Tafuta

Mapadre wa Ufalme wa Kristo, Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Mapadre wa Ufalme wa Kristo, Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (Vatican Media)

Dumisheni Maisha na Wito wa Kipadre; Msimezwe na Malimwengu

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu: Maisha, wito na huduma ya Kipadre na kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu katika Ulimwengu mamboleo. Kwa vile wamewekwa wakfu, mwelekeo huu unaimarishwa zaidi na kukamilishwa na ule wa kieskatolojia. Watambue kwamba, wako ulimwenguni kwa ajili ya ulimwengu lakini wa si waulimwengu huu, wawe makini wasijitafute wala kumezwa na malimwengu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mapadre wa Ufalme wa Kristo lilianzishwa kunako mwaka 1953 na Padre Agostino Gemelli, takribani miaka 70 iliyopita. Leo hii, kuna wanashirika wengi kutoka Barani Afrika hasa ni wale wanaotoka nchini Guinea, Burundi, Rwanda na wengine ni wale wanaotoka nchini Ujerumani na Poland. Kwa sasa Shirika linajenga Kituo kwa ajili ya kumbukumbu ya Askofu mkuu Michael Courtney, Balozi wa Vatican nchini Burundi aliyeuwawa kikatili tarehe 28 Desemba 2003. Hiki ni kituo ambacho kimejengwa kwa muda wa miaka mitatu. Pamoja na mambo mengine, kitatumika kama shule ya ufundi hususan jinsi ya kuvuna maji ya mvua na kinalishwa na umeme wa jua!

Ufalme wa Mungu unatangazwa kwa njia na hali tofauti za waamini
Ufalme wa Mungu unatangazwa kwa njia na hali tofauti za waamini

Mapadre wa Ufalme wa Kristo, Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake amekazia kuhusu maisha, wito na huduma ya kipadre; Kama Mapadre wa Jimbo wanaitwa kushiriki kikamilifu karama ya Daraja Takatifu ya Upadre huku wakiwa na ushirika na Askofu pamoja na ndugu zao katika Kristo Yesu, mintarafu karama ya Mtakatifu Francisko; wawe makini ili wasitumbukie katika tabia ya kujipenda na kuyapenda malimwengu! Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu maisha, wito na huduma ya Kipadre na kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu katika Ulimwengu mamboleo. Kwa vile wamewekwa wakfu, mwelekeo huu unaimarishwa zaidi na hatimaye, kukamilishwa na ule wa kieskatolijia. Ndani ya Kanisa kila mtu aliyebatizwa, yuko Ulimwenguni na ni kwa ajili ya Ulimwengu, lakini si wa Ulimwengu huu. Kumbe, waamini walei na makleri, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu kwa njia tofauti tofauti, kadiri ya hali, maisha na utume wao.

Mapadre wasitumbukie katika tabia ya kupenda malimwengu
Mapadre wasitumbukie katika tabia ya kupenda malimwengu

Na Mapadre wanajitambulisha kikamilifu katika shamba la Bwana kama Wamisionari wa Ufalme wa Kristo huku wakishiriki kikamilifu katika Upadre, katika ushirika na Askofu pamoja na ndugu zao watawa na kwamba, Shirika hili linawasaidia kutekeleza haya yote mintarafu karama ya Mtakatifu Francisko wa Assisi inayofumbatwa katika unyenyekevu na udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya huduma na sadaka ya uwapo na ukarimu, kwa kujisadaka tayari kujenga mafungamano na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, katika Ufalme wa Kristo Yesu, wao ni wamoja kama anavyoshuhudia Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Unyenyekevu na udugu wa kibinadamu!
Unyenyekevu na udugu wa kibinadamu!

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre hawa kujenga mshikamano na urafiki na watu wa Mungu; wawe ni Mitume wa huruma na ukweli, ili Injili ya Kristo Yesu iwe ni moyo wa Ulimwengu. Hiki ni kiini cha nadhiri zao zinazothibitishwa katika utume na ubinadamu wake Kristo Yesu pamoja na fadhila ambazo Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamezithibitisha kwa kuzitaja kuwa ni: Uaminifu, heshima kwa haki, Uaminifu kwa Neno wa Mungu; wema, busara, uthabiti wa akili, kufikiri na unyoofu. Rej. Optatam totius, 1. Baba Mtakatifu Francisko amewataka wawe makini ili wasitumbukie katika tabia ya kujipenda, kujitafuta na kuyapenda malimwengu, kwa sababu huko kuna “kilio na kusaga meno.” Kumbe ni vyema kuwa na mang’amuzi ya kutosha ili kuomba msaada wa neema na baraka za Mungu.

Maisha na utume wa Mapadre
11 January 2024, 15:42