Tamasha la Nyimbo za Noeli Kwa Mwaka 2023: Injili ya Noeli ni Moja!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu “Fondazione Pontificia Gravissimum Educationis – Cultura per l’Educazione”, Jumamosi tarehe 16 Desemba 2023 umeandaa Tamasha la Noeli kwa mwaka 2023 linalohusisha nyimbo za zamani ambazo zimegeuzwa kuwa ni sehemu ya sala za waamini na ziliimbwa kwa kichwa! Hata katika ulimwengu mamboleo, zile nyimbo zinazopendwa sana na vijana wa kizazi kipya wanaziimba kwa kichwa; maneno yanayowekwa kwenye muziki yanaamsha hisia kali ya mambo msingi katika maisha. Inasadikiwa kwamba, Italia ni kati ya nchi ambazo zina utajiri na amana kubwa ya nyimbo za zamani za Noeli, zinazofahamika na kuimbwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu.
Hizi ni nyimbo zenye utajiri na amana kubwa ya kitaalimungu na kwamba, Mtakatifu Alfonsi Maria de Liguori, ni kati ya watunzi mahiri sana wa nyimbo za Noeli. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wasanii wa Tamasha la Nyimbo za Noeli kwa Mwaka 2023 mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewakumbusha wasanii hawa kwamba, hata wao wanaingia katika Mapokeo ya nyimbo za Noeli, zenye ujumbe wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Nyimbo za Noeli zimeenea sehemu mbalimbali za dunia na zinapania kuwasilisha ujumbe wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Huu ni ujumbe unaomwilishwa katika lugha na tamaduni mbalimbali, kwa sababu Injili ya Noeli ni moja, lakini inamwilishwa katika lugha na tamaduni mbalimbali.
Lakini kwa bahati mbaya mwelekeo wa sasa wa “kiteknokratiko” unakwenda kinyume chake kwa kutaka kufanya mambo yote kuwa sawa. Sanaa ya nyimbo za Noeli ni tofauti na nyimbo hizi ambazo zinapaswa kuimbwa kama zinazovububujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za waamini na wasanii katika ujumla wao. Kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu Francisko Sherehe ya Noeli imetekwa na wafanyabiashara na hivyo kugeuzwa kuwa ni kipindi cha ulaji wa kupindukia. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya wasanii, kulinda na kudumisha maana ya Sherehe ya Noeli kwa nyimbo zao. Baba Mtakatifu amewataka wasanii hawa kuwakumbuka na kuwaombea watu wanaoishi katika vita hata na mahali alipozaliwa Mtoto Yesu yaani Bethlehemu kuna vita. Baba Mtakatifu amewashukuru na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!