Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024. Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024.   (Vatican Media)

Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu: Nguvu ya Neno la Mungu: Wito, Utume na Sala

Papa Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Nguvu ya Neno la Mungu inayoamsha wito na utume; Sala inayosimikwa katika Neno la Mungu, Neno la Mungu linalowasukuma Mitume kuacha yote na kumfuasa Kristo Yesu na nafasi ya Neno la Mungu katika maisha ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume wa “Appeluit llis” yaani: “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45) alitangaza rasmi kwamba, Dominika ya Tatu ya Mwaka wa Liturujia ya Kanisa itakuwa ni kwa ajili ya Neno la Mungu. Lengo ni kuliwezesha Kanisa zima kupata utambuzi mpya wa jinsi Kristo Mfufuka anavyowafungulia waamini wake hazina ya Neno lake na hivyo kuwawezesha kutangaza utajiri huu mkubwa kwa walimwengu. Anasema, utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika uhusiano wa dhati kati ya Bwana Yesu Mfufuka, jumuiya ya waamini na Maandiko Matakatifu. Bila ya Bwana Yesu anayetuangaza, haiwezekani kabisa tuelewe kwa kina Maandiko Matakatifu; lakini pia ni kweli kinyume chake: yaani, bila ya Maandiko Matakatifu haiwezekani kuelewa matukio ya utume wake Yesu na wa Kanisa lake ulimwenguni. Ndiyo maana Mtakatifu Hieronimo aliweza kuandika: “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo” (In Is., Utangulizi: PL 24,17). Dominika ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika maisha halisi. Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27.

Papa anakazia Ibada ya Neno la Mungu katika maisha na utume
Papa anakazia Ibada ya Neno la Mungu katika maisha na utume

Na Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu tarehe 21 Januari 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Nguvu ya Neno la Mungu inayoamsha wito na utume; Sala inayosimikwa katika Neno la Mungu, Neno la Mungu linalowasukuma Mitume kuacha yote na kumfuasa Kristo Yesu na nafasi ya Neno la Mungu katika maisha ya kila mwamini! Neno la Mungu lina nguvu sana, kiasi kwamba, wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu walipolisikia waliacha yote na kumfuasa, kama ilivyokuwa hata kwa Nabii Yona aliyeitwa na kutumwa kwenda kutangaza toba na wongofu wa ndani na huo ukawa ni mwanzo mpya wa maisha na utume wa watu wa Mungu. Kwa wafuasi wale wa kwanza wa Kristo Yesu, walipolisikia Neno la Mungu, likaamsha ndani mwao wito na utume, kiasi cha kuacha yote na hivyo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kwa bahati mbaya, Neno la Mungu halina nafasi kubwa katika Ulimwengu mamboleo. Lakini kwa Mama Kanisa, anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu. Neno la Mungu lina nguvu, ni kisima cha majadiliano, linagusa sakafu ya moyo wa mwanadamu, kiasi cha kuupyaisha kwa amani ya Kristo Yesu na hivyo kuwa ni faraja kwa wengine. Nguvu ya Neno la Mungu inajionesha kwa akina Mtakatifu Anthony, Abate, Mtakatifu Agostino Askofu na Mwalimu wa Kanisa, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyeitwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, mara nyingi waamini wanayo fursa ya kusikia Neno la Mungu, lakini hawalisikilizi, Wanalisikiliza, lakini hawalihifadhi katika sakafu ya nyoyo zao na wala kuliachia Neno la Mungu liwaletee mageuzi na upyaisho wa maisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza waamini kusoma na kulitafakari na kulizingatia Neno la Mungu nyoyoni mwao, wajifunze katika Liturujia Takatifu na kwamba, kusoma Maandiko Matakatifu lazima kuwe ni katika mazingira ya Sala ili Mungu na binadamu waweze kuongea pamoja, kwa sababu wanaongea na Mungu wanaposali, wanamsikiliza wanaposoma Maandiko Matakatifu sanjari na kumwabudu. Rej. Dei verbum, 25. Wale wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu, walipolisikia Neno la Mungu wakaacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kulipatia Neno la Mungu tafsiri mpya katika maisha, kuliachia nafasi liweze kuganga na kuponya kumbukumbu za zamani na hivyo kubakisha kumbukumbu hai ya matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Neno la Mungu linakita mizizi yake katika wema wa Mungu na kuwakumbusha waamini kwamba, wao kwa hakika ni watoto wanaopendwa na kukombolewa na Mungu na hii inakuwa ni fursa ya kushinda hofu, woga na upweke hasi na hivyo kupyaisha imani na kuendelea kutakasa mapungufu ya binadamu ili kuwarejesha tena katika asili yao inayobubujika kutoka katika Habari Njema ya Wokovu! Waliacha yote na kumfuasa Kristo Yesu na kuufanya ukweli katika upendo uzamishe mizizi yake katika maisha yao; kwa kutakasa unafiki wao, ili kuwakirimia matumaini kama mvua au upanga wenye makali kuwili, au kama mbegu imeayo na kuzaa matunda ajaa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Neno la Mungu lina nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwani ni egemeo na nguvu kwa Kanisa na pia uthabiti wa imani, chakula cha roho na chemchemi safi na ya daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa. Rej. Dei verbum, 21.

Baadhi ya waamini wamepewa daraja ya usomaji
Baadhi ya waamini wamepewa daraja ya usomaji

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu yawasaidie waamini kurejea tena kwa furaha kwenye kisima cha imani kinachopata chimbuko lake kwa kumsikiliza Neno wa Mungu aliye hai, Kristo Yesu. Kwa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu, uwe ni msaada kwa waamini kugundua tena umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa, vinginevyo waamini wataishia tu kwenye tabia ya kutaka “kujimwambafai” bada ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu pamoja na Neno lake la Uzima. Huu ni mwaliko kwa waamini kurejea tena katika chemchemi ya maji hai, ili kuwapatia walimwengu Neno linalookoa badala ya maneno ya vita na uchochezi kutoka katika mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake katika maadhimisho ya Dominika ya Tano ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 kwa kuwaulizia waamini nafasi ya Neno la Mungu katika maisha na utume wao! Je, wamejijengea utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vyao vya maisha? Je, wamejenga utamaduni wa kutembea na Biblia Takatifu? Je, wamewahi kusoma walau Injili yote? Habari Njema ya Wokovu ni chemchemi ya maisha, lakini inasikitisha kuona kwamba, kuna umati wa waamini ambao hawajahi kusoma walau Injili yote, yaani tangu mwanzo hadi mwisho. Huu ni mwaliko wa kutoa nafasi kwa Neno la Mungu katika maisha!

Dominika ya Neno la Mungu
21 January 2024, 15:02