Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na zaidi ya Mapadre, Watawa na Mashemasi 800 wanaotekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na zaidi ya Mapadre, Watawa na Mashemasi 800 wanaotekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Roma.  (Vatican Media)

Mahojiano Kati ya Papa Francisko na Mapadre Wanaoishi na Kufanya Utume Wao Roma

Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake amekazia kwamba, Jimbo kuu la Roma ni “eneo la kimisionari” na hivyo ametoa wito wa Jumuiya ya waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda. Baada ya kusimama kwa muda kutembelea Parokia za Jimbo kuu la Roma kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sasa Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuanza tena kutembelea Parokia ili kujionea hali halisi ya Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na zaidi ya Mapadre, Watawa na Mashemasi 800 wanaotekeleza dhamana na utume wao Jimbo kuu la Roma na kujibu maswali thelathini yaliyoulizwa katika ukweli na uwazi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi. Alipowasili kwenye Kanisa kuu la Yohane wa Laterani, Baba Mtakatifu alikaribishwa na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma. Baada ya Masifu ya Adhuhuri yalifuatiwa na salam kutoka kwa Kardinali Angelo De Donatis na kisha Baba Mtakatifu akaanza majadiliano ya kina na Mapadre. Ikumbukwe kwamba, huu ni mkutano ambao umeendeshwa kwa faragha, kama desturi ya Baba Mtakatifu na Mapadre wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake amekazia kwamba, Jimbo kuu la Roma ni “eneo la kimisionari” na hivyo ametoa wito wa Jumuiya ya waamini kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baada ya kusimama kwa muda kutembelea Parokia za Jimbo kuu la Roma kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sasa Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuanza tena kutembelea Parokia ili kujionea hali halisi ya Jimbo kuu la Roma. Itakumbukwa kwamba, mazungumzo haya ya faragha yametanguliwa pia na mazungumzo yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Roma, mara tatu na kwamba, mazungumzo haya yamekuwa yakifanyika kwa faragha, ili kumpatia fursa Baba Mtakatifu kufahamu hali hali ya wa maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Roma. Lengo ni kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu.

Papa Francisko akizungumza na Mapadre, watawa na mashemasi wa Roma
Papa Francisko akizungumza na Mapadre, watawa na mashemasi wa Roma

Kardinali Fridolin Ambongo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, katika barua yake ya tarehe 20 Desemba 2023 aliyaomba Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika kujadili tamko hili la “Fiducia Supplicans”, ili hatimaye, Kanisa Barani Afrika liweze kutoa msimamo na mwongozo kwa waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika, kwa kutambua dhamana na umuhimu wa Mabaraza ya Maaskofu katika kuambata mchakato wa Sinodi sanjari na kukuza urika wa Maaskofu. Tamko la Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM ni matunda ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi kwa hiyo ni kwa ajili ya Kanisa zima la Bara la Afrika. Ni katika muktadha huu, SECAM, tarehe 11 Januari 2024 imetoa tamko linalosema, hakuna baraka kwa wapenzi wa jinsia moja kwa Makanisa Barani Afrika. Tamko hili limeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Victor Manuel Fernàndez, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hili ni tamko linajadili mafundisho ya Kanisa kuhusu Ndoa na Tendo la Ndoa; Mwongozo wa Kichungaji kwa familia ya Mungu Barani Afrika; Msimamo wa Kanisa Barani Afrika mintarafu mapenzi ya watu wa jinsia moja na hatimaye, SECAM inatoa hitimisho ya tamko lake.

