Papa Francisko Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa “Walinzi wa Familia Tafakatifu”: Papa Francisko Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa “Walinzi wa Familia Tafakatifu”:   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mtandao wa Walinzi wa Familia Takatifu: Bikira Maria Mfano wa Kuigwa

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewapongeza kwa kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, aliyeyaweka hayo yote moyoni mwake. Amekazia huruma, neno ambalo kuna baadhi ya watu wangependa lifutwe kwenye kamusi, lakini Bikira Maria alikuwa ni mpole na Mwenye huruma kwa Kristo Yesu, Kanisa na kwa Ulimwengu. Wito wao unatekelezwa katika hali ya unyenyekevu, uaminifu na imani na ushirika kati yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa “Walinzi wa Familia Tafakatifu”: “Sentinelles de la Sainte Famille”, Mtandao wa sala ulioanzishwa takribani miaka kumi iliyopita, ukiwa na wito maalum kwa ajili ya kuandaa nia za sala kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Huu ni wito unaotekelezwa katika hali ya unyenyekevu, maisha ya sala, mambo msingi na yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ikiwa kama yanatekelezwa kwa uaminifu, imani na moyo wa ushirika kati yao. Mwenyezi Mungu kwa hakika anapenda mambo madogo madogo yanayo zaa matunda. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewapongeza kwa kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, aliyeyaweka hayo yote moyoni mwake. Amekazia huruma, neno ambalo kuna baadhi ya watu wangependa lifutwe kwenye kamusi, lakini Bikira Maria alikuwa ni mpole na Mwenye huruma kwa Kristo Yesu, Kanisa na kwa Ulimwengu.

Mtandao wa sala wa Walinzi wa Familia Takatifu
Mtandao wa sala wa Walinzi wa Familia Takatifu

Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa mtandao wa “Walinzi wa Familia Takatifu” unaoundwa na wanawake peke yao, wito usiokuwa na mbadala ndani ya Kanisa kwa mfano wa Bikira Maria. Huu ni mwaliko kwa walinzi hawa kujifananisha na Bikira Maria katika dhamana na wito wao kwa kazi ya uumbaji, kwa kujiunga pamoja naye ili kuwaombea watoto wote wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Ni katika muktadha huu, bila kujali hali yao ya maisha, wote ni akina mama. Kumbe, dhamana na wajibu wao kama walinzi wa Familia Takatifu unasimikwa katika mtindo wa maisha ya Bikira Maria. Wapende kuutazama Ulimwengu katika uhalisia wa maisha yake; mtazamo wa kimama unaosimikwa katika uvumilivu, upendo na uelewa. Huu ni mwaliko kwa walinzi hawa kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza katika maisha, mahusiano na mafungamano yao, si tu wakati wanapokutana kusali, lakini dhana hii inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ndani ya familia, Kanisani na katika maeneo ya kazi.

Bikira Maria awe ni mfano wao bora wa kuigwa
Bikira Maria awe ni mfano wao bora wa kuigwa

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, nyoyoni mwao wanabeba matukio ambayo pengine yana uchungu maishani mwao kama watu binafsi au kwa kudhaminiwa na watu wengine. Ndani mwa nyoyo zao wanabeba pia nia za ulimwengu, watu walioathirika kwa vita, kinzani, mipasuko pamoja na mahangaiko ya jirani zao, tayari kuyatafakari na kuyahiadhi. Huu ni mwaliko kwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia amani; kwa kuwaongoa watu kutoka katika vita, hali ya kutoeleweka pamoja na kukatishwa tamaa, lakini bila kulalama, huku wakiendelea kubaki katika hali ya ukimya, tayari kuyatafakari na kuyahifadhi. Akina mama wanafahamu vyema namna ya kupandikiza amani, ili kulinda na kudumisha imani na matumaini kwa sasa na kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu amekamilisha hotuba yake kwa kukazia huruma ambayo kwa sasa kuliko pengine wakati wowote wa historia ya mwanadamu inahitajika sana. Kuna baadhi ya watu wangependa neno huruma lifutwe kwenye kamusi, kwa sababu watu wanashindwa kubadilika, wanashindwa kuguswa na mateso pamoja na mahitaji ya wengine, lakini Bikira Maria alikuwa ni mpole na Mwenye huruma kwa Kristo Yesu, Kanisa na kwa Ulimwengu. Huu ndio pia wito wa “Wakinzi wa Familia Takatifu. Bikira Maria Mama wa Kanisa aliyahifadhi yote haya moyoni mwake. Hii ni changamoto kwao kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha ndani mwao huruma na upendo wa Bikira Maria kwa Kanisa na kwa Ulimwengu. Amewashukuru na kuwapongeza kwa kumtembelea na kwamba, ukuaji wao kwa idadi na kijiografia kamwe usiwafanye kupoteza unyenyekevu wa moyo!

Walinzi wa Familia Takatifu
11 January 2024, 15:22