Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu ametangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 itakuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu ametangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 itakuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma.   (Vatican Media)

Papa Francisko: Siku ya Watoto Ulimwenguni Itaadhimishwa Tarehe 25-26 Mei 2024

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia changamoto kuu tatu zinazowakabili Maafisa hawa: Ulinzi na Usalama; Athari za Mabadiliko ya Tabinchi pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wao; kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unalindwa na kuheshimiwa na wale wanaovunja sheria za nchi wanapata haki yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao! Leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbalimbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu! Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari, mwamko na moyo wa kimisionari, kwa kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu ametangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 itakuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma. Maadhimisho haya yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Ni shauku ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inakirithisha kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake kwa kutoa kipaumbele cha kwanza watoto, Mama Kanisa naye katika maisha na utume wake anataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, kwa kuwapatia malezi makini, kwa kuwalinda na kuwaendeleza.

Siku ya Watoto Ulimwenguni tarehe 25-26 Mei 2024
Siku ya Watoto Ulimwenguni tarehe 25-26 Mei 2024

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Novemba 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano huu wa kwanza na wa aina yake ulinogeshwa na kauli mbiu “Tujifunze kutoka kwa watoto wadogo.” Huu ni mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Elimu na Utamaduni, ili kuwawezesha watoto kudhihirisha ndoto yao! Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kurejea tena kuwa na mawazo pamoja na hisia safi kama watoto wadogo, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni kwa wale wote wanaojisikia kuwa kama watoto wadogo. Baba Mtakatifu anasema hii ilikuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujifunza kutoka kwa watoto wadogo. Ni katika muktadha wa watoto wadogo kutokana na nguvu zao za ajabu, Kanisa linaliweza kuwafunda walimwengu jinsi ya kujenga na kudumisha umoja, ushirika pamoja na kushirikishana. Baba Mtakatifu amesikiliza kilio na sauti ya watu wa Mungu kuhusu kuanzishwa kwa Siku ya Watoto Ulimwenguni anasema Padre Enzo Fortunato, Mwandishi wa Habari katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Hii ni siku ya sala na sikukuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maaskofu, wazazi na walezi wengi wameridhishwa na uamuzi wa Baba Mtakatifu wa kuanzishwa kwa Siku ya Watoto Ulimwenguni. Huu ni mwaliko wa Mama Kanisa kwa watu wa Mungu kusimama pamoja na watoto wanaoteseka, utu, heshima na haki msingi za watoto hawa kusiginwa kutoka na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, vita na mipasuko ya kijamii; magonjwa na ukosefu wa fursa za elimu.

Hii ni Siku ya Sala na Sherehe pamoja na Baba Mtakatifu
Hii ni Siku ya Sala na Sherehe pamoja na Baba Mtakatifu

Tunakumbushwa kwamba, familia ni tabernakulo ya uhai wa mwanadamu, ni mahali ambapo watoto wanarithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Familia ni shule ya malezi na makuzi bora; mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho wa kweli; mahali ambapo watu wanajifunza kutaabikiana na kusumbukiana kwa hali na mali. Ni mahali muafaka pa kujifunza maisha ya Kisakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na kuhakikisha kwamba, kweli imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Katika familia za Kikristo, baba na mama wanapaswa kuonesha upendo wa dhati, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata na kufumbata Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, zawadi inayokwenda sanjari na malezi pamoja na makuzi ya watoto. Ni wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawafunda watoto wao katika maisha ya sala, kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, ili waweze kuvuta neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Dhamana na utume wa familia ya Kikristo unajikita katika malezi, ambayo kimsingi ni shule ya kumfuasa Kristo Yesu. Familia ni kikolezo cha uinjilishaji wa kina kwani kwa kujiinjilisha yenyewe inashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji. Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya Kristo Yesu. Watoto wanapaswa kusaidiwa kukua na kuimarika katika fadhila mbalimbali za Kikristo kwa njia ya mshikamano wa umoja, upendo, udugu wa kibinadamu na msamaha unaojikita katika maisha ya wazazi wenyewe. Watoto wajengewe utamaduni wa kushiriki katika sala, tafakari na maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ili kuwasaidia kumwilisha imani katika matendo tangu wakiwa wadogo.

Siku ya Watoto Ulimwenguni inaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni
Siku ya Watoto Ulimwenguni inaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni

Changamoto kubwa inayowakabili wazazi na walezi katika ulimwengu mamboleo ni kutokana na pilika pilika za malimwengu kiasi kwamba, wakati mwingine wazazi hawana nafasi hata kidogo ya kukaa pamoja na watoto wao. Watoto nao kutokana na majukumu mbalimbali wanajikuta kwamba, wanapata muda kidogo sana wa kukutana na kuzungumza na wazazi wao. Kumbe, hapa kuna haja ya kuweka uhusiano mwema kati ya maisha ya kiroho na maisha ya kijamii, ili watoto waweze kuwa na malezi pamoja na makuzi bora: kiroho, kiutu, kijamii na kimataduni. Mambo yote haya ni muhimu katika ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Wataalamu wa masuala ya malezi wanabainisha kwamba, kuna aina nne za malezi na makuzi ya watoto na zote hizi zina athari zake kwa watoto. Kuna malezi ya kimabavu, hapa wazazi hutumia adhabu kali kuliko kuonya na matokeo yake ni watoto kutojiamini. Malezi ya mamlaka, au demokrasia ni malezi yanayotoa nafasi kwa watoto kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha ili kuwajenga na kuwakomaza watoto hawa katika malezi na makuzi yao. Watoto kama hawa mara nyngi hujawa na furaha na kuwa na mafanikio katika maisha.

Watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakutana na Papa.
Watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakutana na Papa.

Malezi Huru: Wazazi wenye malezi huru ni wavumilivu, na hawawafuatilii watoto wao sana. Huingilia na kuonekana pale tu panapojitokeza tatizo kubwa dhidi ya watoto wao. Wazazi hawa hawawajibishi watoto wao kwa wakati na ikitokea kuwawajibisha hufanya hivyo mara chache sana. Hutoa msamaha zaidi na huamini “mtoto ni mtoto tu” wanapowawajibisha watoto mara nyingi hutoa msamaha pale mtoto anapoomba msamaha na kuahidi kubadili tabia. Wazazi hawa huchukua nafasi na jukumu la rafiki zaidi kuliko nafasi na jukumu la mzazi. Huwashawishi watoto wazungumze matatizo yao, lakini hawafanyi juhudi kubwa kukemea tabia na maamzi yasiyo sahihi ya watoto wao. Hawakemei tabia nyingi mbovu za watoto wao. Malezi huria: Wazazi hawatumii nguvu nyingi kutafuta mahitaji ya watoto wao. Wakati mwingine wazazi hawa, hawafahamu juu ya maendeleo ya watoto wao. Mara nyingi wazazi hujikita kutatua shida nyingine tu na mahitaji ya nyumbani. Wazazi hawana ufahamu wa kutosha juu ya wanachofanya watoto wao. Wazazi huweka sheria na miongozo michache tu. Hakuna msisitizo wa kutosha katika kuwaelekeza watoto wao, kuwaongoza na kuwajali. Watoto waliokulia katika malezi huria, huwa hawana ufaulu mzuri darasani, wala hawajiamini. Watoto hawa hukumbwa na matatizo mengi ya kinidhamu na huwa hawana furaha.

Siku ya Watoto 2024
11 December 2023, 15:52