Papa kwa Wakarismatiki amesisitiza juu huduma ya sala na Uinjilishaji
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amekutana mjini Vatican na Baraza la Kitaifa la Harakati ya Uhuisho wa Roho Mtakatifu tarehe 20 Januari 2024. Katika hotuba yake amemsalimia Rai na wajumbe wote pamoja na washiriki wa Harakati hiyo. Kama wanavyojua, katika miaka ya hivi karibuni Papa alitangaza CHARIS kama shirika la huduma ya kimataifa la Upyaishaji wa Karismatiki Katoliki. Na hata hivi karibuni mwezi Novemba 2023, Papa alipata fursa ya kuzungumza na washiriki wa mkutano ulioandaliwa na CHARIS. Kwa njia hiyo amewahimiza kuendelea kutembea kwenye njia hiyo ya ushirika na kufanya kuwa tunu ya maelekezo aliyowapatia. Papa Francisko akiwa nao wanaosimamia harakati katika ngazi ya kitaifa amewaomba awashirikishe mtazamo wa kichungaji kuhusu uwepo wao na huduma yao. Awali ya yote Papa amemshukuru Bwana na kushukuru kwa mema ambayo jumuiya za Harakati hiyo hupanda kati ya Watu watakatifu, waaminifu wa Mungu, kwa kusaidia hata hali ya kiroho rahisi na yenye furaha. Papa amesisitiza mantiki mbili muhimu: Huduma katika sala hasa ya kuabudu, na huduma ya Uinjilishaji.
Harakati ya Karismatiki kwa asili yake hutoa nafasi na umuhimu kwa maombi, kwa namna ya pekee kwa sala ya kutoa sifa, na hii ni muhimu sana. Katika ulimwengu unaotawaliwa na utamaduni wa kuwa na ufanisi, na pia katika Kanisa wakati mwingine unaohusika sana katika shirika, Papa ametoa angalisho la kuwa makini na hilo! “Sisi sote tunahitaji kutoa nafasi kwa kutoa shukrani, sifa na mshangao mbele ya neema ya Mungu.” Papa Francisko amewaomba hao ndugu kuendelea na kulitumikia Kanisa katika hilo, hasa kwa kuendeleza maombi ya kuabudu. Ibada ambayo ndani yake ukimya utawale na , ambapo Neno la Mungu lishinde maneno yetu, kwa kifupi Papa amesisitiza kuwa iwe ibada ambayo Yeye, Bwana, awe katikati, na sio sisi.”Hiyo ndiyo mantiki ya kwanza ambayo Papa amewashukuru na kuwatia moyo kwa sala. Baba Mtakatifu akiendelea amesema: “Mantiki ya pili ni ile ya uinjilishaji, ambayo pia ni, kwa kusema, kuwa ni kinasaba ( DNA) cha Harakati ya Karismatiki. Roho Mtakatifu, akikaribishwa ndani ya moyo na maisha, hawezi kujizuia kufunguka, kusonga, kufanya kutoka nje; Roho daima hutusukuma kuwasilisha Injili, kwenda nje, na anafanya hivyo kwa mawazo yake yasiyoisha.” Kwa upande wetu tunatakiwa kuwa wanyenyekevu na kushirikiana Naye, kama tunavyosimuliwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunavyoambiwa na Stefano, Filipo, Barnaba, Petro, Paulo na wengine. Hawa hawakuwa na mwongozo wa jinsi gani ya kuendelea, bali walikuwa ni Roho Mtakatifu aliyewasukuma na wakafanya mambo mengi makuu.” Papa amesisitiza na kuongeza: Na daima kumbukeni kwamba tangazo la kwanza linatolewa kwa ushuhuda wa maisha!”
Je kuna maana gani kufanya maombi marefu na nyimbo nyingi nzuri, ikiwa sijui kuwa na subira na jirani yangu, ikiwa sijui kukaa karibu na mama yangu aliye peke yake ambayo pia ni amri ya nne,” Papa amesisitza na kuongeza: “Ninachukizwa na wanaume na wanawake ambao wana wazazi katika makazi ya kutunza na hawaendi kuwatembelea, au kwa mtu huyo aliye shida ... Msaada wa dhati, huduma iliyofichwa kila wakati ni uthibitishaji wa tangazo letu. Kwa njia hiyo ni maneno, ishara na nyimbo, bila uthabiti wa upendo, ni bure,” Papa amesisitiza. Ni sala na uinjilishaji. Papa ameongeza “Lakini ikiwa mmekuja kwa Papa sio tu kuthibitishwa katika njia hizi mbili ambazo ni karama yenu na historia yenu. Mrithi wa Petro pia ana karama, ambayo ni ile ya umoja, na zaidi ya yote anaweza na lazima kuthibitisha. Ushirika awali na yote na maaskofu wenu. Mnajua vyema, katika kila Kanisa mahalia Harakari za kikanisa lazima daima zitafute ushirika wenye ufanisi. Na hii ina maana gani? Ina maana kwamba jumuiya ya Upyaisho lazima iwe katika huduma ya jumuiya nzima, jimbo, jumuiya nzima ya parokia, kulingana na maelekezo ya kichungaji ya Askofu.
Ushirika pia na ukweli mwingine wa kikanisa, vyama, Harakati, vikundi na kutoa ushuhuda wa udugu, kuheshimiana katika utofauti, ushirikiano katika kujitolea kwa mipango ya pamoja, katika huduma ya watu wa Mungu na pia juu ya masuala ya kijamii ambayo kuna hatari ya hadhi ya watu. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru kwa ahadi ambayo tayari wanajiwekea katika hilo na amewasihi wawe wajenzi wa ushirika, kwanza kabisa kati yao wenyewe na wawe makini na mazungumzo. “Umoja kati yenu, hii ni muhimu sana; na pia, umoja wa ndani ya harakati zenu, na kisha katika parokia na majimbo.” Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru tena kufika kwao. Amewaomba wandelee mbele kwa Furaa. Mama Maria awalinda, na daima awe katikati yao kama alivyokuwa katikati ya Mitume wa Kwanza katika karamu kuu (Mdo 1,14).
Papa Francisko kwa kuongezea ametoa ushuhuda wake binafsi kwamba : “Nilikuwa na historia maalum na ninyi, kwa sababu mwanzoni nilikuwa sipendi harakati, nilisema ni shule ya samba na sio harakati za kikanisa. Kisha kama Askofu Mkuu niliona jinsi walivyofanya kazi, na jinsi walivyojaza Kanisa kuu wakati wa mikutano na nilianza kuwa na shukrani kubwa kwenu. Endeleeni mbele, lakini si kama shule ya samba, bali kama harakati ya kikanisa.” Na kwa kuhitimisha Papa Francisko amewabariki kwa moyo na huduma yao. Amewaomba tafadhali wasali kwa ajili yake.