COP28:Viongozi wa kidini waomba hatua za pamoja za kuponya sayari
Na Angela Rwezaula, - Vatican.
Katika tamko lililo tiwa saini na Baba Mtakatifu Francisko na viongozi mbalimbali wa kidini wakati huu wa Mkutano wa COP28 lina ahadi na matumaini kama msingi wake. Baada ya kutiwa saini katika Waraka huo uaanakisi umoja, uwajibikaji wa pamoja na udugu kama baadhi ya vipengele muhimu vya kufikia lengo la kupunguza joto la dunia nyuzi joto 1.5 ifikapo mwaka 2030. Viongozi hao wa kidini pia wamesisitiza kuunga mkono jumuiya zilizoathirikana mabadiliko ya tabianchi. Katika COP28, wawakilishi wa imani na tamaduni tofauti za kiasilia, wasomi wa kidini, mashirika ya wanawake, vijana, mashirika ya kiraia, viongozi wa biashara na watunga sera wa mazingira walikusanyika huko Abu Dhabi kuelezea masikitiko yao kwa kile kinachotokea katika ulimwengu wetu. Hapo pia, walitambua na kukiri "uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji, na migogoro na nafasi inayowezekana kwa watu wa imani kuwa kama wajenzi wa amani wa mazingira, wakijitahidi kutengeneza njia za huruma na upatanisho katikati ya migogoro.
Hati hiyo vile vile inataka majibu ya haraka ili kuharakisha mpito wa nishati inayohakikisha usawa na haki, na kuwaalika watu kukumbatia mfano wa mzunguko ili kuishi maisha yenye usawa na yenye heshima kulingana na asili. Pia waraka huo unawahimiza wafanyabiashara kubadili kutoka katika mafuta kwenda kwenye vyanzo vya nishati safi; na kwa serikali kukuza kilimo endelevu katika uhakikisho kamili wa usalama wa chakula na ulinzi wa mifumo wa ikolojia. "Hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma," inasomeka andiko hilo, likisisitiza "mahitaji ya watu wote, hasa watoto, jamii zilizo hatarini zinazokabiliwa na maafa na migogoro, vijana, wanawake na watu wa asili, pamoja na wanyama na asili, lazima kuwa katikati ya juhudi zetu."
Viongozi wa kidini aidha wanaahidi kubadilisha mifumo yao ya matumizi na kukuza ile endelevu. Pia wanaahidi kupaza sauti zao kwa ajili ya kutetea bayoanuwai na uhifadhi wa wanyamapori, kuunga mkono usawa na haki za watu wa kiasili, kutetea hekima ya mababu ambayo inahusishwa na ustawi wa Dunia. Tunaposimama kwenye kilele cha historia, kwa kuzingatia uzito wa changamoto tunazokabiliana nazo kwa pamoja, tunabaki kukumbuka urithi ambao tutauacha kwa vizazi vijavyo, waraka huo unasomeka. Tunawasihi kwa dhati watoa maamuzi wote waliokusanyika katika COP28 kushika wakati huu wa maamuzi na kuchukua hatua kwa haraka, tukisuka mstari wa hatua za pamoja na uwajibikaji wa kina. Hatimaye, hati hiyo inataka hatua za haraka, shirikishi na dhabiti "kuponya ulimwengu wetu uliojeruhiwa na kuhifadhi fahari ya nyumba yetu ya pamoja. Katika mchakato huo, tunahitaji kurudisha matumaini kwa vizazi vijavyo. Kwa pamoja, tunanyoosha mikono yetu wazi kwa wote. watu, kuwaalika kuanza safari hii kuelekea mustakabali wa uthabiti, maelewano, na kustawi kwa maisha yote Duniani."