Askofu Mkuu Mar Raphael Thattil wa Ernakulam-Angamaly, Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar. Uteuzi wake umethibitishwa na Papa Francisko. Askofu Mkuu Mar Raphael Thattil wa Ernakulam-Angamaly, Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar. Uteuzi wake umethibitishwa na Papa Francisko.  (AFP or licensors)

Askofu Mkuu Mar Raphael Thattil wa Ernakulam-Angamaly, Athibitishwa na Papa Francisko

Ni katika muktadha wa uteuzi huu, uliofanywa na Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar mintarafu Sheria za Kanisa la Mashariki namba 153, Baba Mtakatifu ameithibitishia Sinodi hii kuhusu uteuzi huu na kwamba, Askofu mkuu Mar Raphael Thattil, wa Ernakulam-Angamaly wa Madhehebu ya Kisiria la Malabar sasa anakuwa kwao kama: Baba na Mkuu wa Kanisa, ili kunogesha mahusiano na mafungamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Mar Raphael Thattil, kuwa Askofu mkuu wa Ernakulam-Angamaly wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar. Hili ni mojawapo kati ya madhehebu ya Kikristo kutoka Mashariki yenye ushirika kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa Katoliki katika ujumla wake. Ni Kanisa linalofuata Mapokeo ya Mesopotamia na kutumia liturujia ya Mesopotamia, lakini linapatikana hasa India na katika nchi mbalimbali ambapo waamini wake wamehamia, kama vile Marekani, ambako lina majimbo mawili, na Canada, Australia na Uingereza ambako kuna jimbo mojamoja. Askofu mkuu mteule Mar Raphael Thattil, alizaliwa tarehe 21 Aprili 1956 huko Trichur. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 21 Desemba 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika maisha na utume wake kama Padre amewahi kuwa Gambera wa kwanza wa Seminari ya Mary Matha kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2007, ambako amechangia kwa kiasi kikubwa, ustawi na maendeleo ya Seminari hii. Tarehe 18 Januari 2010 akateuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Askofu Msaidizi na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Msaidizi tarehe 10 Aprili 2010.

Papa Francisko athibitisha uteuzi wa Askofu mkuu Mar Raphael Thattil
Papa Francisko athibitisha uteuzi wa Askofu mkuu Mar Raphael Thattil

Tarehe 23 Desemba 2013 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwakilishi wa Kitume wa waamini wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar wanaoishi nchini India, nje ya majimbo yao ya asili. Tarehe 10 Oktoba 2017 kulianzishwa “Eparkia mpya ya Shamshabad” na hivyo kuteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa “Eparkia ya Shamshabad.” Na ilipogota tarehe 9 Januari 2024 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Ernakulam-Angamaly wa Madhehebu ya Kisiria la Malabar. Ni katika muktadha wa uteuzi huu, uliofanywa na Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar mintarafu Sheria za Kanisa la Mashariki namba 153, Baba Mtakatifu Francisko ameithibitishia Sinodi hii kuhusu uteuzi huu na kwamba, Askofu mkuu Mar Raphael Thattil, wa Ernakulam-Angamaly wa Madhehebu ya Kisiria la Malabar sasa anakuwa kwao kama: Baba na Mkuu wa Kanisa, ili kunogesha mahusiano na mafungamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anamtaka aendelee kufuata mifano bora ya watangulizi wake, huku akijisadaka kwa ajili ya utume kwa kundi ambalo amekabidhiwa na Mama Kanisa chini ya ulinzi wake. Katika maisha na utume wake, kamwe asiwasahau maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Roho Mtakatifu aendelee kukoleza umoja na utume wa Kanisa Katoliki Madhehebu ya Kisiria la Malabar. Baba Mtakatifu anamwomba Askofu mkuu, amfikishie salam na matashi mema kwa Mababa wa Sinodi pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wao; amemhakikishia uwepo wake wa karibu na hatimaye, amempatia baraka zake za Kitume.

Uteuzi
11 January 2024, 14:56