Umuhimu wa Nyimbo Katika Liturujia: Furaha, Sala na Unyenyekevu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Vijana Waimbaji Kimataifa, “Federazione Internazionale Pueri Cantores, FIPC” asili yake ni “Schola Cantorum ya “Petits Chanteurs à la Croix de Bois” iliyoanzishwa huko Paris, Ufaransa, na wanafunzi wawili wa muziki, Paul Berthier na Pierre Martin, kufuatia Barua binafsi “Motu proprio Tra le sollecitudini” iliyoachapishwa na Papa Pio X tarehe 22 Novemba 1903 kuhusu “Muziki Mtakatifu ndani ya Kanisa” kwa kuweka sheria, taratibu na kanuni za muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Mnamo mwaka 1921 “Schola” walijiunga na Kwaya ya Belleville. Mwaka 1931 ukawa ni alama ya mwanzo ya kipindi cha kusafiri kwa lengo la kueneza maadili ya “Petits chanteurs à la Croix de Bois” duniani kote. Mwaka 1944 Shirikisho la kwanza la “Pueri Cantores” lilianzishwa ambalo mwaka 1947 lilitambuliwa rasmi kuwa ni vuguvugu la Kikatoliki na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa. Mnamo 1951, baada ya Kongamano la tatu la Kimataifa lililofanyika Roma, Baraza la Kitaifa la Ufaransa liliidhinisha sheria za kwanza za Shirikisho. Tarehe 31 Januari 1996, Baraza la Kipapa la Walei lilitangaza kutambuliwa kwa “Foederatio Internationalis Pueri Cantores” kama Chama cha Kimataifa cha Waamini Waimbaji chenye haki ya Kipapa.
Wanachama wa Shirikisho la Vijana Waimbaji Kimataifa, Jumamosi tarehe 30 Desemba 2023 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika mambo makuu matatu: furaha, sala na unyenyekevu. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa utume wao unaoisaidia Jumuiya ya waamini kushiriki na hatimaye, kusali vyema, huku wakimfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Nyimbo ni chemchemi ya furaha na hasa kama nyimbo hizi zinaimbwa na wanakwaya. Hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo imeendelea kuwatumbuiza watu wa Mungu karne kwa karne. Hivi ndivyo walivyokuwa wanaimba watoto wenzao wakati Shirikisho hili lilipokuwa linazinduliwa. Hawa ni watoto waliokuwa wamesheheni maisha na ndoto, waliopenda kucheza na kuishi kwa pamoja, wakisadaka muda wao kwa ajili ya kujifunza na hatimaye kuimba. Ni zawadi na sadaka inayotolewa kwa wengine, ikiwa imesheheni furaha na kwa hakika “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” 2 Kor 9:7. Kumbe, nyimbo hizi zinapoimbwa kwa ari na moyo mkuu zinageuka na kuwa ni chemchemi ya furaha kwa wasikilizaji wake. Kuna kiu ya furaha ulimwenguni kote, kwa sababu kuna umati mkubwa wa watu ambao umekumbwa na hofu na wala hauna furaha. Kumbe muziki unaweza kuzama kiasi cha kugusa nyoyo za wasikilizaji na hivyo kuwakirimia uzuri na kuwakirimia tena ari na matumaini ya maisha na kwamba, hii ndiyo furaha.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, wao ni wasanii maalum wanaowasaidia waamini wengine kuweza kusali vyema zaidi, changamoto na mwaliko kwa wanakwaya hawa kujenga urafiki, mahusiano na mafungamano ya karibu na Kristo Yesu, ili kujichotea upendo utakaogusa nyoyo za wasikilizaji wao kwa kutambua kwamba, kuimba ni kusali mara mbili; ni tendo na upendo unaowawezesha watu wa Mungu kuonja, huruma, upendo, ukarimu na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye, kuiwezesha Jumuiya ya waamini kutembea katika mshikamano kwa njia ya sala. Nyimbo anakaza kusema Baba Mtakatifu ni shule ya unyenyekevu na huduma kwa watu wa Mungu na kwa Mungu mwenyewe. Hii ni huduma inayowawezesha waamini kukutana na Mwenyezi Mungu, katika hali ya ukimya pamoja na kusikiliza kile ambacho Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake. Baba Mtakatifu amewaangalisha wanakwaya hawa, kwamba, kamwe wasitake “kujimwambafai; kujitafuta na kutaka kujikweza” kwani kuna hatari ya kuwaharibia wengine maisha na utume wao. Katika umoja unaofumbatwa na unyenyekevu muziki unakuwa ni kielelezo cha urafiki na Mungu, jirani na kati yao wenyewe. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja, ili hatimaye, waweze kuishi vyema. Huu ni mchakato unaowatoa jasho kweli kweli na kwamba, kwa njia ya mng’ao wa nyuso zao, wanaweza kutangaza na kushuhudia uzuri. Ikumbukwe kwamba, muziki mtakatifu kiini chake ni Neno la Mungu. Kwa hakika wamebahatika kupokea zawadi hii na kwamba, wanabahatika hata wale pia wanaowasikiliza na pale wanaposhirikishana wao kwa wao. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa huduma yao makini na kuwataka waiendeleze kwa ari na moyo mkuu, chini ya viongozi wao wakuu.