SECAM yakataa kutoa baraka kwa mashoga na wasagaji
SECAM yakataa kutoa baraka kwa mashoga na wasagaji

Maaskofu Barani Afrika wanatambua dhamana na nafasi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kukuza umoja wa imani, ushirika na urika kati yao, daima wakiwa waaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili. Wanatambua mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia ambayo kamwe hayawezi kubadilika na kwamba, Tamko la “Fiducia supplicans” linatambua Mapokeo ya Kanisa Katoliki yanayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na Mamlaka Fundishi ya Kanisa “Magisterium of the Church” kwamba: Kiini cha ndoa ya Kikristo ni maagano baina ya mume na mke au ukubaliano wao wa hiari usiotanguka. Kumbe mahusiano ya watu wa jinsia moja ni jambo lisilokubalika na kwamba, Kanisa Barani Afrika haliwezi kutoa baraka. Kanisa Barani Afrika linaendelea kujitambulisha kuwa ni familia ya Mungu inayowajibika na kwamba, litaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Barani Afrika na kwamba, Mapadre wanahimizwa kutoa huduma kwa watu wenye “ndoa tenge” na kwamba, mashoga na wasagaji waheshimiwe na utu wao uthaminiwe lakini wakumbushwe kwamba mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na kwa mantiki hii hawawezi kupata baraka ya Kanisa kwani mahusiano haya ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. SECAM inasema Mapokeo yametamka daima kwamba matendo ya kujamiana ya jinsia moja ni maovu kwa yenyewe. Ni matendo dhidi ya sheria ya maumbile. Yanatenga paji la uhai na tendo la kijinsia. Hayatokani na kutimilizana kwa kweli kihisia na kijinsia. Kwa namna yoyote ile hayawezi kuidhinishwa. Rej. KKK 2357.

Zaidi ya Mapadre, watawa na masheasi 800 wamehudhuria
Zaidi ya Mapadre, watawa na masheasi 800 wamehudhuria

Mapenzi ya jinsia moja ni kashfa kadiri ya Maandiko Matakatifu. Katika muktadha wa Kanisa Barani Afrika, mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na ni vigumu sana watu wa namna hii kukubalika na hatimaye kupokelewa na jamii kwa sababu ni matendo yanayokwenda kinyume cha tamaduni na kwamba, huu ni uovu! SECAM inahitimisha tamko lake kwa kusema, kadiri ya Maandiko Matakatifu, Mamlaka Fundishi ya Kanisa, tamaduni, kanuni maadili na utu wema, Kanisa Barani Afrika halitatoa baraka kwa watu wa mapenzi ya jinsia moja, kwani kufanya hivi ni kuibua kashfa na kwamba, kuna umuhimu kwa watu wenye shauku ya jinsia moja kutubu na kumwongokea Mungu ili waonje huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, tayari kuwa ni chumvi na nuru ya dunia. Rej. Mt 5:13-14. Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali kuhusu msimamo wa Kanisa Barani Afrika kuhusu Baraka kwa wapenzi wa jinsia moja, amekaza kusema, baraka inatolewa kwa watu na wala si katika dhambi zao na kwamba, mafundisho ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa yako pale pale. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni wa toba, msamaha na upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Kuhusu mahubiri Baba Mtakatifu Francisko anasema,  hiki ni kipimo cha kutambua ni kwa kiasi gani mchungaji yupo karibu na waamini wake na ni kwa kiwango gani anaweza kuwasiliana nao na kwamba, mahubiri yanaweza kuwa ni hisia ya Roho ya nguvu na furaha, faraja na chanzo cha daima cha kupyaisha na kukuza. Mahubiri yasaidie kuamsha imani ya Kanisa, ili kuwafikia watu wengi zaidi mintarafu maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Mahubiri yanapofanyika katika muktadha wa maadhimisho ya Kiliturujia, yanakuwa ni sehemu ya matoleo ya Baba wa milele na neema ambayo Kristo Yesu humimina wakati wa maadhimisho hayo. Muktadha huu unadai kwamba, mahubiri yaliongoze kusanyiko, pamoja na mhubiri, kwenye ushirika na Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo huleta mabadiliko katika maisha. Rej. Evangelii gaudium 135-138. Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena amekazia umuhimu wa mahubiri kuwa ni mafupi kati ya dakika saba hadi nane, ili kuwapata waamini fursa ya kuipokea roho ya Neno la Mungu.

Mapadre wa Roma

 

15 January 2024, 14:29