Wajumbe wa Chama cha Wanataaluma Vijana wa Mwenyeheri Toniolo, Ijumaa tarehe 12 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wajumbe wa Chama cha Wanataaluma Vijana wa Mwenyeheri Toniolo, Ijumaa tarehe 12 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Umuhimu wa Vijana Kuwa ni Vyombo vya Matumaini, Wabunifu na Wajenzi wa Amani

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amegusia kuhusu: Umuhimu wa vijana kuota ndoto na kuangalia ya mbeleni kwa matumaini, wadumishe kipaji cha ubunifu na kuthubutu kuwa ni wajenzi wa uzuri na utulivu na kwamba, Mwenyeheri Toniolo awe ni mfano bora wa kuigwa na kwamba, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani duniani. Vijana wajisadake kutafuta ukweli, uzuri na utulivu kwa kuwa na matumizi bora ya mitandao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

TYPA, “Toniolo Young Professional Association” ni Chama cha Wanataaluma Vijana wa Mwenyeheri Toniolo kilichoanzishwa mwezi Aprili 2016 na huwakusanya pamoja vijana wanaofadhiliwa kimasomo na Taasisi ya Toniolo pamoja na Mabalozi wa Vatican katika nchi mbalimbali na katika Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa ya UNESCO, Baraza la Ulaya, OSCE pamoja na Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji katika Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Hivi karibuni “The Arverd Buschini Foundation” yaani Mfuko wa Arved Buschini ulioanzishwa kunako mwaka wa 1990 umejiunga kutoa ufadhili. Huu ni mpango wa maendeleo wa familia ya Arvedi, kusaidia kugharimia shughuli za maendeleo na kukuza mipango inayolenga kuinua elimu, ustawi, maendeleo na uthamini urithi wa kisanii na kitamaduni. Kwa ushiriki wa Mfuko wa Arvedi, idadi ya vijana wanaofadhiliwa kimasomo imeongezeka maradufu. Wajumbe wa Chama cha Wanataaluma Vijana wa Mwenyeheri Toniolo, Ijumaa tarehe 12 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake amegusia kuhusu: Umuhimu wa vijana kuota ndoto na kuangalia ya mbeleni kwa matumaini, wadumishe kipaji cha ubunifu na kuthubutu kuwa ni wajenzi wa uzuri na utulivu na kwamba, Mwenyeheri Giuseppe Toniolo awe ni mfano bora wa kuigwa na kwamba, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani duniani. Vijana hawa kwa njia ya Mabalozi wa Vatican wanahusiana moja kwa moja na Khalifa wa Mataifa Petro na hivyo kukuza ndani mwao uzoefu wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na hivyo kuendelea pia kupyaisha taasisi za kipapa na hivyo kuwawezesha vijana kuendelea kuota ndoto sanjari na kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini.

Chama cha Wanataaluma Vijana wa Toniolo
Chama cha Wanataaluma Vijana wa Toniolo

Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kukuza na kudumisha kiwango cha kufikiri na kutenda kwa kujikita katika kipaji cha ubunifu, kwani mawazo mgando yanawajenga katika tabia ya kukosoa kila kitu, kurahisha sanjari na kupindisha mambo, kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi, bila kuangalia ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zake. Kumbe, vijana wanapaswa kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kutoka ndani kabisa mwa nyoyo zao! Inasikitisha kuona vijana “wakiponda mali eti kufa kwaja, wakila kuku kwa mirija.” Lakini, kimsingi Kanisa na jamii kwa ujumla inawataka vijana kukuza na kudumisha ndani mwao kipaji cha ubunifu, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta ukweli, uzuri na utulivu na hivyo kuondokana na matumizi mabaya ya njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii. Vijana wa kizazi kipya wawe ni watu wa sala, wajisadake bila ya kujibakiza katika huduma ya upendo inayoleta mageuzi. Wafanye kazi si kwa kusubiri kulipwa,  bali wagunduzi wanaoweza kuleta mapinduzi makubwa katika maisha ya mwanadamu na kamwe wasitatute faida kubwa katika maisha na kwa njia hii, kwa hakika wanaweza kuwa ni watu wa mapinduzi. Mwenyeheri Giuseppe Toniolo katika maisha na utume wake, alijichotea nguvu kwa kuishi kikamilifu imani yake, iliyomwilishwa katika uhalisia wa maisha, akapembua kwa kina na mapana matatizo, changamoto na fursa zilizokuwa mbele yake na matatizo katika maisha na utume wake akayapatia sura ya uchumi wa kibinadamu, kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi.

Chama cha Wanataaluma Vijana wa Toniolo: amani, ubunifu, ukweli na ubunifu
Chama cha Wanataaluma Vijana wa Toniolo: amani, ubunifu, ukweli na ubunifu

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia: Ustawi na maendeleo, amani na utulivu kati ya watu wa Mungu; kwa kuendelea kuota ndoto na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kujikita katika sera za kuzuia vita,  na kujenga amani ya kweli ulimwenguni bila madhara ya kukimbilia katika matumizi ya silaha. Vita ni matokeo ya matumizi ya nguvu, kumbe vijana wanapaswa kusimika maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili ili kuandika kurasa mpya za udugu wa kibinadamu zinazosheheni Injili ya matumaini. Vijana wawe mstari wa mbele katika ujenzi wa uchumi shirikishi, mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaosigina, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wasimame kidete kupinga biashara haramu ya silaha duniani; wajitahidi kuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote. Wajitahidi kuwa ni watumizi wazuri wa njia za mawasiliano ya jamii; kwani mambo yote haya yanahitaji kujikika katika mchakato wa upyaishaji kwa kuthamini kipaji cha ubunifu. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwakabidhi vijana hawa wa kizazi kipya ndoto ya Mzee, akiwa na shauku ya kuona nyuso za vijana kwani hata Kristo Yesu ana moyo wa kijana na anawaita vijana kumfuata.

Vijana

 

 

12 January 2024, 15:33