Tafuta

Baba Mtakatifu Ijumaa tarehe 26 Januari 2024 amekutana na Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki Baba Mtakatifu Ijumaa tarehe 26 Januari 2024 amekutana na Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki   (Vatican Media)

Majadiliano ya Kiekumene Yasimikwe Katika: Upendo, Ukweli na Maisha

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 26 Januari 2024 amekutana na Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki amekazia majadiliano ya uekumene wa upendo na ukweli, tume hii ilianzishwa mwaka 2004 na kila mwaka inakutana; maana ya Sakramenti katika maisha ya Kanisa yote haya yanapania kukuza na kudumisha majadiliano ya upendo, ukweli na maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki inaendelea kutekeleza dhamana na utume wake kwa kutembea katika umoja, udugu na amani, kwa kuendelea kuungwa mkono na watakatifu pamoja na mashuhuda wa imani, wanaosali bila kuchoka kwa ajili ya umoja wa Kanisa, mapambano dhidi ya baa la njaa pamoja na kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Tume hii ya kimataifa kwa mwaka 2024 inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yananogeshwa na uwepo pamoja na ushiriki wa ujumbe wa Mapadre na Wamonaki vijana wanaoboresha matumaini na sala inayoongoza hija hii ya maisha ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 26 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume hii mchanganyiko na hivyo kuwaomba wamfikishie salam na matashi mema kwa viongozi wakuu wa Makanisa, ambao mwaka 2023, baadhi yao walimtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu amekazia majadiliano ya uekumene wa upendo na ukweli, tume hii ilianzishwa kunako mwaka 2004 na kila mwaka inakutana; maana ya Sakramenti katika maisha na utume wa Kanisa yote haya yanapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha majadiliano ya upendo, ukweli na maisha.

Majadiliano ya kiekumene: upendo, haki na maisha
Majadiliano ya kiekumene: upendo, haki na maisha

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hija hizi mjini Vatican zinapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha majadiliano ya upendo na ukweli; mambo msingi yanayoendelezwa na Tume hii tangu kuanzishwa kwake, kama inavyobainishwa katika Hati ya “Huduma ya Ushirika Katika Maisha ya Kanisa la Mwanzo na Matokeo Yake katika Utafutaji wao wa Ushirika Nyakati hizi.” Tume inatambua Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi na ujenzi wa udugu wa kibinadamu mambo msingi katika ujenzi wa majadiliano ya kiekumene. Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki ilianzishwa mwezi Januari 2004 huko mjini Cairo, nchini Misiri na tangu wakati huo, Tume hii imekuwa ikikutana walau mara moja kila mwaka. Tume hii inaundwa na Makanisa ya Kikoptiki kutoka Siria, Armenia, Malankaresi, Ethiopia, Eritrea na Kanisa la Kilatin, kielelezo cha umoja katika tofauti unaojionesha katika maisha ya kitamaduni, kijamii, kibinadamu na kwamba, Kanisa linabeba ndani mwake taalimungu tofauti zinazobubujika kutoka katika imani inayoshuhuhudiwa katika nidhamu mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa; Liturujia pamoja na amana na utajiri wa maisha ya kiroho kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Majadiliano ya kiekumene: Umoja na tofauti msingi.
Majadiliano ya kiekumene: Umoja na tofauti msingi.

Tume Mchanganyiko ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki tangu kuanzishwa kwake, imeendelea kujizatiti katika Sakramenti katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre vijana na wamonaki wanapaswa kufundwa vyema kuhusu tema hii, kwani hiki ni kielelezo cha chanzo cha karama za Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko wa kujizatiti katika kukuza na kudumisha majadiliano ya upendo, ukweli na maisha; mambo msingi ambayo yameacha chapa ya kudumu katika kipindi chote cha miaka ishirini tangu kuanzishwa kwa Tume hii. Kumbe, hiki ni kipindi cha kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mchango mkubwa wa mawazo ya kitaalimungu na maisha ya sala, ili hatimaye kupyaisha tena utambuzi wa umoja mkamilifu wa Kanisa ni jambo linalowezekana na kwamba, ni jambo pia la dharura “ili ulimwengu upate kusadiki.” Yn 17:21. Kwa sasa Tume hii inajadili pamoja na mambo mengine, Mafundisho kuhusu Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaaminisha kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, chini ya ulinzi na tunza yake ya Kimama.

Tume ya Kiekumene

 

26 January 2024, 14:20