Tafuta

Wajumbe wa Chama cha Kimataifa cha Wanahabari Walioidhinishwa kwa Chama cha Waandishi wa Habari cha Vatican, Jumatatu tarehe 22 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wajumbe wa Chama cha Kimataifa cha Wanahabari Walioidhinishwa kwa Chama cha Waandishi wa Habari cha Vatican, Jumatatu tarehe 22 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Akutana na Chama Cha Waandishi wa Vatican: Wito!

Baba Mtakatifu amewashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, ametafakari kuhusu utume wao mjini Vatican; taaluma ya mwandishi wa Habari; umuhimu wa kuzama katika asili na roho ya matukio; vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaasili ya kutaka kupotosha habari za kidini na taswira ya Kanisa na kwamba, waandishi wa tasnia ya mawasiliano ya Vatican wanapaswa kujenga na kuisimika kazi yao juu ya mwamba wa uwajibikaji katika ukweli na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Chama cha Kimataifa cha Wanahabari Walioidhinishwa kwa Chama cha Waandishi wa Habari cha Vatican: “Associazione Internazionale dei Giornalisti Accreditati in Vaticano (AIGAV) Association of Journalists Accredited to the Vatican” kilianzishwa mjini Roma, tarehe 6 Juni 1978 kama as Association de la presse internationale auprès de la salle de la presse du Saint-Siège (ASISS); jina lilibadilishwa rasmi kunako mwaka 1982. Lengo ni kukuza na kudumisha moyo wa Mkataba wa Helsink, Finland wa kuchangia katika mchakato wa usambazaji wa taarifa za shughuli zinazoendeshwa na Vatican pamoja na Taasisi za Kanisa Katoliki, ili kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo mwendelezo kwa mazungumzo kati ya wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii pamoja na Vatican. Wajumbe wa Chama cha Kimataifa cha Wanahabari Walioidhinishwa kwa Chama cha Waandishi wa Habari cha Vatican, Jumatatu tarehe 22 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, ametumia fursa hii kuwashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, ametafakari kuhusu utume wao mjini Vatican; taaluma ya mwandishi wa Habari wa Vatican; umuhimu wa kuzama katika asili na roho ya matukio; vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaasili ya kutaka kupotosha habari za kidini na taswira ya Kanisa na kwamba, waandishi wa tasnia ya mawasiliano ya Vatican wanapaswa kujenga na kuisimika kazi yao juu ya mwamba wa uwajibikaji katika ukweli ili kuepuka usomaji wa kiitikadi.

Waandishi wa Habari mjini Vatican wakutana na Papa Francisko.
Waandishi wa Habari mjini Vatican wakutana na Papa Francisko.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wadau mbalimbali wa tasnia mawasiliano kwa kazi kubwa wanayoifanya katika ngazi ya kitaifa na kwamba, wao wanaunganishwa na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Na kwamba uandishi wa habari wa Vatican ni wito sawa na ule wa udaktari ambaye anachagua kupenda ubinadamu, ili aweze kumponya magonjwa yake. Hivi ndivyo ilivyo kwa mwandishi habari wa Vatican anayechagua kugusa majeraha ya jamii na dunia. Huu ni wito unaopata chimbuko lake katika ujana, changamoto ni kuutambua na hivyo kujenga upendo usio na masharti kwa ukweli. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kazi kubwa wanayoitekeleza, kwa kuandika habari za Vatican na Kanisa katika ujumla wake kwa uvumilivu, kwa kuzingatia huruma, sheria na uaminifu katika kazi zao. Hawa wamekuwa ni wandani wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika hija zake za maisha na utume, sehemu mbalimbali za dunia. Amewaomba radhi kwa kuwanyima fursa za kukaa na kucheza pamoja na familia zao. Wanatasnia hawa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao, wao ni wajenzi wa madaraja ya maarifa na mawasiliano badala ya kuwa ni wajenzi wa kuta za utengano na hali ya kutoaminiana. Mwandishi wa habari wa Vatican ni taaluma ambayo ni ya haraka sana kiasi hata cha kukosa huruma; ni taaluma yenye usumbufu mwingi. Lakini hii ni sanaa ya kutafuta na kusimulia matukio mbalimbali ya maisha na utume wa Kanisa; hii pia ni njia ya kumpenda mwanadamu, kwa unyenyekevu pamoja na majitoleo makuu.

Papa Francisko akizungumza na wajumbe wa AIGAV.
Papa Francisko akizungumza na wajumbe wa AIGAV.

Hii ni kazi yenye magumu yake, lakini jambo la msingi ni kwamba, hii ni kazi nzuri inayotia moyo wa kumpenda binadamu na kuendelea kujifunza kwa unyenyekevu. Hii ni changamoto kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuzama zaidi katika asili na roho ya matukio; kwa kusimamia ukweli wa maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia madhumuni yake ya maisha ya kiroho, maadili na utu wema, badala ya kung’ang’ania na kujikita tu katika kashfa zinazolichafua Kanisa! Wadau wa tasnia ya mawasiliano Vatican wajifunze kuwa na aibu ya kukaa kimya! Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kutafuta na kuandika ukweli; wazingatie ulinganyifu wa habari na tafakari; kuzungumza na  kwa kusikiliza; kwa kuwa na utambuzi mpana pamoja na upendo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii vinalenga kuandika habari za kupotosha mambo ya kidini na kukuza maelekeo ya kiitikadi na kisiasa kwa kutoa habari nyepesi nyepesi. Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutangaza na kushuhudia ukweli, bila kupiga makelele yasiyokuwa na mafao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa: Kanisa lina dhamana ya kujikita katika mchakato wa mawasiliano yaliyo bora zaidi kwa njia ya ushuhuda kabla ya hata ya kusema maneno. Baba Mtakatifu anasema, amejifunza na anawafahamu wote kwa majina na kwamba, anawashukuru sana kutoka katika sakafu ya moyo wake!

Vaticanist 2024 Ok

 

 

 

22 January 2024, 15:38