Tafuta

Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 10 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wanachama wa mradi wa DIALOP kwa kukazia mchakato wa majadiliano. Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 10 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wanachama wa mradi wa DIALOP kwa kukazia mchakato wa majadiliano.  (Vatican Media)

DIALOP: Majadiliano Katika Ukweli na Usawa! Heshima na Udugu

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 10 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wanachama wa mradi wa DIALOP kwa kukazia mchakato wa kuvunjilia mbali mipango ya kale ili kuanza kujikita katika njia mpya za majadiliano; kipaumbele ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukazia utawala wa haki na sheria. Waendelee kuota ndoto ya uhuru wa kweli na usawa; utu, heshima na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

DIALOP ni mradi mkubwa wa majadiliano kati ya Wasoshalisti/Wamarx na Wakristo, unaowahusisha wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wanafunzi kutoka Nchi kadhaa za Ulaya. DIALOP ina amini kwamba, majadiliano ndiyo njia bora ya kufanya mabadiliko ya kweli, ili kuugeuza ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Uzoefu wa DIALOP ulianza tarehe 18 Septemba, 2014, wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wanasiasa wawili wa mrengo wa kushoto: Alexis Tsipras kutoka Ugiriki na Walter Baier kutoka Austria, pamoja na Franz Kronreif kutoka Chama cha Kitume cha Wafokolari. Majadiliano yao yalijikita katika mzozo wa mazingira na kijamii Kimataifa na hatimaye, Baba Mtakatifu akawaalika kuanzisha mchakato wa majadiliano ya pande zote ambayo yangewahusisha na kuwashirikisha wadau kutoka medani mbalimbali za maisha na hasa zaidi vijana wa kizazi kipya.

DIALOP kwa ajili ya majadiliano yanayowashirikisha hata vijana
DIALOP kwa ajili ya majadiliano yanayowashirikisha hata vijana

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 10 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wanachama wa mradi wa DIALOP kwa kukazia mchakato wa kuvunjilia mbali mipango ya kale ili kuanza kujikita katika njia mpya za majadiliano; kipaumbele ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukazia utawala wa haki na sheria. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa DIALOP kujikita katika mchakato wa kuona na kuota, bila kukata tamaa na kurudi nyuma juu ya ndoto ya kuwa na ulimwengu ulio bora zaidi wa kuishi. Hii ni ndoto ya uhuru wa kweli na usawa; utu, heshima na udugu wa kibinadamu unaozalisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

DIALOP ilianzishwa rasmi tarehe 18 Septemba 2014
DIALOP ilianzishwa rasmi tarehe 18 Septemba 2014

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kujikita katika mchakato wa kuvunjilia mbali mipango ya kale, ili kuanza kujikita katika njia mpya za majadiliano zinazojikita katika utamaduni wa kusikiliza na ushirikishwaji wa wadau kutoka medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu katika ngazi ya: kisiasa, kijamii na kidini, ili kila mtu aweze kuchangia katika mchakato wa mabadiliko ulimwenguni, kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, watu wasiokuwa na ajira, watu wasiokuwa na makazi maalum; wakimbizi na wahamiaji. Wanasiasa wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya huduma bora kwa binadamu, kwa kujikita katika mafungamano na mshikamano; huku wakiongozwa na kanuni maadili na utu wema; mahitaji msingi ya haki, yanayodai pia kusafisha dhamiri ili kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mamboleo.

DIALOP kipaumbele cha kwanza ni maskini
DIALOP kipaumbele cha kwanza ni maskini

Kumbe, huu ni mwaliko wa kuweka kipaji cha ubunifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kweli jamii ya binadamu iweze kusimikwa katika utu na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakazia utawala wa haki na sheria ili kupambana kikamilifu na rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma sanjari na matumizi mabaya ya madaraka, tayari kujenga na kudumisha mahusiano mema, ili kushirikiana na kuendelea kuaminiana ili kujenga jamii bora zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka wajumbe hawa kujikita kikamilifu katika majadiliano, bila ya kuwa na woga, bali waendelee kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa hekima na ujasiri, ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na amani.

DIALOP Majadiliano

 

10 January 2024, 14:04