Papa Francisko maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Papa Francisko maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.   (Vatican Media)

Sala ya Papa Francisko Kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kwenda kusali na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu kuweka shada la waridi ya dhahabu kwenye picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” kuonesha umuhimu wa Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa., lakini pia kutolea ushuhuda Ibada yake kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki kila tarehe 8 Desemba, wamekuwa wakienda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kati kati ya mji wa Roma. Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Baba Mtakatifu kabla ya kwenda kusali na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu kuweka shada la waridi ya dhahabu kwenye picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” kuonesha umuhimu wa Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Waridi la dhahabu kwa mara ya kwanza lilitolewa na Papa Giulio III kunako mwaka 1551 na Waridi la pili lilitolewa na Papa Paulo V kunako mwaka 1613. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema, haya mawaridi mawili hayaonekani Kanisani hapo. Kumbe, kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kutoa shada la waridi la dhahabu kwenye Picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi ni kuonesha na kushuhudia mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Bikira Maria, ili kwa maombezi yake, amani iweze kurejea tena sehemu mbalimbali za dunia.

Papa Francisko amesali kwenye picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi
Papa Francisko amesali kwenye picha ya Bikira Maria Afya ya Warumi

Kikosi cha Zima Moto asubuhi na mapema, kama ilivyotokea kunako tarehe 8 Desemba 1857 kimeweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii ni siku ambayo makundi mbalimbali ya waamini yametoa mashada ya maua kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu katika sala yake, ameukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kumshukuru kwa tunza yake ya kimama kwa mji wa Roma na ndiyo maana waamini wamemtuza kwa mashada ya maua kama kielelezo cha upendo wao. Amemwendea Bikira Maria huku moyo wake ukiwa umegawanyika kati ya matumaini na huzuni. Amemwomba Bikira Maria aendelee kuzilinda familia zinazo ogelea katika furaha na wasiwasi, alinde maeneo ya kazi, shule, ofisi, hospitali na nyumba za wagonjwa; magereza, awasaidie wale wote wanaoishi barabarani, parokia na jumuiya nzima ya waamini wa Kanisa la Roma. Baba Mtakatifu anamshukuru Bikira Maria kwa uwepo wake unaowakirimia waamini faraja na matumaini. Baba Mtakatifu amemwendea Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa kutambua kwamba, ubaya hauwezi kuwa na kauli ya mwisho, mwanadamu hakuumbwa ili afe, bali aweze kuwa na uzima wa milele na kwamba, badala ya chuki, watu wajenge udugu wa kibinadamu, badala ya vurugu watu waishi kwa amani na utulivu. Kwa kumwangalia Bikira Maria, waamini wanapata imani na matumaini kwani matukio ya ulimwengu huu yanatia hofu na wasiwasi, ndiyo maana waamini wanamwomba Bikira Maria awaangalie kwa macho yenye huruma watu wanaokandamizwa kwa ukosefu wa haki, umaskini na vita na hapa kwa namna ya pekee kabisa watu wa Mungu nchini Ukraine, Wapalestina na Waisraeli wanaoteseka kwa vita.

Papa Francisko amesali na kuombea amani duniani
Papa Francisko amesali na kuombea amani duniani

Baba Mtakatifu katika sala yake amemweleza Bikira Maria kwamba, anawaleta mbele yake akina mama wenye majonzi na huzuni nyingi kama ilivyokuwa kwake. Ni akina mama wanaolia na kuwaombolezea watoto wao waliouwawa kikatili kutokana na vita pamoja na vitendo vya kigaidi. Watoto wanaosafiri bila ya matumaini kutafuta maisha bora zaidi. Ni akina Mama ambao wanateseka kuwafungua watoto wao kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, watoto wanaoteseka kutokana na magonjwa ya muda mrefu. Baba Mtakatifu amemwambia Bikira Maria kwamba, ulimwengu mambo leo unamhitaji mwanamke kama yeye, ili aweze kukabidhiwa wanawake wote wanaoteseka kutokana na ukatili wa kutupwa, mjini Roma, Italia na Ulimwengu katika ujumla wake. Bikira Maria anawafahamu wote hawa kwa sura na majina. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria apanguse machozi ya wanawake hawa pamoja na yale ya wapendwa wao. Awasaidie waamini kufanya hija ya elimu na utakasaji, kwakutambua vita bado imenata katika nyoyo na akili za watu, awaombee kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaweka huru. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria awaoneshe waamini njia ya toba na wongofu wa ndani, kwani hakuna msamaha bila toba ya kweli. Ulimwengu unaweza kubadilika ikiwa kama nyoyo za watu zimeongoka na hili zoezi linapaswa kuanza kwa mtu mmoja mmoja. Lakini moyo wa binadamu unaweza tu kuongoka kwa neema ya Mwenyezi Mungu; hii ni neema ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia Bikira Maria tangu kutungwa kwake mimba. Neema ya Bwana wetu Kristo Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu awaoneshe Kristo Yesu, Mkombozi wa watu wote na Ulimwengu katika ujumla wake. Njoo Bwana Yesu Kristo, Leta ufalme wako wa upendo, haki na amani. Amina.

Sala Bikira Maria
08 December 2023, 16:21