Nia za sala mwezi Februari 2024:kutunza na kusindikiza wagonjwa mahututi na familia zao

Video ya Papa ya Februari 2024,mwezi ambao Kanisa linaadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani,inazindua wito ili wagonjwa mahututi wapate huduma muhimu na kusindikizwa,kwa mtazamo wa kiafya na wa kibinadamu.‘Ponya ikiwezekana,jitunze sikuzote’anasitiza Papa na jukumu kuu la familia ambazo haziwezi kuachwa peke yake.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika toleo la mwezi Februari  2024 kwa njia ya Video ya Papa, nia ya Papa Francisko anaomba sala na kujitolea kwa ajili ya wagonjwa mahututi na familia zao. Baba Mtakatifu anashiriki nia yake ya maombi kwa mwezi huu unaoadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani, ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alianzisha mnamo mwaka 1992 inayoadhimishwa tarehe 11 Februari kila mwaka na ambayo ni kumbukumbu ya kiliturujia ya Bikira Maria wa Lourdes.

Nia za Papa za kuombea wagonjwa na familia zao  Feb 2024
Nia za Papa za kuombea wagonjwa na familia zao Feb 2024

Baba Mtakatifu Francisko katika nia hiyo anaeleza kwamba: “wakati baadhi ya watu wanapozungumza kuhusu magonjwa yasiyotibika, kuna maneno mawili ambayo mara nyingi huchanganya: yanayotibika na yasiyotibika. Lakini hayafanani.” Akimnukuu Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, Papa Francisko anathibitisha kuwa: “Tibu ikiwezekana; jitunze siku zote”, katika ujumbe kwa njia ya video aliuelekeza kila mwamini kupitia  (Pope’s Worldwide Prayer Network,) Mtandao wa Sala ya Kimataifa.  

Kutunza na kuponya

Katika video hiyo, tunaona: wanandoa kutoka nyuma, wakitafakari bahari, kijana akimkumbatia mwanamke mdogo ambaye amepoteza nywele kutokana na mionzi (chemotherapy); msichana katika chumba cha hospitali akimkumbatia babu yake; mwanaume kando ya kitanda cha baba yake, akiwa na Biblia mapajani mwake na Rozari mikononi mwake; mgonjwa ambaye hawezi tena kutembea akisaidiwa na nesi katika bustani; daktari akiieleza familia njia ngumu watakayohitaji kusindikiza mpendwa wao.

Wanandoa wakitafakari bahari
Wanandoa wakitafakari bahari

Kulingana na jinsi zinavyotafsiriwa, picha kutoka katika Video ya Papa ya mwezi Februari zinaonesha mfululizo wa kushindwa au mafanikio: kushindwa, ikiwa matokeo pekee yanayokubalika ni tiba; mafanikio, ikiwa lengo lake ni utunzaji wa mgonjwa. Kuponya na kutunza hunaonekana kuwa sawa, lakini si hivyo.

Nesi kwa mgonjwa na familia yake
Nesi kwa mgonjwa na familia yake

Papa Francisko anafafanua hilo kwa uwazi kuwa: “hata kama kuna uwezekano mdogo wa kupata tiba, “kila mgonjwa ana haki ya kupata usaidizi wa kimatibabu, kisaikolojia, kiroho na kibinadamu.” Na anaendelea kusema: “Uponyaji hauwezekani kila wakati, lakini tunaweza kumtunza mgonjwa kila wakati na kumbembeleza.”

Wagonjwa, familia na huduma shufaa

Katika utamaduni wetu wa kutupa, hakuna tena mahali pa wagonjwa mahututi. Na si kwa bahati kwamba, katika miongo kadhaa iliyopita, majaribu ya euthanasia yamekuwa yakiongezeka katika nchi nyingi. Badala yake, Papa Francisko anatualika kumtazama mgonjwa kwa upendo na kuelewa, kwa mfano, kwamba kuwasiliana kimwili kunaweza kusaidia sana hata kwa wale ambao hawawezi tena kuzungumza na ambao hawaonekani tena kuwatambua jamaa zao tena  lakini wanahitaji  kuwasaidia kwa njia iliyo bora zaidi kadiri wanavyohitaji. Si swali kuhusu kurefusha mateso isivyo lazima. Badala yake, Papa anasisitiza juu ya umuhimu wa huduma Shufaa na jukumu la familia ambayo, kama Baraza la  Mafundisho Tanzu ya Kanisa linaandika katika barua ya ziada ya Msamaria Mwema mnamo 2020, “Kubaki kando ya kitanda cha wagonjwa, kutoa ushahuda wa thamani na wa kipekee na usiyoweza kurudiwa.”

Kuhusiana na huduma ya tiba shufaa, Papa Francisko amethibitisha kwamba: “humhakikishia mgonjwa si tu matibabu, bali pia usaidizi wa kibinadamu na ukaribu.” Wakati huohuo, anapozungumza kuhusu wajibu wa familia, anatukumbusha kwamba: “hawapaswi kuachwa peke yao katika nyakati hizi ngumu,” na kwamba “jukumu lao ni la kuamua na wanahitaji kupata njia za kutosha ili kuandaa ifaayo kimwili, kiroho na msaada wa kijamii.” Ndiyo maana Papa Francisko anahitimisha  Ujumbe wake kwa njia ya video kwa kuomba sala na ahadi kutoka kwa kila mtu ili: “wagonjwa wasiotibika na familia zao daima wapate huduma na usaidizi unaohitajika wa kimatibabu na kibinadamu.”

Kama samaria Mwema

Kwa mujibu wa Padre Frédéric Fornos S.J.,Mkurugenzi wa Kimataifa  wa (Pope's Worldwide Prayer Network,) wa Mtandao wa sala wa Kimataifa, uliyopo katika nchi 89, zenye Wakatoliki zaidi ya milioni 22, anauliza: “Kwa nini tusali kwa ajili ya nia hii? Je, haitatosha kwa Papa kutoa tamko kuhusu mada hii? Je, kweli maombi hubadilisha chochote? Haya ndiyo maswali ambayo tunaweza kujiuliza.” Padre Fornos anaendelea kusema: “Magonjwa yanapogonga kwenye mlango wa maisha yetu, hitaji linatokea ndani yetu kwamba mtu awe karibu nasi, atuangalie machoni mwetu, atushike mkono, atuoneshe huruma na kutujali, kama Msamaria mwema katika mfano wa Injili. Kwa hiyo ukaribu huu na mapenzi ya kibinadamu kwa wagonjwa mahututi yanaweza kuonekana kuwa nyongeza au ya pili kuhusiana na usaidizi wa kimatibabu. Maombi yanaweza kuangukia katika kundi hili pia. Walakini, msaada huu ni muhimu. Ni upendo unaooneshwa kupitia matendo haya na maombi yetu. Katika nyakati hizi ngumu, familia zina jukumu muhimu, Papa Francisko anasema. Hebu tuombe, basi, kwamba wagonjwa mahututi na familia zao wapate huduma na usaidizi unaohitajika kila wakati.”

Nia za sala ya papa kwa mwezi Februari 2024
30 January 2024, 17:33