Tafuta

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27. Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27.  

Askofu Alex Malalusa: Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Upendo Kwa Mungu na Jirani

Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu: Tukio la kusimikwa kwake kuwa Mkuu wa KKKT; Umoja wa Wakristo Tanzania; Majadiliano ya Kiekumene nchini Tanzania pamoja na changamoto zake: Injili ya mafanikio, Chaguzi za kisiasa pamoja na mchango wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene! Ushuhuda wa Upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27. Tafakari ya Mwaka 2024 imetungwa na Jumuiya ya Kiekumene kutoka Burkina Faso, ambayo imejikita katika umuhimu wa kumwilisha: Upendo, amani na upatanisho kama njia mahususi ya kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 17 Januari 2024, amewaalika Wakristo ili kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo, ili hatimaye waweze kufikia umoja kamili na hivyo kushuhudia kwa pamoja: huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, lakini upendeleo wa pekee ni kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na tilimifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa ndani; sadaka na upendo kwa Mungu na jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwapekenya na kuwatafuna taratibu Wakristo. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi kitakatifu, kufuatana na tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ushirikiano huu ujengeke katika: sala, huku Wakristo wenyewe wakijitahidi kufahamiana; kufundisha kwa kuzingatia mchakato kiekumene na kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Rej. Lumen gentium 5-11.

Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani
Askofu Alex Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani

Ni katika muktadha huu, Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliyezaliwa tarehe 18 April, 1961 katika kijiji cha Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Tanzania, na kuchaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania anayetarajiwa kusimikwa rasmi kwa awamu hii ya pili hapo tarehe 21 Januari 2024, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu: Tukio la kusimikwa kwake kuwa Mkuu wa KKKT; Umoja wa Wakristo Tanzania; Majadiliano ya Kiekumene nchini Tanzania pamoja na changamoto zake: Injili ya mafanikio, Chaguzi za kisiasa pamoja na mchango wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani inayounganisha mkoa wa Dar es Salaam, Pwani Unguja na Pemba, tarahe 21 Januari 2024 anasimikwa rasmi kama Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, hii ikiwa ni awamu ya pili, baada ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumchagua kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania. Askofu Malasusa ana mshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumkirimia utume huu mpana na anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala sanjari na kudumisha ushirikiano na mshikamano. Ujumbe mahususi kwa watu wa Mungu nchini Tanzania ni kwamba, watambue kuwa Mwenyezi Mungu anaita watu wake, kwa wakati wake na kwa mapenzi yake; jambo muhimu ni ushirikiano, kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na bidii ili kutekeleza makusudi ya Mungu kwa wakati huu. Hii ni changamoto kwa Kanisa la Mungu nchini Tanzania kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kuinjilisha pamoja na kumwakilisha Mungu katika maisha na utume huu. Na kwa njia ya unyenyekevu wawe tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, ili waweze kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa,  linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa anasema, umoja wa Wakristo Tanzania unajidhihirisha kuanzia ngazi za chini kabisa kwa Wakristo kushirikiana na kushikamana katika medani mbalimbali za maisha, kiasi hata cha kufikia hatua ya kufunga ndoa za mseto. Kuna ushirikiano mwema kati ya viongozi wa Makanisa nchini Tanzania na kwamba, wanaendelea kujifunza. Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania (CSSC), ni kiungo muhimu sana katika huduma ya “Diakonia.” Lengo la Tume hii ni kuimarisha huduma za kijamii zinazotolewa na Makanisa ya Kikristo nchini Tanzania kwa kuhakikisha kwamba, elimu makini na huduma bora ya Afya inawafikia hata maskini. Tume hii imekuwa mstari wa mbele kuragibisha huduma makini za kijamii kwa watanzania pamoja na kuyajengea Makanisa uwezo wa kupambana na: umaskini, ujinga na magonjwa. Tume imekuwa mstari wa mbele katika miradi ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, magonjwa yanayosababisha vifo vya watu wengi nchini Tanzania. Tume imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukarabati miundo mbinu ya Shule na Afya kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya huduma ya afya inayopania kudumisha utu na heshima ya binadamu! Huduma hii ni ushuhuda wa upendo wa Kristo Yesu kwa watanzania.

Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii Tanzania, CSSC ni kiungo muhimu
Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii Tanzania, CSSC ni kiungo muhimu

Kuna mambo makuu matatu ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza: Uekumene wa Upendo, Ukweli pamoja na Uekumene wa umoja, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu! Haya ni mambo msingi ambayo viongozi wa Kanisa tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamejitahidi kuyavalia njuga katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa anasema, majadiliano ya kiekumene yamepata sura mpya na inayoonekana nchini Tanzania kwa waamini kufanya kazi kwa pamoja. Anasema, hata yeye kukaribishwa na hatimaye, kufanya mahojiano maalum na Radio Vatican ni jambo ambalo lisingewezekana miaka kadhaa iliyopita, lakini leo hii, Makanisa yanashirikiana sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Waamini wangependa kuona ushirikiano huu unaboreshwa zaidi kwa sababu ni chanzo cha neema na baraka kama inavyojionesha kati yake na Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. wa Jimbo Katoliki Zanzibar. Wakristo hata katika uchache wao Zanzibar, lakini umoja na ushirikiano huu unawafanya wawe na nguvu kama Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa na hivyo kumwinua Kristo Yesu kwa pamoja kama Wakristo!

Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani
Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani

Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani anasema kati ya changamoto zinazolikabili Kanisa kwa sasa ni “Injili ya Mafanikio ya chapuchapu” inayowavuta vijana wengi wa kizazi kipya, lakini inawadumaza na kuwadekeza. Mafanikio bila kuchapa kazi kwa: akili, juhudi na maarifa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kanisa linapaswa kubaini taalimungu za mafanikio, kwa sababu ni potofu. Changamoto ya pili ni wanasiasa wengi wakati za chaguzi za kisiasa Barani Afrika hupenda kuyatumia Makanisa kujinadi na kujitafutia umaarufu. Na kwamba, kwa nchi nyingi za Kiafrika mara baada ya uchaguzi mara nyingi yanatokea machafuko jambo ambalo halifai hata kidogo. Makanisa yatumike kuonya, kujenga na kudumisha ushirikiano na mafungamano ya kweli na wanasiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao; amani na haki na kwamba, Kanisa liendelee kuwa ni sauti kwa wale wasiokuwa na sauti. Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani linaendelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani kwa kuangalia yaliyopita kwa toba, ili kuweza kuyaambata ya leo kwa imani, matumaini na mapendo. Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita mchakato wa majadiliano ya kiekumene umechukua kasi kubwa na kupata sura mpya zaidi inayojikita katika ushuhuda wa pamoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo! Ikumbukwe kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni msingi wa mapambazuko ya majadiliano ya kiekumene ambayo yanaendelea kuboreka siku hadi siku kwa matumaini kwamba, siku moja kadiri ya mapenzi ya Roho Mtakatifu, Makanisa yote yatakuwa chini ya Kristo Yesu mchungaji mkuu. historia iliyopita kwa Makanisa mengi, iligubikwa na chuki, vita na ghasia za kidini zilizobebwa na matamanio ya kisiasa na kiuchumi pengine kuliko hata na imani ya Kanisa.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican Pentekoste Mpya kwa Kanisa Katoliki.
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican Pentekoste Mpya kwa Kanisa Katoliki.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Benedikto XVI wamechangia sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Lakini, kwa mshangao mkubwa, Baba Mtakatifu Francisko ameweka majadiliano ya kiekumene kama moja ya vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na matunda yake yanaonekana katika mahusiano na mafungamano ya Wakristo katika medani mbalimbali za maisha. Ni mwelekeo, mtazamo na hisia tofauti kabisa zilizowawezesha waamini wa Kanisa la Kiluteri kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuungana na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani! Miaka kadhaa iliyopita, ndoto ya namna hii, isingeweza kuwepo! Hili tukio lilihudhuriwa pia na Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kwake tukio hili lilikuwa ni mwendelezo wa mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ya kujenga na kudumisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kumbe, majadiliano ya kiekumene yanafumbatwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuthubutu kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukatishwa tama na magumu pamoja na changamoto za maisha! Makanisa yanahamasishwa kujikuta katika uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa huduma na ushuhuda wa damu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Majadiliano ya kekumene katika masuala ya kitaalimungu yataendelea ili kuwasaidia waamini kutambua imani, maisha na utume wa Kanisa. Ni mchakato ambao unapaswa pia kuyahusisha Makanisa ya Kiinjili ya Kipentekosti ambayo kwa miaka mingi yalitelekezwa pembezoni mwa majadiliano ya kiekumene kimataifa!

Uekumene Tanzania
17 January 2024, 13:36