Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, 14 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Usafirishaji wa Wagonjwa kwenye Madhahabu ya Lourdes na Maeneo Matakatifu ya Kitaifa na Kimataifa (U.N.I.T.A.L.S.I.) Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, 14 Desemba 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Usafirishaji wa Wagonjwa kwenye Madhahabu ya Lourdes na Maeneo Matakatifu ya Kitaifa na Kimataifa (U.N.I.T.A.L.S.I.) 

UNITALSI Kumbukizi ya Miaka 120 ya Huduma Kwa Wagonjwa: 1903-2023

UNITALSI Kumbukizi ya Miaka 120 tangu kuanzishwa kwake 1903 - 2023: Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa hija inayofumbatwa katika: Kuwapokea, Ukarimu na Mshikamano wa watu wote wa Mungu, alama hai ya Kanisa linalosafiri na watu wote, Umoja huu ni rejea kwa wagonjwa na familia zao; mwaliko wa kujiaminisha kwa Bikira Maria. Huu ni ushuhuda wa Kanisa linalowasindikiza, wahudumia wagonjwa na kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Kitaifa wa Usafirishaji wa Wagonjwa kwenye Madhahabu ya Lourdes na Maeneo Matakatifu ya Kitaifa na Kimataifa (U.N.I.T.A.L.S.I.) unajikita katika kutoa huduma kwa wagonjwa katika safari ya kutembelea Madhabahu ya Kitaifa na Kimataifa. Kilianzishwa kunako mwaka 1903 na Giovanni Battista Tomassi akiwa na umri wa miaka 22 na mwaka 2023 kinafanya kumbukizi ya Miaka 120 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chama kinachowahusisha watu wa kujitolea, wagonjwa, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na mapadre vijana. Huu ni ushuhuda wa uzuri wa Kanisa linalowasindikiza, wahudumia wagonjwa sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo. Mama Kanisa anawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika huduma hii muhimu kwa wagonjwa, kama hija ya kumwendea Bikira Maria, huku wakisukumwa na tunu msingi za Kiinjili kuendelea kumkazia macho Bikira Maria. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 14 Desemba 2023 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Kitaifa wa Usafirishaji wa Wagonjwa kwenye Madhahabu ya Lourdes na Maeneo Matakatifu ya Kitaifa na Kimataifa (U.N.I.T.A.L.S.I.) waliomtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa hija inayofumbatwa katika: Kuwapokea, Ukarimu na Mshikamano wa watu wote wa Mungu, alama hai ya Kanisa linalosafiri na watu wote, Umoja huu ni rejea kwa wagonjwa na familia zao, changamoto na mwaliko wa kujiaminisha kwa Bikira Maria.

Wagonjwa wajiaminishe chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria
Wagonjwa wajiaminishe chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria

Baba Mtakatifu anasema, huu ni ushuhuda wa uzuri wa Kanisa linalowasindikiza, wahudumia wagonjwa sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo. Huu ni wito na mwaliko wa kuendelea kutunza ari na moyo wa hija inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Injili sanjari na kuendelea kumkazia macho Bikira Maria. Chama hiki kilianzishwa na Giovanni Battista Tomassi akiwa na umri wa miaka 22 baada ya kupata mang’amuzi na faraja katika sala wakati wa hija yake kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes yanayoendelea kuwa ni chemchemi ya faraja kwa wagonjwa na walemavu; wazee na wahitaji wanaosindikizwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes na Madhabahu mengine yaliyotawanyika ndani na nje ya Italia. Hii ni safari ya maisha na uponyaji, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa miongoni mwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka. Waamini wanakumbushwa kwamba, hapa duniani watu wote ni mahujaji na wapita njia, kumbe wanapaswa kuutafakari Uso wa Kristo Yesu aliyebeba mwilini mwake udhaifu na magonjwa ya mwanadamu ili aweze kumkomboa kwa nguvu ya Ufufuko. Hija kimsingi inafumbata ndani mwake tunu msingi za kuwapokea, ukarimu na mshikamano wa kuwapokea watu wa Mungu, kiasi kwamba, hiki kinakuwa ni kielelezo hai cha Kanisa linalotembea na watu wote na hakuna anayeachwa nyuma, kielelezo cha Kanisa ambalo ni “Hospitali” katika Uwanja wa vita na Msamaria Mwema aliyemwona yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai. Rej. Lk 10:34 katika hali ya ukimya kwani katika mateso na mahangaiko ujirani mwema unachukua nafasi ya maneno na kwamba, huu ni muda wa kumwilisha upendo katika matendo, huu ndio mtindo wa maisha ya U.N.I.T.A.L.S.I.

Huduma kwa wagonjwa ni kielelezo cha Msamaria Mwema
Huduma kwa wagonjwa ni kielelezo cha Msamaria Mwema

Baba Mtakatifu anasema, Umoja wa Kitaifa wa Usafirishaji wa Wagonjwa kwenye Madhahabu ya Lourdes na Maeneo Matakatifu ya Kitaifa na Kimataifa umekita mizizi ya huduma nchini Italia na kinajielekeza zaidi katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Neno la Mungu daima liwe ni lishe katika safari ya maisha yao kwani hili ni Neno linaloganga na kuponyesha; Neno linalosamehe na kufariji; Ni Neno linalotoa matumaini na kwamba, nyuma yake yuko Mwenyezi Mungu anayewategemeza ikiwa kama nguvu zitawapungukia. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa U.N.I.T.A.L.S.I. kujiaminisha kwa Bikira Maria, huku wakiendelea kumtafuta, kumtafakari na kumwomba, ili aweze kuwafariji kutokana na magumu, machungu na maumivu ambayo kila mmoja anayabeba ndani mwake. Kumbukizi hii imewawezesha U.N.I.T.A.L.S.I kufanya hija inayowajumuisha watu wengi wa Mungu kutoka katika medani mbalimbali za maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati huu, Mama Kanisa anapoelekea katika Maadhimisho ya Noeli ya Bwana, Bikira Maria anaonekana kuwa karibu sana na waamini, mwaliko ni kumwachia nafasi ili aweze kuwaangalia, ili hatimaye waweze kujifunza kusema “Ndiyo” na hivyo kupokea mipango ya Mungu katika maisha yao bila ya kuwa waoga na hivyo kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa. Bikira Maria ni hujaji wa imani na matumaini aendelee kuwasinsikiza wajumbe wa U.N.I.T.A.L.S.I. katika maisha yao na huduma kwa wagonjwa.

Unitalsi 120

 

14 December 2023, 14:36