Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi  

Mzunguko Mpya wa Katekesi: Fadhila Na Mizizi ya Dhambi

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Katika katekesi yake amekazia kuhusu dhambi na vishawishi vya dhambi, usithubutu kamwe kufanya majadiliano na Shetani, Ibilisi na kwamba, kila mwamini anapaswa kuulinda moyo wake, lakini Waswahili wanachakarika kuumwagilia moyo! Kila mwamini anapaswa kulinda moyo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kadiri ya mafundisho ya Kristo Yesu, mzizi wa dhambi umo ndani ya moyo wa mtu, katika utashi wake huru, “moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushuhuda wa uwongo na matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.” Mt 15:19-20. Moyoni pia hukaa upendo, msingi wa kazi njema na safi, ambamo dhambi huujeruhi. Rej. KKK 1853. Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.

Papa Francisko: Katesi Mpya: Fadhila na mizizi ya dhambi
Papa Francisko: Katesi Mpya: Fadhila na mizizi ya dhambi

“Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Adanu na Hewa, walijaribiwa sana na nyoka
Adanu na Hewa, walijaribiwa sana na nyoka

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 ameanza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Katika katekesi yake amekazia kuhusu dhambi na vishawishi vya dhambi, usithubutu kamwe kufanya majadiliano na Shetani, Ibilisi na kwamba, kila mwamini anapaswa kuulinda moyo wake, lakini Waswahili wanachakarika kuumwagilia moyo! Maandiko Matakatifu na hasa Kitabu cha Mwanzo kinaonesha vishawishi na asili ya dhambi na Nyoka, Ibilisi katika Bustani ya Edeni anakuwa ndiye chanzo cha vishawishi. Nyoka ni mnyama mwerevu na hatari kabisa. Alimshawishi Hawa hadi akala tunda la mti waliokatazwa kula kwani watakuwa kama Mungu, huku wakijua mema na mabaya. Katika ukweli wake, Mwenyezi Mungu alimpatia mwanadamu uhuru wa kula matunda yote ya bustani ya Eden pamoja na busara ya kutumia uhuru huu, kwa kutambua kikomo cha uhuru wake na kwamba, kiburi na majivuno ni mizizi ya dhambi. Mwenyezi Mungu akawaweka kuwa ni walinzi wa kazi ya uumbaji na wala si wamiliki wa kufahamu mema na mabaya! Hii ni hatari kubwa, kumbe, mwamini anapaswa kuulinda moyo wake. Adamu na Hawa hawakufaulu kukishinda kishawishi kile kwa kudanganywa kwamba, kwa hakika Mungu hakuwa mwema kivile na hatimaye wakagundua kwamba, upendo unalipa na dhambi pia zina matokeo yake kama yanavyosimulia Maandiko Matakatifu. Waliamini kwamba, wangekuwa kama Mungu, lakini wakajigundua kwamba, wako uchi, kielelezo cha kiburi cha mwanadamu na matokeo yake ni dhambi.

Katekesi Mpya Fadhila na Mizizi ya Dhambi
Katekesi Mpya Fadhila na Mizizi ya Dhambi

Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, mwanadamu anaanza kutenda dhambi pale anapoanza kuvutiwa kwenye dhambi, kama ilivyokuwa kwa Kaini kwa kuwa na ghadhabu na matokeo yake ni mauaji ya Abeli. “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwa 4:7. Kaini hakuweza hata kusikiliza ushauri wa Mungu. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kamwe usithubutu kujadiliana na Shetani, Ibilisi, kwani aliwahi kumshawishi hata Kristo Yesu alipokuwa Jangwani kwa muda wa siku arobaini, kwa kutumia vifungu vya Maandiko Matakatifu. Kinapokujia kishawishi, kamwe usithubutu kujadiliana nacho, bali waamini wanapaswa kuwa makini kwa kufunga milango, madirisha na hata nyoyo zao, ili kujilinda dhidi ya Shetani. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni walinzi wa nyoyo zao dhidi ya vishawishi kutoka kwa Shetani, Ibilisi. Kumbe, waamini wawe na unyenyekevu wa kuomba neema na baraka ya kulinda nyoyo zao na kwa hakika wanapaswa kulinda na kutunza nyoyo zao.

Fadhila na Mizizi ya Dhambi
27 December 2023, 13:49