Tafuta

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Desemba anaadhimisha Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Desemba anaadhimisha Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani. 

Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa Imani: Injili ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo!

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii tarehe 28 Desemba 2023 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kusali kwa ajili ya kuwaombea watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia: Kwa kutolewa mimba, watoto wanaoteseka kutokana na: Umaskini, baa la njaa na magonjwa na wale ambao wanabebeshwa silaha na kutumwa mstari wa mbele kama chambo kwenye mapigano bila ya kuwasahau wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto ambao wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao! Leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbalimbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu! Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari, mwamko na moyo wa kimisionari, kwa kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Desemba anaadhimisha Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani, waliomuungama Mtoto Yesu hata bila ya kumtambua, kiasi cha kuyamimina maisha yao. Hii ni Sikukuu inayofungamanishwa na Sherehe ya Noeli na kwamba, ni tarehe ambayo imeandikwa pia kwenye orodha ya majina ya wafiadini ya Mtakatifu Jerome kati ya Karne V-VI, “Martyrologium Hieronymianum.”

Watoto wajengewe mazingira mazuri ya ukuaji kiroho na kimwili
Watoto wajengewe mazingira mazuri ya ukuaji kiroho na kimwili

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii tarehe 28 Desemba 2023 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kusali kwa ajili ya kuwaombea watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia: Kwa kutolewa mimba kabla hata hawajazaliwa kutokana na watu kumezwa na utamaduni wa kifo; watoto wanaoteseka kutokana na: Umaskini, baa la njaa na magonjwa na wale ambao wanabebeshwa silaha na kutumwa mstari wa mbele kama chambo kwenye mapigano bila ya kuwasahau watoto wanaotumbukizwa katika uhamiaji wa shuruti ili mradi tu wapate tumaini. Hawa kwa hakika ni Yesu wa wadogo katika ulimwengu mamboleo. Watoto Mashahidi waliuwawa na Mfalme Herode kwa hofu ya kupoteza kiti chake za kifalme, baada ya kuambiwa kwamba, Kristo Yesu, Mfalme wa Mataifa amezaliwa mjini Bethlehemu. “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.” Huu ulikuwa ni utimilifu wa Unabii uliokuwa umetolewa na Nabii Yeremia akisema: “BWANA asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako.” Yer 31:15.

Watoto wanahitaji amani na utulivu
Watoto wanahitaji amani na utulivu

Tangu mwanzo, Mama Kanisa amewaangalia watoto hawa kama mashuhuda wa Fumbo la Umwilisho, watoto ambao hata kama hawakubahatika kumwona Kristo Yesu, lakini walikirimiwa Ubatizo wa Damu. Kumbe, wao ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya sadaka ya maisha yao. Mama Kanisa daima anafundisha kwamba, kifodini ni sadaka kubwa ambayo Mwenyezi Mungu hupenda kuwakirimia waja wake. Sikukuu ya Watoto mashuhuda wa imani inafuatana na mashuhuda wa imani kama vile: Mtakatifu Stefano Shemasi na shahidi wa kwanza wa Kristo Yesu na Mwinjili Yohane ambao daima wamesimama kidete kutangaza na kushuhudia: Imani, Matumaini na Mapendo; daima wakitetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. “Mungu Baba Mwenyezi, ambaye kwa mahubiri ya Watoto Mashuhuda wa imani wasio na hatia, leo wamekiri si kwa maneno, bali kwa kifodini; ili imani yetu tunayoitangaza kwa ndimi zetu, ishuhudiwe kwa maadili na utu wema.” “Deus, cuius hodierna die præcónium Innocéntes Mártyres non loquéndo, sed moriéndo conféssi sunt: ómnia in nobis vitiórum mala mortífica; ut fidem tuam, quam lingua nostra lóquitur, étiam móribus vita fateátur.”

Watoto wana haki ya kupata ulinzi na usalama wa maisha yao
Watoto wana haki ya kupata ulinzi na usalama wa maisha yao

Wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu ametangaza kwamba, tarehe 25 na 26 Mei 2024 itakuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, itakayoadhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma. Maadhimisho haya yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Ni shauku ya Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inakirithisha kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake kwa kutoa kipaumbele cha kwanza watoto, Mama Kanisa naye katika maisha na utume wake anataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa watoto, kwa kuwapatia malezi makini, kwa kuwalinda na kuwaendeleza. Ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za mtoto ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake; kama ilivyo kwa “Tamko la Haki za Mtoto la Mwaka 1959” na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Mtoto wa Mwaka 1989 na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwa kina katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira bora, rafiki na salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Kristo Yesu anaonya kwamba, ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini!

Watoto waonjeshwe huruma, upendo na mshikamano ndani ya familia zao
Watoto waonjeshwe huruma, upendo na mshikamano ndani ya familia zao

Changamoto pevu kwa wakati huu ni ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za watoto na vijana; ukuaji wao makini na salama; furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda na kudumisha haki msingi za watoto, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata elimu bora na huduma msingi ya afya hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Watoto hawa wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika wimbi la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Matokeo yake ni kwamba, baadhi yao wana nyanyaswa, wanadhulumiwa na kutumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo! Kuna watoto wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibika pamoja na ujinga! Watoto hawa ni mboni ya jicho la Kristo Yesu! Kanisa litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa na kwamba, watoto wanapewa haki ya kufurahia utoto wao katika mazingira: salama, ya amani na utulivu na kwamba, watoto hawa wasipokwe furaha na matumaini yao kwa sasa na kwa siku za usoni!  Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Novemba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoteseka kwa sababu mbalimbali; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wahanga wa vita na wale wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo; wote hawa wapewe fursa ya kupata elimu na kuonja upendo kutoka katika familia zao.

Watoto mashuhuda wa imani
Watoto mashuhuda wa imani

 

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika ulimwengu mamboleo kuna watoto wanaoteseka na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi mithili ya watumwa. Hawa ni watoto wenye majina, sura na utambulisho ambao wamepewa na Mwenyezi Mungu na wala si namba au idadi yao inayowafanya watu kuwavutia hisia. Watu wanasahau dhamana na wajibu wao kwa watoto hawa na matokeo yake, wanawanyanyasa, wanawanyonya na kuwadhulumu, kiasi cha kupokwa haki yao ya kucheza, kusoma na kuwa na ndoto ya maisha bora zaidi. Hawa ni watoto ambao kamwe hawafurahii hata kidogo fukuto na maisha na upendo wa kifamilia. Kwa mtoto yoyote anayedhulumiwa, anayetelekezwa, bila kupelekwa shule au kupatiwa matibabu muafaka ni kilio kinachopaa mbinguni kwa Baba wa milele na hii ni aibu kwa miundo mbinu ambayo imejengwa na watu wazima na kwamba, kutelekezwa kwa watoto katika mazingira magumu na hatarishi ni makosa ya familia na jamii katika ujumla wake. Kimsingi watoto wanayo haki ya kupata elimu, kupendwa na watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu kamwe hajawasahau. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, yatima na wahanga wa vita. Wawe na uhakika wa kupata elimu na fursa ya kufurahia maisha na upendo wa kifamilia.

Watoto mashuhuda
28 December 2023, 15:37