Papa kwa Klabu ya Tenisi ya Barcelona:watoto wana ndoto ya maisha bora ya baadaye
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu, Jumatatu tarehe 29 Januari 2024 amekutana na Klabu ya mchezo wa Tenisi ya Barcelona nchini Hispania ambapo ameshukuru kufika kwao katika fursa ya maadhimisho ya miaka 125 ya kuanzishwa kwa Klabu ya mchezo huo na kuonesha furaha ya kusisitiza kwa mara nyingine tena kuhusu fursa ambayo mchezo unatoa kwa ajili ya kukua kila siku kama mtu na kama jamii. Papa amesema kuwa "Tenisi hasa, kutokuwa mchezo wa timu, lakini kuwa mchezo wa mtu binafsi au watu wawili, unatoa kipengele cha kuvutia kwa tafakari yetu." "Unaweza kuonekana kuwa changamoto kati ya wachezaji unaohusiana zaidi na hamu ya kumshinda mpinzani. Walakini, tukiangalia historia ya kilabu yao, tunaweza kuona kwamba kiukweli, tangu asili yake ya Kiingereza, ni kielelezo cha uwazi wa waanzilishi wa kile kizuri kinachoweza kutoka nje na mazungumzo na tamaduni zingine, ambazo ziliwaruhusu kutoa maisha kwa ukweli mpya."
Baba Mtakatifu Francisko kwa hiyo amesema hili ni fundisho linalotumika hadi leo kama ilivyokuwa kwa miaka 125 iliyopita. Katika mchezo wa tenisi, kama ilivyo katika maisha, hatuwezi kushinda kila wakati, lakini itakuwa changamoto ya kutajirisha ikiwa, kwa kucheza kwa adabu na kulingana na sheria, tunajifunza kuwa sio pambano bali ni mazungumzo ambayo yanahusisha juhudi zetu na kuturuhusu kuboreka. Kwenye uwanja, kama vile uwepo wa maisha, wakati mwingine tunahisi kuwa peke yetu, wakati mwingine tunaungwa mkono na wale wanaocheza mchezo huo wa maisha na sisi. Lakini, hata tunapocheza ‘binafsi’, sisi huwa tuko mbele ya Bwana ambaye hutufundisha nini maana ya heshima, ufahamu na hitaji la mawasiliano ya mara kwa mara na wengine.
Kwa kumalizia, Papa Francisko ameomba aruhusiwe kuwaeleza “jambo la mwisho kwamba wao wamewafunza wachezaji wa tenisi wa kimataifa ambapo ni changamoto kubwa, lakini tunapofanya kazi na watoto hawa, ambao wana ndoto ya maisha bora ya baadaye ya michezo, mahitaji ya mafunzo hayawezi kuwashinda ukuaji kamili; hakuna kitu muhimu zaidi kuliko maendeleo haya ya kibinadamu na kiroho. Kwa hivyo watunze watoto, wale ambao wanaweza kufaidika na maadili ya michezo katika muktadha tata wa kijamii, na pia wale ambao wanaweza kufanikiwa katika mashindano ya kiwango cha juu. Wasiache kuwa watoto! Asante.”