Papa kwa Vyuo vikuu Katoliki:visaidie kutafsiri lugha mpya kiutamaduni kwa vizazi
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 19 Januari 2024 amekutana mjini Vatican na Shirikisho la Kimataifa la Vyuo Vikuu Katoliki, (FIUC/IFCU) ambapo, hotuba yake amewakabidhi ili wajisomee. Kabla ya hapo, Baba Mtakatifu amezungumza maneno machache bila kusoma kwamba: “Nilikuwa nimandaa kusoma hotuba ndefu, lakini nina pumzi fupi kidogo; kama mnavyoona, baridi hii haiendani nami! Ninawapatia maandishi ili mjisomee wenyewe. Ninawashukuru nyote kwa mkutano huu na kwa mema yote ambayo vyuo vikuu vyetu vya Kikatoliki vinafanya kwa kuwasilisha maarifa, neno la Mungu na ubinadamu halisi. Msichoke kuvumilia katika utume wa ajabu wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki. Sio katika hali yake ya umojia inayowapatia utambulisho wao: hiyo ni kipengele kimoja tu, lakini sio cha kipekee. Pengine ni ule ubinadamu ulio wazi, unaowafanya watu watambue kwamba wanadamu wana maadili na kwamba haya yanahitaji kuheshimiwa. Hili labda ndilo jambo bora na kuu zaidi kuhusu vyuo vikuu vyenu. Asante sana.” Papa alihitimisha.
Katika hotuba iliyowakabidhi Baba Mtakatifu anayofuraha kushiriki katika maadhimisho ya miaka mia moja ya Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Duniani (IFCU). Miaka mia moja ya ukuaji na maendeleo ni sababu ya shukrani kubwa! Amemsalimia na kumshukuru Kadinali José Tolentino de Mendonça na Profesa Isabel Capeloa Gil, Rais wa Shirikisho hilo. Baba Mtakatifu anabainisha kuwa Papa Pio XI alibariki chama cha kwanza cha vyuo vikuu kumi na nane vya Kikatoliki mnamo mwaka 1924, ambacho, kwa kutaja Azimio la baadaye la “Baraza la Seminari na Vyuo Vikuu vya Mafunzo, lilikusanyika pamoja ili Wakuu wao kufanya mambo ambayo yalihitaji kushughulikiwa kwa pamoja katika kutekeleza azimio hilo”(29 Juni 1948).
Miaka 25 baadaye, mnamo 1949, Mtakatifu Pio XII alianzisha Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki. Papa Francisko amependa kwa hiyo kuakisi vipengele viwili vya mizizi hii ya kihistoria ya Shirikisho lao. Kwanza, kutia moyo ili kushirikiana kupitia "mitandao". Leo kuna karibu vyuo vikuu elfu mbili vya Kikatoliki katika ulimwengu wetu. Tunaweza kufikiria uwezekano wa mahusiano ya kazi yenye ufanisi zaidi na kuboreshwa kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki. Wakati wa mgawanyiko mkubwa ni lazima kuthubutu kukabiliana na mwelekeo huo, na kutandaza matumaini, umoja na maelewano badala ya kutojali, ubaguzi na migogoro.
Mantiki ya Pili ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuakisi amebainisha kuwa inatokana na ukweli kwamba, kama vile Pio XII alivyosema, Shirikisho lilianzishwa “kufuatia vita vya kutisha”, ili kuwa njia ya kuhamasisha upatanisho na ukuaji wa amani na upendo kati ya watu” (Waraka wa Kitume Catholicas, Studiorum Universitates, 27 Julai 1949). Papa amesema inasikitisha kusema, tunasherehekea miaka mia moja dhidi msimamo wa vita, vita vya tatu vya ulimwengu vilivyogawanyika vipande vipande. Ni muhimu zaidi, basi, kwamba vyuo vikuu vya Kikatoliki viwe mstari wa mbele katika juhudi za kujenga utamaduni wa amani katika nyanja zake zote, unaohitaji kushughulikiwa katika maono kati ya taaluma mbalimbali.
