Tafuta

Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa.   (AFP or licensors)

Mbiu ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana 31 Machi 2024 & Sala Waamini

Katika Sherehe ya Tokeo la Bwana Mama Kanisa anatangaza Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa: Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 31 Machi 2024.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Kila Dominika, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Sikukuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 14 Mwezi Februari 2024 kwa waamini kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 12 Mei 2024 na Pentekoste, Sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei itaadhimishwa hapo tarehe 19 Mei 2024.

Pasaka kwa Mwaka 2024 itaadhimishwa tarehe 31 Machi 2024
Pasaka kwa Mwaka 2024 itaadhimishwa tarehe 31 Machi 2024

Jumapili ya kwanza ya Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo Yesu itaadhimishwa hapo tarehe Mosi Desemba 2024. Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Sherehe na Sikukuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Sikukuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo Yesu aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake, ni Alfa na Omega. Amina.

Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 19 Mei 2024
Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 19 Mei 2024

Wakati huo huo, Maria Salome Melchior Kaigarula kutoka Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Tanzania ndiye aliyebahatika kusoma Sala ya Waamini kwa lugha ya Kiswahili kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Epifania ya Bwana, Jumamosi tarehe 6 Januari 2024, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 6 Januari ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake. Radio Vatican inamtakia kheri na baraka tele katika maisha katika kipindi cha mwaka 2024. Amewawakilisha wazungumzaji wa Lugha ya Kiswahili kwa ufasaha kabisa.

Mbiu ya Pasaka 2024
06 January 2024, 14:07