ya Upadre

Baba Mtakatifu Francisko anafanya kumbukizi ya Miaka 54 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969, Siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake ametoa kipaumbele cha pekee kuhusu: Haki na Amani; Maskini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anafanya kumbukizi ya Miaka 54 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969, Siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi, Mlinzi na Mwombezi wa Vipofu na Watu wenye Ulemavu wa kuona. Inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Lucia aliuwawa wakati wa madhulumu ya Diocleziano kati ya Mwaka 303-305 na kuzikwa huko Siracusa. Ibada yake ilianza kuenea kuanzia kwenye karne V toka Siracusa hadi Roma na hatimaye, kuenea sehemu mbalimbali za dunia. Jina lake limeandikwa katika orodha ya mashuhuda wa imani “Hieronymian Martyrology” na kwenye Kanuni ya Misa ya Kiroma. Kwa hakika alikuwa ni mkarimu kwa maskini. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 13 Desemba 2023 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Mtakatifu Lucia ili aweze kuwasaidia kung’ara kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji kwa Kristo Yesu, ili kweli Kristo Yesu aendelee kuwa ni mwanga angavu kwa Mataifa.

Kumbukizi ya Miaka 54 ya Daraja Takatifu ya Upadre
Kumbukizi ya Miaka 54 ya Daraja Takatifu ya Upadre

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Mwaka 2023 anatimiza miaka 87 tangu alipozaliwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 22 Februari 1998 na hatimaye kama Kardinali tarehe 21 Februari 2001.

Papa: Maskini ni kati ya vipaumbele vyake
Papa: Maskini ni kati ya vipaumbele vyake

Tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuanza utume wake rasmi tarehe 19 Machi 2013. Hii ndiyo siri ya zawadi na fumbo la Daraja Takatifu ya Upadre linalomwezesha Baba Mtakatifu kuwa ni Kristo mwingine, “Alter Christus” kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kuwa ni mtetezi wa haki na amani; kwa kuendelea kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya: utu, heshima, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa mambo yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Papa Miaka 54 ya Daraja

 

13 December 2023, 14:28