Katika Katiba yake ya Kitume Ex Corde Ecclesiae, Magna Carta ya vyuo vikuu vya Kikatoliki, Mtakatifu Yohane Paulo II alianza kwa kutoa kauli ya kushangaza kwamba Chuo kikuu cha Kikatoliki kimezaliwa “kutoka moyoni mwa Kanisa” (Na. 1). Kwa hiyo Papa Francisko anabainisha kuwa “Huenda tulitarajia aseme kwamba ilizaliwa na akili ya Kikristo. Lakini hata hivyo Papa alitoa kipaumbele kwa moyo wa katiba hiyo: ex corde ecclesiae. Kwa hakika, chuo kikuu cha Kikatoliki, kikiwa “mojawapo ya chombo bora zaidi ambacho Kanisa hutoa kwa zama zetu” (ibid., 10), hakiwezi kushindwa kuwa onesho la upendo unaochochea kila utendaji wa Kanisa, yaani, upendo wa Mungu kwa mtu wa kibinadamu.
Katika wakati ambapo, kwa bahati mbaya, elimu yenyewe inageuka kuwa “biashara,” na mifumo mikubwa ya kiuchumi isiyo na utu inawekeza katika shule na vyuo vikuu kama inavyofanya katika soko la hisa, taasisi za Kanisa lazima zioneshe kwamba zina asili tofauti na kutenda katika kulingana na mawazo tofauti. Biashara ya elimu haitegemei programu tu kamilifu, vifaa bora au mazoea mazuri ya biashara. Shauku kubwa lazima ihuishe chuo kikuu, kama inavyothibitishwa katika utafutaji wa pamoja wa ukweli, upeo mkubwa wa maana, unaoishi katika jumuiya ya ujuzi ambapo ukarimu wa upendo unaonekana.
Mfalsafa Hannah Arendt, ambaye alisoma dhana ya upendo katika maandishi ya Mtakatifu Augustino, alisema kwamba mwalimu mkuu alielezea upendo kwa neno appetitus, inayoeleweka kama mwelekeo, hamu, kujitahidi. Ushauri wa Baba Mtakatifu kwao basi ni huu: “Msipoteze hamu yenu! Hifadhi nguvu ya upendo wenu wa kwanza! Msiruhusu vyuo vikuu vya Kikatoliki kuchukua nafasi ya tamaa na utendakazi au urasimu. Haitoshi kutoa digrii za kitaaluma bali ni muhimu kuamsha na kuthamini katika kila mtu hamu ya “kuwa” to “be”.
Haitoshi kuwatayarisha wanafunzi kwa kazi za ushindani: ni muhimu kuwasaidia kugundua miito yenye matunda, kuhamasisha njia za kuwepo kiukweli na kuunganisha mchango wa kila mtu ndani ya mienendo ya ubunifu ya jumuiya kubwa. Kwa hakika, tunahitaji kutafakari juu ya akili ya bandia, lakini pia juu ya akili ya kiroho, ambayo bila kufanya hivyo watu hubakia wageni kwao wenyewe. Chuo kikuu ni rasilimali muhimu sana kuweza kuishi tu “kulingana na wakati,”,tukiweka kando wajibu unaotakiwa na mahitaji ya kina ya binadamu na ndoto na matarajio ya vijana.
Katika hilo Papa Francisko katika hotuba yake amependa kutaja historia iliyosimuliwa na mwandishi Franz Kafka, ambaye alikufa miaka mia moja iliyopita. Tabia yake kuu ni panya ambaye anaogopa na ukuu wa ulimwengu na anatafuta ulinzi wa kutuliza kati ya kuta mbili, moja kulia na nyingine upande wa kushoto. Wakati fulani, hata hivyo, aliona kwamba kuta zinaanza kusogea karibu zaidi na alikuwa katika hatari ya kupondwa. Alianza kukimbia lakini pembeni alipata mtego wa panya unaomsubiri. Wakati huo, alisikiliza shauri la paka, ambaye alimwambia: “Unachohitaji kufanya ni kubadili mwelekeo tu.” Akiwa amekata tamaa, alimsikiliza paka, ambaye kisha alimkanyaga.”
