Miaka 60 ya Kamati ya Ushirikiano wa Kitamaduni: Huduma ya Umoja wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kamati ya Ushirikiano wa Kitamaduni kati ya Kanisa Katoliki, Makanisa ya Kiorthodox pamoja na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki ilianzishwa kunako mwaka 1964, kama sehemu ya mbinu mkakati unaolenga kurejesha uhusiano wa kidugu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, kwa kukuza miradi ya kitamaduni yenye maslahi kwa pande zote. Hasa, Kamati inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kiorthodox na wale wa Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki wanaopania kukamilisha masomo yao ya kitaalimungu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki na baada ya masomo, wanafunzi hawa wanarejea tena katika nchi zao ili kutoa huduma. Kwa njia hii, wanashiriki kikamilifu katika malezi na majiundo ya watu wa Mungu, ili kuwawezesha kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Kamati hukutana na Bodi yake ya Usimamizi mara moja kwa mwaka. Kamati hii kwa mwaka 2024 inaadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, tukio ambalo limepambwa kwa wanakamati kukutana na kuzuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi na wanafunzi wanaofaidika na ufadhili huu pamoja na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazotoa hifadhi na masomo kwa wanafunzi hawa; amekazia umoja wa wafuasi wa Kristo Yesu katika upendo kutoka kwa Roho Mtakatifu pamoja na uaminifu kwa Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Hii ni nafasi ya kuweza kufahamu safari ya malezi na majiundo: kiroho na kiliturujia miongoni mwa wanafaunzi hawa vijana, sanjari na kushirikishana mang’amuzi ya maisha ya kijumuiya katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, huku wakifundwa na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu.
Hii ni fursa kwa wanafunzi wote kuondokana na maamuzi mbele, pamoja na kuta za utengano, ili hatimaye, kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu katika majadiliano na urafiki wa kijamii. Hata miongoni mwa Mitume wa Kristo Yesu, kulikuwa na tofauti kubwa; kuna wale waliokuwa ni wanafunzi wa Yohane Mbatizaji, wavuvi pamoja na watoza ushuru, lakini wote hawa wakaunganishwa na kufungamanishwa na Kristo Yesu, huku wakifuata nyayo zake na wao wenyewe wakiendelea kushikamana katika umoja na upendo kutoka kwa Roho Mtakatifu. Hii ni changamoto kwa wafuasi wa Kristo Yesu kufuata nyayo zake. Kwa wanafunzi kutoka katika Makanisa ya Kiorthodox ni fursa ya pekee kupata nafasi ya kusoma mjini Roma, ili kwa pamoja kuweza kumjifunza Kristo Yesu ni nani kwao? Kwa vile wanao msingi, ambaye ni Kristo Yesu mwenyewe, kumbe, wanaweza kushirikiana kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, tayari kurekebisha historia ya Makanisa haya, ili kujikita katika uaminifu kwa Kristo Yesu, ambaye alilipenda Kanisa kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya yake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wanafunzi hawa katika masomo na majiundo yao ya maisha ya kiroho, wataweza kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, heshima na utukufu kutokana na ukarimu, heshima ya kidugu, kusikiliza na kuonjeshana upendo kwa ajili ya ujenzi wa amani. Katika maisha na masomo yao waendelee kujikita katika malezi na majoundo ya maisha ya kiroho na kichungaji; mambo msingi katika malezi na majiundo.