Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa,Januari 2024:Zawadi ya utofauti wa karama katika Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila mwezi Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa unachapisha nia za sala za Baba Mtakatifu kwa njia ya Video. Kwa mwezi Januari 2024, Baba Mtakatifu anajikita na mada ya “kuombea zawadi ya utofauti wa karama za Kanisa.” Katika muktahda huo tunachapisha nia hizo ambapo Papa Francisko anazungumza kwa lugha ya Kihispania na kutafsiriwa kwa lugha mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema: “Hatupaswi kuogoa utofauti wa karama katika Kanisa. Kwa sababu wote hatuko sawa. Kinyume chake, tunapaswa kufurahi ya kuwa na tofauti hizi. Tayari katika Jumuiya za kwanza za Kikristo, utofauti na umoja ulikuwapo sana na katika nia, kwa ajili ya kusuluhisha katika mpango wa juu."
Papa vile vile anafafanua kuwa: "Lakini kuna cha zaidi. Kwa sababu ili kuweza kusonga mbele katika njia ya imani tunahitaji pia mazungumzo ya kiekumene na ndugu zetu wa madhehebu mengine na jumuiya za kikristo. Na sio jambo ambalo linachanganya au kuleta usumbufu, lakini ni kama zawadi ambayo Mungu anafanya kwa Jumuiya ya Kikristo, ili iweze kukua kama mwili mmoja, yaani mwili wa Kristo. Tufikirie kwa mfano, katika Makanisa ya Mashariki. Wao wana tamaduni zao, baadhi ya ibada za kiliturujia maalum, lakini bado wao wanahifadhi umoja wa imani. Wanaiimarisha, na sio kuigawanya. Ikiwa tunaacha tuongozwe na Roho Mtakatifu, utajiri, ukweli, utofauti haugeuki kamwe kuwa sababu ya migogoro."
Baba Mtakatifu Francisko anakazia kusema kuwa: "Roho Mtakatifu anatukumbusha kuwa awali ya yote, sisi ni wana wapendwa wa Mungu. Sisi sote tunafanana katika upendo wa Mungu na wote tuko tofauti. Tusali ili Roho atusaidie kujua zawadi ya utofauti wa karama ndani ya Jumuiya za Kikristo na kugundua utajiri wa tofauti za tamaduni, za ibada katika umbu la Kanisa Katoliki." Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha."
Ikumbukwe kwamba Ujumbe wa Papa kwa njia ya Video umetafsiriwa katika lugha 23 na kusambazwa katika nchi 114, na ambao hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara milioni 189 kwenye mitandao yote ya kijamii ya Vatican tangu 2016. Mtandao wa Nia ya Maombi ya Papa Kimataifa ni Kazi ya Kipapa, ambayo dhamira yake ni kuwahamasisha Wakatoliki wote kwa njia ya sala na matendo thabiti katika kukabiliana na changamoto za binadamu na utume wa Kanisa. Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni Padre Frédéric Fornos S.J.