Baba Mtakatifu amekazia kusema kuwa “Hatuwezi kuruhusu woga kuongoza usimamizi wa vyuo vikuu vyetu; kwa bahati mbaya, hii hutokea mara nyingi zaidi kuliko tunavyofikiri. Kishawishi cha kujificha nyuma ya kuta, katika kiputo salama cha kijamii, kuepuka hatari au changamoto za kiutamaduni, kugeuza migongo yetu juu ya utata wa ukweli unaweza kuonekana kuwa njia salama zaidi. Lakini huu ni udanganyifu mtupu. Hofu inakula roho. Kamwe msizunguke chuo kikuu na kuta za hofu. Msiruhusu chuo kikuu cha Kikatoliki kuiga tu kuta za jamii tunamoishi: zile za ukosefu wa usawa, kudhalilisha utu, kutovumilia na kutojali, au mifano inayolenga kukuza ubinafsi badala ya kuwekeza katika udugu.”
Kwa hiyo Chuo kikuu kinachotafuta ulinzi ndani ya kuta za hofu kinaweza kupata hadhi, kutambuliwa na kuthaminiwa, na kupata cheo cha juu katika suala la uzalishaji wa kitaaluma. Hata hivyo, kama vile mwanafalsafa Miguel de Unamuno alivyosema wakati mmoja: “Maarifa kwa ajili ya ujuzi: huo si utu.” Ni lazima kila mara tujiulize: Ni nini kusudi la mafunzo tunayotoa? Je, ni uwezo gani wa kubadilisha maarifa tunayozalisha? Tunatumikia nini na nani? Kutoegemea upande wowote ni utani. Chuo kikuu cha Kikatoliki lazima kifanye chaguzi, chaguzi zinazoakisi Injili. Ni lazima ichukue msimamo na ioneshe waziwazi katika matendo yake, “kuichafua mikono yake” katika roho ya Injili, kwa ajili ya mabadiliko ya ulimwengu na katika huduma kwa mwanadamu.
Kabla ya mkutano huu mashuhuri unaojumuisha Makansela Wakuu, Wasimamizi na mamlaka nyingine za kitaaluma, Papa amependa kutoa shukrani zake kwa yote ambayo vyuo vikuu vya Kikatoliki tayari vinafanya katika suala hili. Ni kiasi gani cha kujitolea, uvumbuzi, hekima na utunzaji unaoleta kwa dhamira tatu ya chuo kikuu yaani ya: kufundisha, utafiti na kufanya kumbu kumbu kwa jamii! Kwa hilo, hakika amewashukuru. Pia Baba Mtakatifu ameomba msaada wao. Hasa wa kulisaidia Kanisa, wakati huu katika historia yake, kutoa mwanga juu ya matarajio ya ndani kabisa ya mwanadamu kwa kutoa ufahamu na maarifa, pamoja na ‘sababu za matumaini’ (rej. 1 Pet 3:15) iliyozaliwa na imani na hivyo kusaidia Kanisa kushiriki kwa ujasiri katika mazungumzo juu ya masuala makuu ya wakati wetu. Vyuo vitusaidie kutafsiri kiutamaduni, kwa lugha iliyo wazi kwa vizazi vipya na nyakati mpya, utajiri wa mapokeo ya Kikristo; kubainisha mipaka mipya ya fikra, sayansi na teknolojia na kuiendea kwa usawa na hekima.
Papa Francisko vile vile amesema vyuo vikuu Vitusaidie kujenga maagano ya vizazi na kiutamaduni kwa ajili ya ulinzi na utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja, ndani ya maono ya ikolojia fungamani na kwa njia hii kujibu kwa ufanisi kilio cha dunia na ombi la maskini. Baba Mtakatifu aidha amebainisha kuwa katika makanisa mengi ya Vyuo Vikuu vyao kuna picha ya Mama Yetu, Kikao cha Hekima. Papa amewaalika kutafakari kwa upendo hekima na kuzingatia kwa makini. Nini siri ya Mama yetu wa Hekima? Ni kwamba anatuletea Yesu, Hekima ya Mungu, ambaye anatupatia vigezo vya kuelekeza kila utafutaji wa maarifa. Kwa hiyo watazamae moyo wa Maria ili waweze kusindikizwa naje, jumuiya zao za kitaaluma na mipango yao ya baadaye. Papa Francisko anahitimisha kwa kuwapatia Baraka na kuomba tafadhali wasali kwa ajili yake.