Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini”   (Vatican Media)

Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Matumaini

Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 unapania pamoja na mambo mengine anasema Baba Mtakatifu Francisko kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini yanayoboreshwa kwa njia ya maisha ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024.

Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025
Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025

Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 unapania pamoja na mambo mengine anasema Baba Mtakatifu Francisko kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini. Huu ni mwaliko kwa kila jimbo, baada ya kusoma alama za nyakati kwa watu wake, liandae katekesi kuanzia wakati huu, hadi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 hapo tarehe 24 Desemba 2024. Katekesi hii ilenge kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kuingia katika lango la Jubilei, ambalo ni Kristo Yesu, Mwanakondoo Mungu. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 9 Machi 2024 anatarajiwa kuchapisha Waraka wa kuitisha Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Mwaka 2024. Waraka huu utakuwa na maelezo ya kina ya jinsi ya kuuishi mwaka wa Jubilei, tayari kujichotea neema na baraka. Majimbo mbalimbali yanahamasishwa kujiandaa kwa ajili ya hija majimboni mwao, kwenye madhabahu ya kikanda, kitaifa na kimataifa. Ili kuweza kuratibu vyema maadhimisho haya, kila Jimbo na kila taifa litatakiwa kuwa na Kamati ya Jubilei itakayokuwa na jukumu la kuratibu maadhimisho haya. Mababa wa Kanisa wanasema, Sala ni maisha ya moyo mpya; ni majadiliano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu, kielelezo cha juu kabisa cha mafao katika maisha ya mwanadamu. Sala ni nuru katika moyo wa mwanadamu, inayomwonjesha mwamini ile furaha ya maisha na uzima wa milele. Kusali ni silele mama ni jambo linalohitaji majiundo makini, ubunifu na utamaduni na kamwe kusali kusiwe ni mazoea!

Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025: Matumaini
Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025: Matumaini

Kwa upande wake, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, anasema, katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, kuna haja ya kujifunza kusali, ili sala iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa sanjari na kuzima kiu ya maisha ya kiroho yanayomuunganisha mwamini na Muumba wake. Kumbe, sala inakuwa ni rutuba ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni wakati wa kupyaisha tena na tena maisha ya sala. Kuna vitabu ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya malezi na majiundo ya sala kwa waamini, kwani kusali ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini katika ulimwengu mamboleo: Namna ya kusali Zaburi, Kusali na Watakatifu pamoja na wadhambi; Kanisa linalosali, Sala ya Bikira Maria na ya Watakatifu, Sala kuu ya Baba Yetu. Kumbe, waamini wajenge utamaduni wa kusali kama mtu binafsi, ndani ya familia, kwenye Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Parokiani. Hizi ni Sala za kushukuru, kuomba, kutukuza, kutafakari, faraja na kuabudu.

Mwaka wa Sala unalenga kupyaisha imani, matumaini na mapendo
Mwaka wa Sala unalenga kupyaisha imani, matumaini na mapendo

Ni katika muktadha wa Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameandika dibaji kwenye kitabu kilichotungwa na Kardinali Angelo Comastri “Pregare Oggi. Una Sfida da Vincere” yaani “Sala kwa nyakati hizi ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga.” Baba Mtakatifu katika utangulizi huu anakazia maana ya sala, utamaduni wa kujenga na kudumisha ukimya kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Rej. Mt 6:7-8. Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Hii ni fursa kwa Mama Kanisa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni muda muafaka wa kujenga imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu hasa baada ya patashika nguo kuchanika kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, athari za mabadiliko yatabianchi bila kusahau mgogoro wa kiikolojia, kiuchumi na kijamii pamoja na vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia; yote haya ni mambo yanayoonesha umuhimu wa kusali. Huu ni wakati muafaka wa kurudi tena kwenye shule ya sala, kama walivyoomba wale Mitume wa Yesu: Bwana tufundishe kusali. Rej. Lk 11:1. Waamini wajinyenyekeshe mbele ya Mungu katika sala, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawasikiliza. Wamwachie nafasi Roho Mtakatifu katika maisha na sala zao, ili aweze kuwakirimia maneno yanayofaa ili kuwaunganisha waamini kama familia moja ya Mungu. Maisha ya sala yawe ni msingi wa kutangaza na kushuhudia matumaini kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala Kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Familia, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo pamoja na nyumba ya kitawa ziwe ni mahali muafaka pa sala, kama ilivyo hata kwa mwamini mmoja mmoja, kutafuta fursa ya ukimya, ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yake. Rej. Lk 18:1.

Mwaka wa sala 2024

 

31 January 2024, 15:48