Tafuta

Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 184 kutoka Cyprus akitoa hotuba ya salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 184 kutoka Cyprus akitoa hotuba ya salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko  (Vatican Media)

Diplomasia ya Majadiliano Katika Ukweli na Uwazi; Ustawi na Maendeleo ya Wengi

Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 184 kutoka Cyprus katika hotuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya salam na matashi mema kwa Mwaka mpya wa 2024 amejikita katika diplomasia ya majadiliano; “Vita Kuu ya Tatu ya Dunia” inayopiganwa vipande vipande; Amani ya kweli inasimikwa katika huduma kwa maskini pamoja na teknolojia ya akili mnemba; utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 8 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo na utaratibu wa kutakiana heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2024. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Diplomasia ya Vatican; Ujenzi wa Amani Duniani; Utendaji wa kiuchumi kijamii, na Ufalme wa Kristo Yesu; Biashara haramu ya silaha; Athari za Mabadiliko ya Tabianchi; Maabara ya Amani; Wimbi kubwa la Wakimbizi na Wahamiaji; Miaka 75 ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu na Ukoloni wa Kiitikadi; Majadiliano katika ukweli na uwazi; Elimu kwa vijana wa kizazi kipya; Akili Mnemba, Artificial Intelligence; pamoja na Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 2025. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema, “Familia ya Diplomasia” ya Vatican imeongezeka baada ya Sultani wa Omani kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican pamoja na kumteuwa Balozi wake wa kwanza na hivyo Vatican kwa sasa ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184. Vatican na Vietnam katika kipindi cha Mwaka 2023 vimekamilisha Mkataba kuhusu Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam, lengo ni kuendeleza mahusiano na ushirikiano kati ya Serikali ya Vietnam na Kanisa mahalia. Mwaka 2023 umeshuhudia kuridhiwa kwa Nyongeza ya Mkataba wa makubaliano wa tarehe 23 Septemba 1998 kati ya Vatican na Kazakhstan unao rahisisha utendaji wa wahudumu katika shughuli za kichungaji.

Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Vatican pia imeafanya kumbukizi ya Miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia na Panama, Miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia Iran pamoja na miaka 60 na Jamhuri ya Watu wa Corea sanjari na miaka 50 ya uhusiano ya kidiplomasia na Australia. Baba Mtakatifu anasema amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu. Zawadi ya amani imesikika kutoka kwa Malaika, alipozaliwa Kristo Yesu na alipofufuka kwa wafu, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutafuta, kuijenga na kuidumisha amani na kwamba, Vatican itaendelea kuwa ni sauti ya kinabii katika Jumuiya ya Kimataifa ili kuasha dhamiri za watu. Kunako tarehe 24 Desemba 1944, Papa Pio XII alizungumzia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani ulimwenguni baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, kwa binadamu kupyaisha maisha kutoka katika undani wao. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata baada ya miaka 80 tangu Vita ya Pili ya Dunia ilipotokea, bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kielelezo cha Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia.

Diplomasia ya majadiliano katika ukweli na uwazi
Diplomasia ya majadiliano katika ukweli na uwazi

Kwa upande wake, Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 184 kutoka Cyprus katika hotuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya salam na matashi mema kwa Mwaka mpya wa 2024 amewasilisha salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2024 kwa kujikita katika diplomasia ya majadiliano katika kukabiliana na “Vita Kuu ya Tatu ya Dunia” inayopiganwa vipande vipande na kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Dubai, Hija za Kitume za Baba Mtakatifu, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni na mwisho amemtakia Baba Mtakatifu heri na baraka kwa mwaka 2024. Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, amewakumbuka watu wote wanaoathirika kutokana na “Vita Kuu ya Tatu ya Dunia” inayopiganwa sehemu mbalimbali za dunia, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kuwa ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa amani duniani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika diplomasia ya majadiliano ili kuwaunganisha watu na kuondokana na yale mambo yanayowagawa na kuwatenganisha watu. Ulimwengu mamboleo unaendelea kukabiliana na changamoto za kiutu, athari za mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, vita; changamoto ambazo zinahitaji kupata majibu muafaka kwa kujikita katika sera zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza, kama kikolezo cha amani duniani.

Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba
Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba

Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 imenogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa. Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafunagamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za watu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba iwe inategemewa. Balozi Georgios F. Poulides amegusia kuhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unaokita ujumbe wake juu ya: Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP 28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji.

Laudate Deum
Laudate Deum

Balozi Georgios F. Poulides amegusia pia Hija za Kitume za Baba Mtakatifu huko Mongolia, DRC na Sudan ya Kusini na Marseille, Ufaransa kwa kukazia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, binadamu awe ni kipimo cha maendeleo, kwa kujikita zaidi na zaidi katika haki, amani na upatanisho; ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 - 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Kwa hakika vijana wa kizazi kipya wanazo nguvu za ajabu zinazoweza kuleta mabadiliko katika ulimwengu mamboleo ambao “unachechemea”, kwa kujenga mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani yaani wazee, ili kuibua sera na mbinu mkakati utakaosaidia kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi. Mwishoni amemtakia Baba Mtakatifu heri na baraka kwa Mwaka mpya 2024, afya njema na kuendelea kuwa na matumaini ya maboresho, ili ulimwengu huu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Diplomasia ya Majadiliano
09 January 2024, 14:11