Tafuta

Salam na Baraka za Baba Mtakatifu Francisko kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Noeli ya Mwaka 2023 Salam na Baraka za Baba Mtakatifu Francisko kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Noeli ya Mwaka 2023  (ANSA)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Urbi et Orbi: Noeli 2023

Papa: “Urbi et Orbi” Noeli tarehe 25 Desemba 2023 amekazia kuhusu: Habari Njema ya furaha ya kuzaliwa kwa Yesu Mfalme wa Amani, mwaliko kwa waamini kukataa: mawazo na vita, safari isiyo na lengo, ushindi bila mshindi, huu ni mwaliko wa kukataa matumizi ya silaha sehemu mbalimbali za dunia na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, majadiliano na upatanisho na hivyo kuwa ni sauti kwa watu wasiokuwa na sauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” zilianza kutolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya satellite saba. Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2023 amekazia kuhusu: Habari Njema ya furaha ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mfalme wa Amani, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukataa: mawazo na vita, safari isiyo na lengo, ushindi bila mshindi, huu ni mwaliko wa kukataa matumizi ya silaha sehemu mbalimbali za dunia na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, majadiliano na upatanisho na hivyo kuwa ni sauti kwa watu wasiokuwa na sauti. Baba Mtakatifu katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” anasema, macho na nyoyo za Wakristo zimeelekezwa mjini Bethlehemu, mahali ambako kwa sasa kunatawaliwa na mateso na kimya kikuu, lakini bado kunaendelea kusikika ujumbe wa Habari Njema ya furaha kwani katika Mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Rej. Lk 2:11. Huu ni ujumbe wa furaha na matumaini kusikia kwamba, Neno wa Baba wa milele amefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Hii ni habari inayotoa mwelekeo mpya wa historia ya maisha ya mwanadamu. Hii ni furaha kuu inayompandisha hadhi mwanadamu, chemchemi ya matumai kwa kutambua kwamba, wamezaliwa kutoka juu.

Papa Francisko akitoa ujumbe na baraka za Urbi et Orbi, Noeli 2023
Papa Francisko akitoa ujumbe na baraka za Urbi et Orbi, Noeli 2023

Kristo Yesu ni Mwana pekee wa Mungu anayewakirimia waja wake uwezo wa kuwa “Watoto wa Mungu.” Kumbe hii ni furaha inayofariji nyoyo za watu na kupyaisha matumaini na hatimaye, kuwakirimia watu amani. Hii ndiyo furaha ya Roho Mtakatifu, furaha inayowafanya wanadamu kujisikia kwamba wao ni watoto wa pendwa wa Mungu. Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa anayefukuzia mbali giza la dunia hii na hivyo kutoa nuru halisi ya Mungu imtiaye nuru kila mtu, changamoto na mwaliko wa kufurahi wale wote ambao wamepoteza matumaini na uhakika wa maisha kwani Kristo Yesu amezaliwa kwa ajili ya watu hawa; na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwashika mkono, ili aweze kuwaokoa kwa hofu na hatimaye, kuwaonesha macho yake angavu. Leo utabiri wa Nabii Isaya unapata utimilifu wake, kwa sababu binadamu amepewa Mtoto mwanaume na jina lake litakuwa ni Mfalme wa amani na amani yake haitakuwa na mwisho. Katika Maandiko Matakatifu Mfalme wa amani ni wazo linalokinzana na utamaduni wa kifo. Baada tu ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu mjini Bethlehemu kukatokea mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia. Hata leo hii mauaji haya yanaendelea kutokana na sera za utoaji mimba; wakimbizi na wahamiaji wa shuruti wanaotafuta matumaini na kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto wadogo ambao utoto wao umeathirika kutokana na vita, hawa ndio watoto wadogo wanaomwakilisha Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, kusema ndiyo kwa Mfalme wa Amani ni kukataa mawazo pamoja na vita kwa kutambua kwamba vita ni safari isiyo na leo; huu ni ushindi bila ya kuwa na mshindi; huu ni upumbavu usiokuwa na sababu, kukataa vita kuna maanisha ni kukataa kwa biashara haramu ya silaha inayokoleza utamaduni wa kifo.

