Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Januari 2024 amekutana na kuzunguza na vijana wakatoliki kutoka Jimbo kuu la Bari-Bitonto, lililoko Kusini mwa Italia Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Januari 2024 amekutana na kuzunguza na vijana wakatoliki kutoka Jimbo kuu la Bari-Bitonto, lililoko Kusini mwa Italia   (Vatican Media)

Sakramenti ya Kipaimara Inaimarisha Zawadi ya Ubatizo: Ushuhuda na Upendo

Papa katika hotuba yake amekazia kuhusu dhamana na wajibu wa waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara inayoimarisha zawadi ya Sakramenti ya Ubatizo. Amekazia umuhimu wa sala, ushuhuda na upendo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kukumbuka na kuadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wao inayowaingiza katika familia kubwa ya Mama Kanisa na kwamba, Roho Mtakatifu anaishi kati yao kwa daima, ili, kurithi maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanampokea Roho Mtakatifu anayewawezeshwa kufanywa wana wa Mungu; kwa kuunganishwa zaidi na nguvu za Kristo Yesu pamoja na kupata mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwasaidia kukamilika zaidi kama viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanajitoa sadaka na kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao! Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia: Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kristo Yesu anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao. Kwa njia ya Sakramenti hii, wabatizwa wanakamilishwa na hivyo kufanana na Kristo Yesu. Ni Sakramenti inayowaunganisha waamini kuwa viungo hai zaidi vya Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa. Utume wa Kanisa unapata asili na chimbuko lake kwa wale wote wanaofanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hakuna mtu awaye yote ndani ya Kanisa anayeweza kujigamba kwamba, Kanisa ni mali yake!

Sakramenti ya Kipaimara inaimarisha zawadi ya Ubatizo
Sakramenti ya Kipaimara inaimarisha zawadi ya Ubatizo

Kila mwamini anao wajibu wa kusaidiana na waamini wenzake katika mchakato wa kutakatifuzana, kusaidiana na kutaabikiana. Kila mwamini anayo dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa, lakini wote kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kristo linatoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wote wamefungwa pamoja katika kifungo cha upendo kati ya waamini, Askofu mahalia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanapokea zawadi ya amani, wanayopaswa kuwashirikisha pia majirani zao; kwa kuendeleza Injili ya upendo na mshikamano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu katika Kristo Yesu, huku wakitakiana mema! Wakristo wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani, umoja, mshikamano katika udugu wa kibinadamu. Sakramenti ya Kipaimara hutolewa mara moja tu na huchapa katika roho alama ya kiroho isiyofutika ambayo ni ishara kwamba, Kristo Yesu amemtia Mkristo alama ya mhuri wa Roho wake, kwa kumvika nguvu itokayo juu, ili aweze kuwa shuhuda wake kwa kutoa harufu nzuri ya utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Waamini wana dhamana ya kutangaza na kushuhudia imani yao
Waamini wana dhamana ya kutangaza na kushuhudia imani yao

Waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wanapaswa kutambua kwamba, wanawajibika kuwasaidia jirani zao kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kutoka katika uchoyo na ubinafsi wao, tayari kukutana na jirani zao, ili kwa pamoja, waweze kukua na kusaidiana katika kuziishi karama mbalimbali walizokirimiwa na Roho Mtakatifu, ili kuzaa matunda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo wote walioimarishwa kwa Roho Mtakatifu, kamwe wasimfungie Roho Mtakatifu katika ubinafsi wao; wasizime moto wa upendo uliowasha na Roho Mtakatifu, wala kuzuia upepo wa mageuzi unaovumishwa na Roho Mtakatifu. Ni katika muktadha wa Sakramenti ya Kipaimara, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Januari 2024 amekutana na kuzunguza na vijana wakatoliki kutoka Jimbo kuu la Bari-Bitonto, lililoko Kusini mwa Italia wanaotarajiwa kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, huku wakiwa wameandama na viongozi wa Kanisa, wazazi na walezi wao. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu dhamana na wajibu wa waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara inayoimarisha zawadi ya Sakramenti ya Ubatizo. Amekazia umuhimu wa sala, ushuhuda na upendo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kukumbuka na kuadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wao inayowaingiza katika familia kubwa ya Mama Kanisa na kwamba, Roho Mtakatifu anaishi kati yao kwa daima, ili hatimaye, kurithi maisha ya uzima wa milele.

Vijana wanaojiandaa kupokea Kipaimara Jimbo kuu la Bari-Bitonto
Vijana wanaojiandaa kupokea Kipaimara Jimbo kuu la Bari-Bitonto

Sakramenti ya Kipaimara inaimarisha zawadi ya Ubatizo na hivyo kumwezesha Roho Mtakatifu kuendelea kulipyaisha Kanisa kwa Mapaji yake na Kanisa liweze kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu na kwamba, kwa waamini hii ni dhamana inayotekelezwa katika ngazi ya mtu binafsi kama wadau wakuu wa Uinjilishaji na wala si watazamaji. Baba Mtakatifu amewasimulia kuhusu maisha ya Mwenyeheri Carlo Acutis, aliyeishi huko Milano, Kaskazini mwa Italia na hatimaye akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 15 tu. Katika kipindi hiki kifupi cha maisha yake, ametenda mambo makubwa, hasa kwa kukuza na kudumisha ibada na uchaji kwa Kristo Yesu; alikuwa gwiji wa matumizi ya internet kwa ajili ya huduma ya Injili, akakita maisha yake katika upendo kwa sala, ushuhuda wa imani na upendo kwa jirani. Mwenyeheri Carlo Acutis alitumia muda mwingi kwa ajili ya kuabudu Ekaristi Takatifu, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa upendo, changamoto kwa waamini wote. Waamini hawa wanaojiandaa kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wajiandae kikamilifu kwenda kwa Kristo Yesu, ili kushuhudia upendo wake wa daima, kwani anawapenda na kuwasubiri daima. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka vijana hawa kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Kristo Yesu na kwamba, inalipa kukaa na Kristo Yesu.  

Sakramenti ya Kipaimara
27 January 2024, 14:54