Mama Kanisa Anawathamini Wanamichezo: Udugu, Ujirani na Ukaribu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania pamoja na mambo mengine: Kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.
Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 13 Januari 2024 alikutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Wanamichezo wa Vatican. Katika hotuba yake amekazia kuhusu: Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu”; ushuhuda wa imani katika Kristo Yesu na Kanisa lake; Maisha ya sala na huduma kwa maskini; Michezo ni fursa ya kushirikisha talanta, karama sanjari na ujenzi wa jamii. Wanamichezo wakuze na kudumisha ujirani, huruma na udugu wa kibinadamu! Sehemu kubwa ya Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inajikita katika sheria, kanuni na taratibu na kwamba, kila Mkristo kwa Ubatizo wake ni Mtume mmisionari anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema.
Ni katika muktadha huu, hata waamini walei wenye sifa zinazohitajika wanaweza kuteuliwa kuchukua nafasi za uongozi kwenye Sekretarieti kuu kadiri ya Mamlaka aliyokabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja kwa Mama Kanisa kukuza na kudumisha majadiliano na wanamichezo, kwani Kanisa linawatambua na kuwathamini wanamichezo, daima wako katika huduma ya kutafuta na kuambata, kile kilicho chema na kizuri. Anawashukuru wana michezo wa Vatican kwa ushuhuda wao bila kuwasahau viongozi wa michezo wa Vatican, Kitaifa na Kimataifa, mashuhuda wa majadiliano na ushirikiano na Vatican. Imekwisha gota miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wanamichezo wa Vatican, ambao wamekuwa mstari wa mbele kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu; ushiriki na ushuhuda wa imani ya Kanisa Katoliki, tayari kuvunjilia mbali kuta za utengano ili kujenga misingi ya amani sanjari na kudumisha michezo katika ngazi mbalimbali. Baba Mtakatifu anawapongeza wanamichezo wa Vatican kwa ushiriki wao katika michezo katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa, kielelezo cha jumuiya ya wanamichezo, wanaojikita katika huduma ya Vatican, huku wakiwa na uzoefu wa mchakato wa uinjilishaji. Chama hiki kinatoa fursa pia ya nyakati za sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huu ni ushirika katika utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, Mwenyezi Mungu yuko karibu sana na mwanadamu, ndiyo maana anapenda kumwonesha huruma, upendo na ujirani mwema. Michezo ni muda muafaka wa kudhihirisha vipaji na karama za binadamu, tayari kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kuweza kufikia lengo la jumla la michezo, kwa kutambua kwamba, hata katika tofauti zao msingi, lakini wote wanaunda familia moja ya binadamu inayoundwa na watu: kimwili, kiuchumi na kijamii.
Michezo ni chombo cha kinachowajumuisha watu na hivyo kubomolea mbali kuta zinazowatenganisha watu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu kumwelimisha binadamu katika utamaduni mzima kwamba, pamoja na hayo, huweza pia kutoa mchango wake katika kustawisha mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, wa mataifa na makabila mbalimbali. Wakristo wanahamasishwa kushiriki katika michezo inayokolezwa na roho ya kiutu na ya Kikristo. Rej. Gaudium et spes 61. Michezo inaendeshwa na kusimamiwa na sheria, kanuni na taratibu. Wanamichezo wajifunze ili kushinda kwa unyenyekevu na kukubali kushindwa kwa staha, huku wanamichezo wakijitahidi kujenga jamii inayosimikwa katika haki na udugu. Michezo ni shule ya ukweli, ujasiri, uamuzi, udugu wa kibinadamu, fadhila za kibinadamu zinazoimarishwa na fadhila za Kimungu na hivyo kuwa ni msingi imara kama alivyowahi kusema Papa Pio wa XII tarehe 25 Mei 1945. Michezo inaonesha kwamba, watu wanaweza kukabiliana kwa uvumilivu, madhaifu pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu na hatimaye, kufikia malengo. Huu ni ujumbe wa matumaini ambao ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya, katika mchakato wa ujenzi jumuiya inayosimikwa katika kanuni na maadili mema ya Kikristo yaani: Uaminifu, sadaka, moyo wa timu, kujisadaka bila ya kujibakiza, ushirikishwaji, kujinyima, ili hatimaye kuleta ukombozi. Amewaambia wanamichezo kukumbuka michezo inaanza kukuzwa tangu mtu akiwa mdogo, changamoto na mwaliko kwa wana michezo kujitoa kikamilifu.