Tafuta

Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inanogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace. Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inanogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace. 

Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Ulimwenguni, 2024

Tarehe Mosi Januari 2024, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Au “Akili Mnemba na Amani. Papa Francisko anasema mifumo yote ya akili mnemba itumike kupunguza mateso ya binadamu, kukuza maendeleo shirikishi na kusaidia kumaliza vita, kinzani na migogoro; na wala si kuongeza ukosefu wa haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe Mosi Januari 2024, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema mifumo yote ya akili mnemba itumike kupunguza mateso ya binadamu, kukuza maendeleo shirikishi na kusaidia kumaliza vita, kinzani na migogoro; na wala si kuongeza ukosefu wa usawa na haki za binadamu duniani. Bikira Maria Mama wa Mungu: Kwa lugha ya Kigiriki: Theotokos, Θεοτόκος; kwa Kilatini “Deipara” au “Dei genitrix.” Kiri ya imani kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, Bikira Maria Mama wa Kristo ni mfano bora wa kuigwa katika kulinda na kudumisha imani inayomwilishwa katika ushuhuda. Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba, yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa milele wa Baba, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni “Mama wa Mungu” “Theotokos, Θεοτόκος.” Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira kwa sababu mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu. Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso ili kukukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo. Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake.

Bikira Maria Mama wa Mungu
Bikira Maria Mama wa Mungu

Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa. Bikira Maria ni Mama pia wa maisha ya kiroho kama alivyofafanua Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Bikira Maria alitekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akawa ni zaidi ya mfuasi wa Kristo kwa sababu alikuwa kwanza kabisa ni Mama wa Kristo. Huu ni uhusiano wa ndani kabisa uliojengeka kati ya Bikira Maria na Kristo Yesu kutokana na imani thabiti ya Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu ni cheo kikubwa kutokana na upendeleo na neema aliyopata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hiki ni kiini cha imani ya Kanisa. Bikira Maria Mama wa Mungu kama anavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu anapaswa kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo na kamwe asiwe ni sababu ya mipasuko, kinzani, migawanyiko na utengano.

Bikira Maria awe ni mfano bora wa mafungamano ya kijamii
Bikira Maria awe ni mfano bora wa mafungamano ya kijamii

Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inanogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema akili ni kati ya zawadi ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa kumuumba kwa sura na mfano wake, akampatia akili ya kuweza kujibu upendo wa Mungu kwa uhuru zaidi na kwamba, kwa njia ya kazi na maarifa yake, binadamu daima amefanya bidii ili kuyaendeleza maisha yake. Huu ni mwaliko wa kushirikiana na mpango wa Mungu ili kujenga na kudumisha amani miongoni mwa watu wa Mataifa; kukuza uhuru, ushirika wa kidugu ili kuboresha maisha ya binadamu na hatimaye ulimwengu. Mama Kanisa anatambua maendeleo makubwa ya sayansi ambayo yameboresha maisha ya watu wengi, mwaliko ni kuwajibika barabara na matumizi haya makubwa ya sayansi na teknolojia, ili kuepuka hatari sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo haya makubwa yanajionesa katika ulimwengu wa kidigitali na wasi wasi wake kwa siku za mbeleni.

Akili Mnemba na amani duniani, 2024
Akili Mnemba na amani duniani, 2024

Teknolojia ya siku zijazo: Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafunagamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za wat una kwamba, teknolojia ya akili bandia iwe inategemewa. Kuwepo na chombo kitakachodhibiti masuala ya maadili, haki msingi za watumiaji na waathirika. Teknolojia ya akili mnemba itumie pia tafiti za kitekolojia na kisayansi, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo na kwamba, itakuwa na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, kwa kuweka msingi wa ufahamu hadi kufikia ukweli na kamwe teknolojia hii isitumike kwa ajili ya kusambaza habari za kughushi na hivyo kusababisha njia za mawasiliano ya jamii kutoaminika, kwa kujikita katika masuala ya ubaguzi; kuingilia katika michakato ya uchaguzi, kwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kukomaza ubinafsi; mambo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa cha kutafuta na kudumisha amani. Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia kwani kuna hatari kushindwa kuchakata takwimu nyingi na hivyo kusababisha ukosefu wa haki na maamuzi mbele katika mazingira zilimotoka takwimu hizi, kumbe, binadamu anapaswa kufanya tathmini na hatimaye kutoa uamuzi wa mwisho. Hapa, kuna haja ya kufikiria ukomo katika teknolojia kamwe teknolojia isitumike kuzalisha utajiri kwa watu wachache ndani ya jamii na hivyo kuhatarisha demokrasia na amani katika ujumla wake.

Akili mnemba itumike kupunguza mateso ya watu duniani
Akili mnemba itumike kupunguza mateso ya watu duniani

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia pia masuala motomoto kwa maadili kwani hapa watu na haki zao msingi, utu na heshima yao vinahusishwa kwa ukaribu na hivyo mifumo hii ya teknolojia ya akili mnemba inaweza kusababisha ubaguzi, ukosefu wa haki na usawa katika jamii na hata wakati mwingine, kuathiri fikra na utendaji wa watu. Kumbe utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, sanjari na fadhila ya huruma, upendo na msamaha. Hapa haki za wafanyakazi na fursa za ajira zinapaswa kuzingatiwa, ili kwamba, matumizi ya teknolojia ya akili mnemba isiwe ni sababu ya wafanyakazi kukosa ajira. Je, tugeuze panga ziwe majembe? Kwa sasa matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kijeshi ni jambo la hatari sana kimaadili na kwamba, wajanja wachache wasije kuibuka na kuanza kuwekeza kwenye biashara ya silaha na hivyo kusababisha maafa makubwa ya vita, bali matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yasaidie kukoleza amani duniani; yaboreshe sekta ya kilimo, sekta ya elimu na maisha ya watu kwa kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mafungamano ya kijamii; pamoja na majadiliano katika ukweli na uwazi. Huu ndio mwelekeo wa kimaadili wa matumizi sahihi ya teknolojia ya akili mnemba. Kwa hakika teknolojia ya akili mnemba imeleta changamoto za kielimu katika mfumo wa kufundishia na majiundo ya wanafunzi. Wanafunzi wanapaswa kufundishwa kujikita katika upembuzi yakinifu, weledi na kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; kwa kujenga madaraja ya watu kukutana, ili kuishi kidugu na kwa amani.

Teknolojia ya akili mnemba isaidie maboresho katika kilimo
Teknolojia ya akili mnemba isaidie maboresho katika kilimo

Na hatimaye Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa zinazopaswa kukazia pamoja na mambo mengine ni umoja, mwongozo utakaoratibu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; kwa kuheshimu na kulinda haki msingi za binadamu, ili kudumisha misingi ya haki na amani sanjari na kusikiliza na kuzingatia maoni ya watu mbalibali mintarafu teknolojia ya akili mnemba. Baba Mtakatifu anahitimisha Ujumbe wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani” kwa kusema, amani ni matunda mafungamano yanayotambua utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kushirikiana na wengine kwa ajili ya ustawi wa wengine. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba ili mifumo yote ya akili mnemba itumike kupunguza mateso ya binadamu, kukuza maendeleo shirikishi na kusaidia kumaliza vita, kinzani na migogoro; na wala si kuongeza ukosefu wa usawa pamoja na uvunjaji wa haki za binadamu duniani.

Ujumbe wa amani 2024
30 December 2023, 15:46