Madhara na athari za vita kati ya Israeli na Palestina
Madhara na athari za vita kati ya Israeli na Palestina

Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna ongezeko kubwa la utengenezaji sanjari na biashara ya silaha duniani inayoendelea kuteketeza maisha ya watu wengi. Watu wanahitaji chakula na wala si sihala, ili waweze kujikita katika mchakato wa uzalishaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni fedha ya umma inanayotumika kununulia silaha. Nabii Isaya katika utabiri wake anasema, “nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kwa msaada wa Mungu, Jumuiya ya Kimataifa ijibidiishe ili siku hii iweze kuwadia kwani vita kati ya Israeli na Palestina imesababisha madhara makubwa na kwamba, bado anabeba moyoni mwake, shambulizi la kigaidi lililofanywa tarehe 7 Oktoba 2023. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wahusika ili kuhakikisha kwamba, wanawaachilia wafungwa na mateka wa vita pamoja na kusitisha operesheni ya kijeshi, ili kuruhusu misaada ya kiutu iweze kupelekwa kwa waathirika. Ni mwaliko kwa Israeli na Palestina kujikita katika upatikanaji wa suluhu ya kudumu kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; utashi wa kisiasa pamoja na msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu nchini Siria, Yemen na Lebanon ili wapate utulivu wa kisiasa na kijamii. Mtoto Yesu aiombee Ukraine ili iweze kupata amani na kwamba, bado anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu, kiroho kwa watu wa Mungu nchini Ukraine, ili kwa njia ya jitihada za kila mmoja, waweze kuhisi upendo wa Mungu katika maisha yao.

Papa Francisko Ujumbe wa Urbi et Orbi 2023
Papa Francisko Ujumbe wa Urbi et Orbi 2023

Baba Mtakatifu amezikumbuka na kuziombea nchi za Armenia na Azerbaijan ili ziweze kupata amani ya kudumu, msaada kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum, kwa kuzingatia sheria wapate uhakika wa usalama pamoja na kuheshimu mapokeo ya dini mbalimbali, hii ikiwa ni pamoja na kuheshimu maeneo ya ibada. Baba Mtakatifu amelikumbuka Bara la Afrika linalokabiliwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kisiasa hasa maeneo yaliyoko Kusini mwa Jangwa na Sahara, Pembe ya Afrika, Sudan, Cameroon, DRC pamoja na Sudan ya Kusini. Huu ni mwaliko kwa Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, kuimarisha vifungo vya umoja na mshikamano wa kidugu, kwa kujikita katika majadiliano na upatanisho wa Kitaifa, ili kujenga mazingira yatakayosaidia kujenga amani ya kudumu. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu asaidie juhudi za Amerika ya Kusini pamoja na zile za watu wema, ili hatimaye, kuvuka kinzani na mipasuko ya kisiasa na kijamii; waunganishe nguvu zao ili kupambana na umaskini unaosigina utu, heshima, na haki msingi za binadamu. Wajikite katika mchakato wa ujenzi wa usawa na hivyo kujizatiti katika kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Mtoto Yesu kutoka katika hori ya kulishia Wanyama anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti; sauti ya maskini wanaopoteza maisha kutokana na ukosefu wa maji safi na salama; uhakika wa chakula; fursa za ajira; Sauti kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaohatarisha maisha yao kutokana na kufanya maamuzi magumu ya maisha na wakati mwingine wanatumbukia katika “makucha” ya wafanya biashara ya binadamu na viungo vyake.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Utamaduni wa amani
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025: Utamaduni wa amani

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Muda wa maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo iwe ni fursa ya kukataa utamaduni wa kifo kwa kupinga vita na hivyo kujikita katika ujenzi wa amani duniani kama Nabii Isaya anavyosema: “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.” Isa 61:1. Baba Mtakatifu amehitimisha Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” kwa kusema kwamba, maneno haya yalipata ukamilifu wake katika Kristo Yesu, Rej. Lk 4:18 aliyezaliwa mjini Bethlehemu. Anawaalika kumpokea, kumkaribisha na kumfungulia nyoyo zao, Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia na Mfalme wa amani.

Urbi et Orbi 2023
25 December 2023, 14:23