Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewaandikia vijana wa kizazi kipya waraka kama utanguzi wa Toleo Jipya la Katekisimu ya Vijana, maarufu kama “Youcat.” Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewaandikia vijana wa kizazi kipya waraka kama utanguzi wa Toleo Jipya la Katekisimu ya Vijana, maarufu kama “Youcat.”   (Vatican Media)

Katekisimu ya Kanisa Katoliki Kwa Vijana: Youcat 2024 Ni Ufunguo wa Furaha ya Kweli

Mkazo ni: Upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, ufunuo wa mafumbo makuu uliofanywa na Kristo Yesu kwa njia ya maisha, mateso, kifo na ufufuko. Ni wajibu wa Kanisa kuendelea kumshuhudia Kristo Yesu na kuhakikisha kwamba, waamini wanajibidiisha ili aweze kufahamika na kupendwa na watu wengi. Katekisimu ya Vijana wa Kizazi Kipya inachota amana na utajiri wake kutoka katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ili kuwasaidia vijana kuweza kumfahamu Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi chombo cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala
Katekisimu ya Kanisa Katoliki: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala

Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala
Katekisimu ya Kanisa Katoliki: Imani, Sakramenti, Maadili na Sala

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewaandikia vijana wa kizazi kipya waraka kama utanguzi wa Toleo Jipya la Katekisimu ya Vijana, maarufu kama “Youcat.” Katika waraka huu, Baba Mtakatifu anakazia sana upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, ufunuo wa mafumbo makuu uliofanywa na Kristo Yesu kwa njia ya maisha, mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Ni wajibu wa Mama Kanisa kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na kuhakikisha kwamba, waamini wanajibidiisha ili aweze kufahamika na kupendwa na watu wengi. Katekisimu ya Vijana wa Kizazi Kipya inachota amana na utajiri wake kutoka katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ili kuwasaidia vijana kuweza kumfahamu, kumpenda na hatimaye kumtumikia Kristo Yesu katika maisha yao.

Katekisimu ni chombo makini cha uinjilishaji wa kina
Katekisimu ni chombo makini cha uinjilishaji wa kina

Katekisimu ya Kanisa Katoliki, ijulikane na ipokelewe, ili umoja katika imani ambao ni chemchemi na msingi wake ni katika umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, uimarishwe na kuenezwa hadi miisho ya dunia. Katekesimu ya Kanisa Katoliki ni muhtasari wa Habari Njema ya Wokovu na amana ya wokovu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwapatia vijana wa kizazi kipya neno la siri, “Password” ili kufungua nyoyo zao na kuweza kuingia katika fumbo la imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chemchemi ya maisha na furaha ya kweli ni kujisomea Injili. Baba Mtakatifu anawahimiza vijana wa kizazi kipya kujenga utamaduni wa kusali, kusoma, kutafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yao na kwa sasa wafanye bidii ya kusoma Katekesimu Ya Kanisa Katoliki, ili waweze kumfahamu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Youcat 2024
30 January 2024, 11:03