Jubilei ya Miaka 100 Tangu Kuzaliwa kwa Don Lorenzo Milani: Elimu na Maskini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Don Lorenzo Milani aliamini neno kama msingi na kanuni ya ujenzi wa usawa, alionesha ukaribu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumimizwa pembezoni mwa jamii. Ujuzi wa lugha ni chachu ya ukombozi. Jukumu lake kama Mwalimu na uzoefu wake wa kufundisha watoto waliotoka katika familia maskini huko Barbinana uliashiria njia ambapo maono ya Kanisa, shule, demokrasia na maisha ya kujitolea viliwekwa bayana. Kumbukizi ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Don Lorenzo Milani: 1923 -2023 ni kuendeleza maono ya jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki na uhuru, ili kujenga na kudumisha usawa. “I Care, maana yake “Ninajali” ni ujumbe makini unaopania pamoja na mambo mengine, kufutilia mbali ukosefu wa usawa ndani ya jamii. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 22 Januari 2024 amekutana na Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Jubilei ya Miaka 100 Tangu alipozaliwa Don Lorenzo Milani. Katika hotuba yake alijikita katika wongofu wa ndani, alijitahidi kumwilisha Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika vipaumbele vya maisha yake. Alikuwa ni shuhuda wa mageuzi makubwa ya kijamii, kiuchumi na maendeleo makubwa ya viwanda na kwamba, elimu bora na makini ni chachu ya maendeleo.
Huu ni ushuhuda na urithi ambao Don Lorenzo Milani kama: Padre, Mwalimu, Nabii na Mtu wa Mungu! Hii ni kamati ambayo inajizatiti kuhakikisha kwamba, ushuhuda na ujumbe wa Don Lorenzo Milani unawafikia watu wengi zaidi, lakini hasa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wongofu wa ndani kwa Kristo Yesu ulikuwa ni mchakato wa maisha na utume wake kama Padre. Huu ni wongofu unaokita mizizi yake katika moyo na mang’amuzi yake ya kiutu na kiroho na kwanza kabisa kama mwamini na padre, alilipenda sana Kanisa pamoja na kuhakikisha kwamba, anakuwa ni mtumishi mwaminifu wa Injili na maskini. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Don Lorenzo Milani alijitahidi kuzimwilisha Heri hizi katika unyenyekevu, huduma makini kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, wote hawa akawaonjesha Injili ya upendo na hivyo kutambulika na wengi kuwa ni Padre shujaa aliyetafuta kuzima kiu ya njaa na haki miongoni mwa watu wake na kwamba, shule ilikuwa ni mahali muafaka pa kumrudishia maskini: utu, heshima na haki zake msingi na kutambua kwamba, kwa hakika ni mwana mpenda wa Mungu.
Yote haya ni matunda ya mang’amuzi ya shughuli zake za kichungaji yaliyomwezesha kutambua na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mtu! Don Lorenzo Milani ni shuhuda aliyebahatika kuona mageuzi makubwa ya kijamii, kiuchumi pamoja na maendeleo makubwa ya viwanda yaliyowasukuma watu kutoka vijijini kwenda mijini kutafuta fursa za kazi na ajira. Katika hali na mazingira kama hawa, cheche za ubaguzi zilianza kujitokeza hata katika shule za Serikali. Shule badala ya kuwa ni mahali pa kumwendeleza mtu kijamii, zikageuzwa kuwa ni sehemu ya kuchochea ubaguzi. Lakini, Don Lorenzo Milani, akageuza shule kuwa ni mahali muafaka pa kuwainjilisha vijana wa kizazi kipya, kwa kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwarithisha imani. Akagundua kwamba, elimi ilikuwa ni kitovu cha maendeleo endelevu na fungamani kwa binadamu.
Maskini akawapatia kipaumbele cha kwanza na kwamba, juhudi zote hizi zilinogeshwa na kauli mbiu: “I care” yaani “Ninajali.” Huu ni urithi wa kudumu kutoka kwa Don Lorenzo Milani, changamoto na mwaliko kwa jamii mamboleo kugundua mifumo mipya ya umaskini na maskini, ili kuwatafutia ufumbuzi wa kudumu. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na kila mwamini anasema Baba Mtakatifu Francisko. Don Lorenzo Milani alibahatika kukutana na ukweli kuhusu maisha yake kwa kukutana na Kristo Yesu na kushikamana nao hadi kifo. Kumbe, kumbukizi ya Jubilei ya Miaka Mia Moja tangu Don Lorenzo Milani alipozaliwa ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa huyu Padre, mwaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa amana na urithi ambao ameliachia Kanisa na jamii katika ujumla wake; Urithi unaowajibisha. Ni muda muafaka wa kumfanya afahamike na hatimaye, kusikilizwa na wengi.