Mtakatifu Francisko wa Sale, Askofu na Mwalimu wa Maisha ya Kiroho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mama Kanisa tarehe 28 Desemba 2022 alizindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Francisko wa Sales, Askofu, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari alipofariki dunia. Yeye alizaliwa tarehe 21 Agosti 1567, huko Sales; Thorens-Glières, Ufaransa, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 18 Desemba 1593, na Desemba 1602 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geneva, Uswis na hatimaye kufariki dunia tarehe 28 Desemba 1622 huko Lyon. Papa Alexander VII akamtangaza kuwa Mwenyeheri 8 Januari 1662 na hatimaye Mtakatifu tarehe 19 Aprili 1665. Papa Leo wa XIII kunako mwaka 1887 akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Januari 2024 amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Sale, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Kwa hakika ni Mwalimu wa maisha ya kiroho. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa kuimarika na misaada ya wokovu mingi namna hii na ya ajabu, waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Bwana, kila mmoja kwa njia yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Baba mwenyewe alivyo Mtakatifu. Rej. Lumen gentium 11. Utakatifu wa maisha ni jambo linalowezekana. Kila mwamini ajitahidi kufanya mang’amuzi ya maisha yake, ili kugundua ile karama ya Mungu iliyofichwa katika maisha yake, ili kupata ile furaha ya kweli katika maisha. Upendo kwa Mungu na jirani kiwe ni kiini cha furaha ya kweli katika kazi na maisha. Huu ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi, ili kusikiliza sauti ya Mungu, tayari kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani, kama anavyosimulia Mtakatifu Paulo katika utenzi wake wa upendo. Furaha ya kweli inafumbatwa katika utii, ukweli, haki, wajibu na sadaka binafsi. Upendo wa kweli ni dira na mwongozo wa maisha kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kilele cha upendo wa Kristo kimetundikwa Msalabani na kwamba, Mlima wa Kalvari ni mahali ambapo wapendwa wanakutana. Yote yanapita, isipokuwa upendo unadumu daima. Jubilei ya Miaka 400 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Sale, iwe ni fursa ya kukuza heshima kwa Mtakatifu huyu, pamoja na kumwomba, ili kwa njia ya Roho Mtakatifu, karama na mapaji ya Roho Mtakatifu yaweze kuwashukia waja wake katika safari hii ya utakatifu pamoja na waamini. Mafundisho yake ya maisha ya kiroho yawasaidie waamini kushinda mizizi ya dhambi pamoja na vishawishi, tayari kuambata mchakato wa utakatifu wa maisha.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amechapisha Waraka wa Kitume “Totum Amoris Est” yaani “Yote ni Kuhusu Upendo”: Miaka 400 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Francisko wa Sales.” Katika Waraka huu wa Kitume, “Totum Amoris Est” yaani “Yote ni Kuhusu Upendo”: Miaka 400 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Francisko wa Sales.” Baba Mtakatifu anapembua utume wa Mtakatifu Francisko wa Sales uliosimikwa katika ushuhuda wa upendo na kwamba, kigezo kikuu kilikuwa ni upendo. Malezi ya awali ilikuwa ni safari ya kujitambua binafsi mbele ya Mwenyezi Mungu; Kuvumbua Ulimwengu mpya na kwamba, upendo hufanya yote kwa ajili ya watoto wake; mahitaji ya mabadiliko ya nguvu katika kuhubiri, kiasi cha kuhitaji upepo na mbawa. Baba Mtakatifu afafanua kuhusu Ibada ya kweli inayopata chimbuko lake katika upendo kwa Mungu, chemchemi ya utakatifu wote na kilele cha furaha ya maisha. Utume na maisha ya Mtakatifu Francisko wa Sales yalisimikwa katika ushuhuda wa upendo uliomwilishwa katika huduma ya majadiliano ya kina na watu mbalimbali; kwa kuungamisha, kutoa mahubiri na mihadhara pamoja na kuwasiliana na jirani zake, ili kuwashirikisha uwepo wa Mungu kutoka katika sakafu ya moyo wake na kwamba, mahali muafaka pa kukutana na Mwenyezi Mungu ni katika nyoyo za waamini wake; Mwenyezi Mungu ambaye daima yuko katika kila hali ya maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao. Shule ya Fumbo la Umwilisho, iwasaidie waamini kutoa tafsiri ya kina, kwa kumwamini na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika maisha na mang’amuzi yake alitambua kwamba, upendo ndicho kigezo muhimu kwa mwanadamu kuweza kufikia utimilifu wa maisha, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake na kwamba, upendo ndicho kipimo kinachoongeza thamani kwenye kazi mbalimbali zinazotendwa na mwamini. Watu wanapaswa kufahamu na kutafakari ili matendo yao, yanaporutubishwa na upendo, yaweze kumpendeza na hatimaye kukutana na Mungu.
Ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II anamwita Mtakatifu Francisko wa Sales, “Mwalimu wa Upendo wa Kimungu” kwa sababu amejitahidi kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo wa Mungu uliomwilishwa katika utume na shughuli mbalimbali za kichungaji. Malezi na majiundo ya awali kwa Mtakatifu Francisko wa Sales yalimwezesha kupata mang’amuzi mbalimbali ya maisha na hatimaye, kufahamu uzoefu wake pamoja na mang’amuzi ya jirani zake. Ni mtakatifu aliyeonja makali na athari za vita, kiasi cha kujikita katika haki na ukweli, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ili kupata amani ya ndani tayari kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi pamoja na jirani zake, kiasi cha kuwezeshswa kuwa na mang’amuzi mbele ya Mungu: Kwanza kabisa katika maisha ya sala, na pili ni katika maisha ya Kanisa, kwa kufikiri na kutenda kwa ajili pamoja na Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wanataalimungu kutekeleza dhamana na wajibu wao huku wakichota nguvu, ari na mwamko kutoka katika jamii inayowazunguka bila kusahau umuhimu wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Mambo haya mawili yalimwezesha Mtakatifu Francisko wa Sales kuwa na mang’amuzi mapana. Katika safari ya maisha yake, anasema, Baba Mtakatifu, baada ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Desemba 1593, alikumbana na changamoto pevu: za wazushi, vita na magumu ya maisha, kiasi cha kugundua kwamba, ndani mwake alikuwa amekirimiwa kipaji cha kuwa mpatanishi, mtu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, na mwana mawasiliano na mhubiri mahiri sana aliyejitaabisha kuwaandaa katika medani mbalimbali za maisha: kiroho na kimwili kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; mabadiliko makubwa katika maisha na utume wake. Machapisho mbalimbali yaliwawezesha kupata mavuno mengi, hasa kutokana na mbinu yake: kwa kutambua magonjwa ya kiroho na kuwawezesha wasikilizaji wake kupata mbinu ya kuganga na kutibu magonjwa hayo. Tarehe 8 Desemba 1602 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Geneva nchini Uswis, kiasi cha kujipambanua kuwa ni: Mtume, mhubiri, mtunzi, mchapa kazi, mchamungu na mtekelezaji wa maamuzi makubwa yaliyokuwa yamefikiwa kwenye Mtaguso wa Trent. Akajizamisha katika majadiliano ya kiekumene, mahusiano na mafungamano ya binasi pamoja na huduma ya upendo. Alidhaminishwa shughuli za kidiplomasia, akatafsiri mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakitendeka nchini Ufaransa na hatimaye, kuwa ni kiongozi aliyezima kiu ya watu waliokuwa wanamtafuta Mungu.
Kati ya Mwaka 1620 na 1621 alitambua kwamba, mshumaa wa maisha yake, ulianza kuzimika taratibu na katika maandishi yake akakazia kwa namna ya pekee kuhusu upendo kwamba, hufanya yote kwa ajili ya watoto wake na kwamba, upendo unapaswa kuwa ni kiini cha mabadiliko katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, akakazia amani katika mahitaji ya mabadiliko ya nguvu. Baba Mtakatifu Francisko anasema maadhimisho ya Miaka 400 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Sales, ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na mang’amuzi yake na kwamba, amekuwa ni chachu muhimu sana katika kutangaza na kushuhudia Injili; mambo msingi yaliyompatia nguvu ya mabadiliko ya ndani. Katika maisha na utume wake alikazia: utu, upendo na urafiki kama vifungu muhimu vilivyobainisha ile nguvu ya neema ya Mungu kama inavyofafanuliwa na wanalasafa na wanataalimungu. Neema ya Mungu ni kielelezo makini cha upendo wake, unaoheshimu uhuru wa mwanadamu, na kumwachia fursa ya kuwa ni mdau katika maamuzi yake. Haya ni mambo muhimu katika maongozi ya maisha ya kiroho. Mtakatifu Francisko wa Sale anasema, Ibada ya kweli haijipambanui kwa kusali kwa muda mrefu na kufunga; kwa kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kuwasamehe maadui au kulipa deni. Kwa maneno mafupi, mizizi ya dhambi ni sehemu ya mapambano ya maisha ya kiroho na wala si kielelezo cha Ibada ya kweli. Kwa hakika ibada ya kweli inapata chanzo na hitimisho lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kuwasha moto wa upendo na kuendelea kuambata Amri za Mungu na Mashauri ya Kiinjili, kiasi kwamba, Ibada ya kweli inakuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa mwamini unaokoleza mchakato wa kutafuta na kuambata utakatifu ambao kimsingi ni wito na mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa kikundi cha watu wachache tu! Ibada ya kweli ni kwa ajili ya watu wote.