Wanachama wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta”, Jumamosi tarehe 27 Januari 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wanachama wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta”, Jumamosi tarehe 27 Januari 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Msingi wa Diplomasia ya Vatican na Kanisa Kwa Ujumla: Utu wa Binadamu

Baba Mtakatifu Francisko amekazia: Umuhimu wa diplomasia ya Vatican inayotoa kipaumble cha kwanza kwa maskini; nafasi ya Bikira Maria, Ushiriki wao katika Jumuiya ya Kimataifa kama chombo cha shughuli za Kitume na Kidini pamoja na Diplomasia ya Kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo kuu la Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Diplomasia ya utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu!

Chama cha Kitume cha Kijeshi cha Malta
Chama cha Kitume cha Kijeshi cha Malta

Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Hii ni amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli. Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kukiri na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbalimbali za dunia, kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu.

Hii ni diplomasia inayojikita katika utu, heshima na haki msingi
Hii ni diplomasia inayojikita katika utu, heshima na haki msingi

Wanachama wa Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta”, Jumamosi tarehe 27 Januari 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake amekazia umuhimu wa diplomasia ya Vatican inayotoa kipaumble cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; nafasi ya Bikira Maria, Ushiriki wao katika Jumuiya ya Kimataifa kama chombo cha shughuli za Kitume na Kidini pamoja na Diplomasia ya Kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo kuu la Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa, kwa njia ya huduma makini, kama Kristo Yesu alivyotoa kwa maskini na wale wote waliokuwa wanatengwa na jamii. Kwa hakika wanafuata na kuiga mfano wa Maria wa Bethsaida aliyempaka Kristo Yesu marhamu ya nardo safi yenye thamani kubwa. Rej. Yn 12:3-8. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, hata wao wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa njia ya huduma kwa maskini, wagonjwa na wahitaji zaidi, kielelezo cha huruma ya Mungu kwa wanyonge na maskini.

Lengo kuu ni kumtukuza Mungu na Mwanadamu kutakatifuzwa
Lengo kuu ni kumtukuza Mungu na Mwanadamu kutakatifuzwa

Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” kinatoa huduma katika nchi 113 na kwenye Mashirika ya Kimataifa kina wawakilishi 37, daima kwa kujikita katika huduma ya maisha ya kiroho, kama ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Hiki ni Chama kinachojihusisha na huduma ya upendo, Ulinzi wa imani pamoja na utii “Tuitio fidei, obsequium” kama alivyobainisha Papa Pio XII na kwamba, Chama hiki kiko chini ya usimamizi wa Vatican na kwamba, kinatekeleza utume wake kama chombo cha shughuli za Kitume na Kidini chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa, hata wakati mwingine, Papa ameingilia mara kadha wa kadha hasa katika nyakati za shida na changamoto pevu za Chama hiki cha kitume. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia yenye mwelekeo wa kimisionari na Kikanisa, ushuhuda wenye thamani kubwa unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  

Diplomasia ya Vatican
29 January 2024, 13:47