Tafuta

Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. 

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Utakatifu

Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inaonesha: Mfano bora wa wema na fadhila, sanjari na vifungo vya upendo. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wanasema, Mama Kanisa tangu mwanzo wa maisha na utume wake amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba: Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” na kama zinavyojitokeza kwa sasa katika Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023.

familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo
familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo

Baba Mtakatifu anasema, Ndoa ya Kikristo kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, inatekelezwa kwa utimilifu katika muungano kati ya mwanaume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenziye kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na wa kipekee, ambamo kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzake hadi kufa, na wanakuwa radhi kuendeleza uzao, tena wamewekwa wakfu kwa Sakramenti inayowaletea neema ya kuwa Kanisa la nyumbani na kuwa chachu ya maisha mapya kwa jamii. Hii ndio maana ya Ndoa ya Kikristo na wala si vinginevyo! Rej. Amoris laetitia 292. Pamoja na msimamo huu wa Kanisa, lakini pia upendo wa kichungaji unapaswa kuoneshwa kwa kujikita katika: uelewa, uvumilivu, huruma na ujasiri bila kuwahukumu waamini wengine kuwa ni wadhambi! Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, huu ni wakati wa kugundua tena: Ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungano, ili kweli mahusiano ya wanandoa yageuke na kuendelea kujenga na kuziimarisha familia, Kanisa dogo la nyumbani.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Bwana, huwajia wanandoa Wakristo katika Sakramenti ya Ndoa na kubaki nao, katika tafakari ya Neno la Mungu, Sala na katika hali zote za maisha. Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Liturujia ya Familia iwe ni shirikishi.
Liturujia ya Familia iwe ni shirikishi.

Liturujia ya Kanisa la nyumbani ipewe uzito na msukumo wa pekee, ili kuachana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea. Maisha ya familia yageuzwe kuwa ni Liturujia ya Ndoa kwa njia ya Sala zinazowashirikisha wanafamilia wote, kwa kugawana majukumu; kwa kusoma na kushirikishana tafakari ya Neno la Mungu; kwa kusali kwa ajili ya mahitaji msingi ya familia pamoja na Kanisa katika ujumla wake, bila kusahau kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Njia za mawasiliano namitandao ya jamii, ziwezeshe familia nyingi kuweza kuunganika kwa njia ya sala pamoja na kuwashirikisha watoto katika Liturujia hii ambayo inapaswa kuwa ni Liturujia shirikishi. Wanandoa wanakumbushwa kwamba Sakramenti hii ni kwa ajili ya kuwatakatifuza na kuwakomboa wanandoa. Kwa sababu hiyo, wanandoa ni ukumbusho wa daima kwa Kanisa juu ya kile kilichotokea Msalabani; nao ni mashuhuda wa wokovu wanaoushiriki kwa njia ya Sakramenti kila mmoja mbele ya mwenzake na watoto wao. Wanandoa ni mashuhuda wa: unabii na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo makini cha zawadi kama alivyofanya Kristo Yesu. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anawahimiza wanandoa na familia kutumia fursa hii ya neema katika mchakato wa ujenzi wa familia, kama Kanisa dogo la nyumbani.

Sikukuu ya Familia Takatifu
29 December 2023, 15:15