Mtakatifu Rosa wa Viterbo: Shuhuda wa Toba ya Ndani, Upatanisho na Utakatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Rosa wa Viterbo, Italia alizaliwa kunako mwaka 1233 na kwamba, alikuwa ni msichana maarufu sana wa imani yake katika Kristo Yesu, aliyethubutu kujiunga mapema sana na Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Alianza kuishi kama mkaa pweke, akiwa na umri wa miaka saba na alihubiri toba na upatanisho. Alifariki dunia tarehe 6 Machi 1251. Chama cha Wapagazi wa Mtakatifu Rosa wa Viterbo kilianzishwa kunako mwaka 1978 ili kubeba Sanamu ya Mtakatifu Rosa wa Viterbo wakati wa maadhimisho ya sikukuu yake, huku wakikumbuka tukio la mwaka 1258 Papa Alexander IV aliporuhusu masalia ya Mtakatifu Rosa wa Viterbo kuhamishwa kutoka katika Kanisa la “Santa Maria in Poggio” kwenda kwenye Kanisa la “Santa Maria delle Rose”, Kanisa hili leo hii ni Madhabahu ya Mtakatifu Rosa wa Viterbo. Maadhimisho haya yamendelea kuboreka hadi kufikia nyakati hizi.
Kwa hakika Mtakatifu Rosa wa Viterbo aliishi mjini Viterbo akahamasisha na kukuza Ibada ya uhai wa maisha ya Kikristo. Katika ujana wake, akaamua kuishi ufukara na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini kiasi cha “kuchafua” hali ya hewa na kuanza kuchukiwa hata na viongozi wa Serikali, kiasi cha kupelekwa uhamishoni pamoja na familia yake. Huyu ni Mtakatifu aliyejaa nguvu za Roho Mtakatifu, kiasi kwamba, mang’amuzi yake ya ndani, yasingeweza kubaki yamefichama, bali yalionekana na kudhihirika kwa watu. “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Mt 5:14-16.
Hii ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 alipokutana na kuzungumza na Wanachama wa Chama cha Wapagazi wa Mtakatifu Rosa wa Viterbo, aliyekuwa na mwamko wa kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kueneza utakatifu wa maisha. Wanachama hawa wanaendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu mintarafu huduma yao yenye mvuto na mashiko kwa watalii wanaotoka sehemu mbalimbali za dunia kwenda kutembelea Viterbo. Kunako mwaka 2013 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO liliwatambua kwamba, mashine ya wapagazaji wa Mtakatifu Rosa wa Viterbo kuwa ni urithi wa dunia na kwa njia ya hii wamekuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu.
Huu ni utume unaotekelezwa kwa njia ya umoja na mshikamano unaofumbatwa katika imani, nguvu, utashi, heshima na unyenyekevu mkubwa, kwani katika maandamano na katika maisha, kuna haja ya kushikamana. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa utume huu wanaoutekeleza kwa kujikita katika tunu msingi za kitamaduni, kanuni maadili na utu wema, bila kusahau huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kumbe, ni wajibu na dhamana yao kuhakikisha kwamba, wanaendeleza mapokeo haya na hatimaye, amewabariki.