Iran,masikitiko makubwa ya Papa kwa wahanga wa milipuko huko Kerman
Vatican News
Ni masikitiko makubwa kwa upande wa Baba Mtakatifu Francisko kwa kupoteza maisha ya binadamu yaliyosababishwa na milipuko ya hivi karibuni huko Kerman, katikati kusini mwa Iran. Katika telegram iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican anabainisha kuwa Papa anatuma rambirambi zake na kuombea wale waliofariki na kwa ajili ya familia zao zinazoomboleza. Akionesha kwa njia sawa mshikamano wake wa kiroho na waliojeruhiwa, Papa Francisko “anaomba baraka za Mwenyezi wa hekima na amani juu ya watu wote wa Iran.”
Kuhusiana na milipuko hiyo ilitokea ndani ya dakika 20 kwa kila mmoja mnamo tarehe 3 Januari 2024 karibu na kaburi la Kerman, ambapo maelfu ya mahujaji walikuwa wanakwenda kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kifo cha Qassem Soleimani, aliyekuwa mkuu wa Vikosi vya Walinzi wa Qods wa Mapinduzi ya Iran, aliyeuawa mnamo tarehe 2 Januari 2020, nchini Iraq katika operesheni iliyoongozwa na Marekani. Idadi ya waliofariki kwa sasa ni karibu 100 na zaidi ya 280 wajeruhiwa. Mauaji hayo yalidaiwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu ambalo kwenye chaneli zake za Telegram liliweka jukumu la mashambulizi dhidi ya washambuliaji wake wawili wa kujitoa mhanga. Video na habari za moja ya shambulio kali zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini Iran pia ilitumwa kwenye mitandao ya kijamii.