Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji kwa Mwaka 2023 inanogeshwa na kauli mbiu: "kila hatua ni muhimu." Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji kwa Mwaka 2023 inanogeshwa na kauli mbiu: "kila hatua ni muhimu."   (AFP or licensors)

Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji Kwa Mwaka 2023: Kila Hatua Ni Muhimu

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu: "kila hatua ni muhimu." Bado madhara makubwa yaliyosabishwa na Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yanaendelea kuwasigana watu sehemu mbalimbali za dunia. Vita, migogoro na mipasuko ya kijamii, kidini na kisiasa inachangia watu kuyakimbia makazi na nchi zao. Papa anasema uhamiaji ni ishara ya nyakati, dumisheni uaminifu kwa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 18 Desemba inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji. Nalo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, (IOM) hutumia siku hii kubainisha mchango unaotolewa na takribani wahamiaji milioni 272, wakiwemo watu wasiokuwa na makazi maalum zaidi ya milioni 41 sanjari na changamoto wanazokabiliana nazo wahamiaji. Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu: "kila hatua ni muhimu." Bado madhara makubwa yaliyosabishwa na Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yanaendelea kuwasigana watu sehemu mbalimbali za dunia. Vita, migogoro na mipasuko ya kijamii, kidini na kisiasa inachangia watu kuyakimbia makazi na nchi zao. Athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa ni chanzo kikuu cha umaskini na magonjwa ya milipuko, kiasi kwamba, kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: Hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Bado kuna athari kubwa za myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa inayopelekea makundi makubwa ya watu kuzihama nchi zao, ili kutafuta maisha bora zaidi ughaibuni. Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Ulinzi na Haki za Wafanyakazi Wahamiaji na Familia zao ulipitishwa kunako tarehe 18 Desemba 1990 na ukaanza kutumika kunako mwaka 2003 baada ya Mkataba wa Guatamela kuridhia kwamba, idadi ya chini kabisa inayokubalika ni jumla ya nchi ishirini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasema katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji, anaangalia hitaji la dharura la utawala salama wa uhamiaji unaojikita katika mshikamano, ushirikiano, na kuheshimu haki msingi za binadamu.

Huduma kwa Wakimbizi na Wahamiaji: Injili ya Msamaria mwema
Huduma kwa Wakimbizi na Wahamiaji: Injili ya Msamaria mwema

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu tarehe 18 Desemba 2023 anasema, uhamiaji ni ishara ya nyakati ambapo ustaarabu uko hatarini. Kwa Wakristo, uaminifu wao kwa Kristo Yesu uko hatarini kwani alisema: “Nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha.” Mt 25:35. Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka 2023 kwa upande wa Kanisa Katoliki yamenogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine: kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea watu kulazimika kuyahama makazi na nchi zao, ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Haki ya kubaki nchini mwako ina mizizi yake katika maisha ya mwanadamu, kwani hii ni haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni haki inayomwezesha mtu kuishi kwa kuzingatia utu, heshima na haki zake msingi na hivyo kujipatia pia maendeleo fungamani. Haki inapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Siku ya Wahamiajia Duniani 2023: Haki Msingi za Wafanyakazi
Siku ya Wahamiajia Duniani 2023: Haki Msingi za Wafanyakazi

Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia nk. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 19 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliongoza tafakari mintarafu wakimbizi na wahamiaji katika mwelekeo wa Injili ya Msamaria Mwema. Mwinjili Luka anakazia kuhusu Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alimwona, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai. Huu ndio wito na mwaliko anaoutoa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya Msamaria Mwema
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya Msamaria Mwema

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufungua malango yake kwa wakimbizi na wahamiaji, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema aliyethubutu kuokoa maisha ya mtu yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Hata leo hii kuna watu wanaohatarisha maisha yao huko jangwani, misituni na kwenye mito, maziwa na bahari. Ni watu wanaoteswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi, kiasi hata cha kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Mara nyingi hawa ni watu wanaokimbia: majanga asilia, vita pamoja na vitendo vya kigaidi kama inavyojitokeza kwa sasa. Kuna watu ambao hawawajali hata kidogo, kielelezo cha ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa huruma na mapendo kwa sababu huu ndio utambulisho wa Mwenyezi Mungu katika mioyo ya wanadamu. Itakumbukwa kwamba, mtindo wa Mungu unasimikwa katika maneno makuu matatu: Ukaribu, Huruma na Upole na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Ukristo uliopelekea yule Msamaria mwema kutangaza na kushuhudia wema wa Mungu na udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kama Msamaria Mwema kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji katika mateso yao.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani
Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani

Ni vyema jamii ikajenga utamaduni wa kudumisha usalama barabarani, ili kusitokee watu wakaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Hii ni changamoto ya kujizatiti kikamilifu katika mapambano ya mitandao ya biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanatumia njia halali katika kupata hifadhi. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na majadiliano ya sera za kisiasa mintarafu idadi ya watu duniani, pamoja na ukuaji wa uchumi, ili wakimbizi na wahamiaji waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini zinazowajibisha ili kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji linalotarajia kuongezeka maradufu kwa siku za usoni.

UN Siku Wahamiaji 2023
18 December 2023, 14:31